Na Andrew Chale, Dar es Salaam
SPIKA
wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson
amemuapisha Balozi Mahmoud Thabit Kombo kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania katika ofisi ndogo za Bunge, jijini Dar es
Salaam.
Balozi Kombo
ameapishwa leo Alhamisi Julai 25, 2024, Ofisi hizo huku akiambatana na
familia yake, sambamba na kusindikizwa na Wabunge kadhaa pamoja na
maafisa wa Bunge n wale wa ofisi ya Mambo ya Nje tukio lililoshuhudiwa
na Waandishi wa Habari mbalimbali.
Julai
21, 2024 Balozi Kombo alipoteuliwa kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Rais Samia Suluhu Hassan,
kuchukua nafasi ya January Makamba ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
Katika
tukio hilo, Dk. Tulia amempongeza kwa kuaminiwa na Rais Samia Suluhu
Hassan na kupewa nafasi ya ubunge, huku akisema zipo chache hivyo yeye
kuwa miongoni mwao ni heshima kubwa.
"Tukio
hili ambalo tumelikamilisha hapa ni kiapo cha uaminifu ambacho
kinamfanya Balozi Kombo kuwa mbunge kwa matakwa ya ibara ya 68 ya Katiba
ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na kwa mujibu wa kanuni za Bunge za
kudumu.
"Kanuni ya 30
fasili ya kwanza ambayo inaeleza kabla ya mbunge kuanza kushiriki kanuni
za Bunge lazima ale kiapo cha uaminifu mbele ya Spika,” amesema Dk
Tulia.
Amesema fasili
ndogo ya 2(b) inaleza mbunge ataapishwa na Spika kwa mujibu wa eneo
ambalo litapangwa na Spika huku akisema awali kulikuwa na changamoto
jambo ambalo lilifanya kanuni zibadilishwe.
“Tulilazimika
kutoa ufafanuzi huu kila wakati ili watu wasione kwa nini wabunge
wengine wanaapishwa bungeni wengine nje ya Bunge, kanuni zetu zinaruhusu
hayo mazingira na Spika akiagiza wapi kiapo kitafanyika hapo, leo
tumefanyia ofisi ndogo za Bunge hapa Dar es Salaam lakini ingeweza
kufanyika sehemu nyingine yoyote,” amesema Dk Tulia.
Dk
Tulia amesema anaamini Balozi Kombo na wengine walioteuliwa watakwenda
kufanya kazi na kuendeleza mipango ambayo imewekwa wazi na Rais ikiwemo
uhusiano wa kimataifa na Afrika Mashariki.
Mhe Balozi Kombo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia.
No comments:
Post a Comment