August 15, 2024

Rais Dkt. Samia kukutana na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma Agosti 27 jijini Arusha

Katika kinachoonekana kuwa ni juhudi za kuhakikisha Mashirika na Taasisi za Umma zinafanyakazi na kutoa tija chanya, Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) inayosimamia taasisi na mashirika hayo, imekuja na mpango mkakati wa mashirika yanayoimarika kiuchumi yaanze kuwekeza nje ya Tanzania.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.


Bila shaka Ofisi ya Msajili wa Hazina chini ya Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu, imekuja na mkakati huo kwa lengo la kuhakikisha yale taasisi na mashirika yanayochechemea yachechemke na yanayoinuka kiuchumi yaimarike zaidi, hivyo kuchangia vilivyo uchumi wa Taifa.

Taarifa zinaonyesha hadi sasa Msajili wa Hazina anasimamia mashirika 248 ya Umma,  kati yake 81 yakiwa ya biashara na 167 yasiyo ya kibiashara, huku  serikali ikiwa na hisa 56, za ndani 46 na za nje kumi (10) na yaliyobinafsishwa 341.

Pamoja na jitihada kubwa anazoonekana kufanya Msajili wa Hazina, mwaka huu (2024) kati ya mashirika 304, ni mashirika 145 yaliyotoa gawio kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, ambalo lilikuwa Sh. Bilioni 637 wakati 159 hayakutoa kabisa.

Mwaka huu (2024) kuna ongezeko la mashirika yaliyotoa gawio, ambapo jumla ya mashirika 109 yaliyotoa gawio, na hivyo kufanya ongezeko la mashirika 36 yaliyotoa gawio hilo mwaka huu ikilinganishwa na mwaka jana 2023.

Licha ya ongezeko hilo,  Mchechu anasisitiza kuwa bado kiwango hicho siyo cha kuridhisha, ni hali mbaya. Na anaposema ni hali mbaya bila shaka anamaanisha bado maboresho yanahitajika, maana inafikirisha sana, Inakuwaje iwe kati ya mashirika 304, mashirika 248 ambayo Serikali ina hisa nyingi yatoe gawio kidogo wakati mashirika 56 ambayo ina hisa chache ndiyo yaongoze kutoa gawio kubwa!

Kwa kauli ya Mchechu, taswira hiyo ni somo ambalo Serikali ina kila sababu ya kujifunza namna taasisi zake zinavyoendeshwa, kwa sababu uwekezaji wa Serikali katika kampuni na mashirika hayo ni Sh. 3 trilioni. Kwa jumla, Serikali imewekeza Sh. 76 trilioni kwenye mashirika na taasisi mbalimbali.

Kwa mujibu wa Mchechu, mwaka 2019/2020, 2020/2021 na 2021/2022 Mashirika ya Umma yalichangia Sh. 255 Bilioni, Sh. 161 Bilioni na Sh. 207 bilioni, mtawalia, huku Kampuni na Mashirika ambayo Serikali ina hisa chache yakichangia gawio dogo la Sh. 44 bilioni, Sh. 147 bilioni na Sh. 10 Bilioni mtawalia.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo


Lakini anasema, kwa miaka miwili 2022/2023 na 2023/2024 Gawio kwa mashirika ya umma yanayofanya biashara lilikuwa Sh. 109 bilioni na Sh. 110 bilioni mtawalia; huku ambako Serikali ina hisa chache yakichangia Sh. 219 bilioni na Shs. 168 bilioni kwa kipindi hicho.

Sasa kutokana na kinachoonekana kwamba sehemu ya sababu ya kutofanya vizuri kwa Mashirika na taasisi kadhaa pengine ni kutojitambua kuwa wana wajibu wa kufanyakazi zinazolipa kulingana na uwekezaji wa matrilioni ya fedha uliofanywa na serikali, kutozingatia sawasawa kwamba mashirika hasa yale ya kibiashara yanatakiwa yawe na ubunifu ili kuwa na sura ya kibiashara kwelikweli.

Bila shaka ni sababu hizo na nyininezo ndizo zinaonekana zimemsukuma Msajili wa Hazina kuibua mkakati mahsusi wa mashiri yale yenye hali njema kiuchumi yaaze kuwekeza nje ya Tanzania ili uwe msukumo kwa taasisi na mashirika yote ya umma kupambana kuelekea kuwekeza nje ya Tanzania.

Hata hivyo, kuibua mkakati huo na kuzipa taasisi na mashirika kuukabili haitoshi, ni lazima itengenezwe mbinu itakayosaidia kuzifanya mkakati huo uingine vichwani na kuona kuwa hakuna namna nyingine mbadala itakayovusha kutoka kwenye kudumaa kwenda kunakotaakiwa.

Bila shaka kwa kutambua hilo, ndiyo maana Msajili wa Hazina amepanga jukwaa la Kikaokazi (CEO Forum) cha Wenyeviti wa Bodi, Watendaji Wakuu wa Taaasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali, ili 'wajifungie' ukumbini na kutoka wakiwa wmeiva juu ya kile serikali inachokitaka wakifanye.

Kwa mujibu wa Mchechu Kiikaokazi hicho kitaperuzi kw kina maeneo muhimu ya kufanyiakazi kutokana na maazimio yaliyojiri katika kikao kazi cha kwanza kama hicho cha CEO Forum kilichofanyika mwaka jana (2023).

Akizungumza na Wahariri, Julai 15, 2024 jijini Dar es Salaam, Mchechu alisema kikaokazi hicho kitafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa (AICC) mwezi huu wa Agosti 2024, kikikutanisha  wajumbe (Watendaji Wakuu wa Taaasisi, Mashirika ya Umma na Wenyeviti wa Bodi) zaidi ya 600.

Wakati huo, Mchechu alisema tarehe ya kufanyika kikaokazi hicho ingetangazwa baadaye na sasa tarehe hiyo imekwishatangazwa ikiwemo kwenye Tovuti rasmi ya Ofisi ya Msajili wa Hazina, kwamba kitafanyika kuanzia tarehe 27 hadi 30 Agosti, 2024 na kitafunguliwa kwa kishindo na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Bila shaka kikaokazi kimepewa umuhimu wa kufunguliwa na Rais mwenyewe ili akutane uso ka uso tena na Wenyeviti wa Bodi, Watendaji Wakuu wa Taaasisi, Mashirika ya Umma na Wakala za Serikali ili awe na wasaa mwingine mzuri wa kuwashikisha vilivyo nira yake juu ya anavyotaka uendeshaji wenye tija wa Tasisi na mashirika ya umma.

Siwezi kukisia, lakini hapana shaka Mheshimiwa Rais atawafunda kwa kina wajumbe hadi wajue na kushika vilivyo dhima iliyopo mbele yao juu ya taasisi na mashirika wanayosimamia, na pia kuwawekea wazi tena muktadha na faida ambayo taifa litavuna kupitia taasisi na mashirika kuitia kuwekeza nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Mchechu, Serikali imedhamiria taasisi na mashirika ya umma kuwekeza nje ya Tanzania kwa sababu hatua hiyo itaongeza wingo wa Taasisi hizo kukua kiuchumi hivyo kukuza pato la taifa kwa uhakika na kwa uendelevu sanjari na kuifanya Tanzania kushiriki vilivyo katika Diplomasia ya Uchumi.

Mashirika ambayo kwa sasa yana sifa ya kuwekeza nje ya Tanzania Mchechu anayataja kuwa ni yale ambayo mazingira yake ya kiutendaji yanaruhusu kama Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na Shirika la Reli Tanzania (TRC), huku akitaja sifa za Taasisi kuwa ni uwezo wake kukua kiuchumi kama Benki za NMB, CRDB na TCB.

Mchechu anasema, wakati Serikali ikiwa katika mikakati ya mashirika na taasisi zake kuwekeza nje ya nchi, pia inaendelea kufanya maboresho ya kimsingi kuhakikisha umadhubuti wa kutosha unakuwepo katika mashirika na taasisi zote.

Katika kuboresha na kuimarisha, kwa mujibu wa Mchechu hatua mbalimbali zinaendelea  kufanyika ikiwemo kuhakikisha Wakuu wa Taasisi na Mashirika wanakuwa wenye uwezo unaokidhi, na katika kufanya hivyo wakuu watakaoonekana hawakidhi wataondolewa, sanjali na hivyo, taasisi na mashirika yatapewa uwanja mpana wa kujisimamia katika uendeshaji, badala ya kusimamiwa na serikali.

“Katika kufanya hivi, baadhi ya mashirika au taasisi kama hazifanyi vizuri zitavunjwa na majukumu yake kuhamishiwa kwingine na taasisi ambazo shughuli zake zinafanana zitaunganishwa au kubadilishiwa majukumu”, anasema Mchechu.

Mchechu anasema, katika kuhakikisha Taasisi na Mashirika ya Umma yanakomaa kiuchumi, sasa jukumu la kuchangia mfuko wa taifa litakuwa ni la lazima kwa kila Taasisi na Shirika na fedha za uchagiaji lazima zitokane na mapato ya Taasisi au Kampuni husika siyo vinginevyo.

Kwa muktadha huo maana yake ni kwamba ili taasisi au shirika liweze kumudu ulazima huo kuchangia gawio kutoka kwenye mapato yake itakuwa lazima kuchapakazi kwa juhudi na maarifa na kuivaa vilivyo ya Mikakati ya serikali juu ya Taasisi na Mashirika ya Umma Kuwekeza Nje ya Tanzania, ambayo ndiyo kaulimbiu itakayoangaza kikaokazi cha CEO Forum cha Agosti 27, 2024 jijini Arusha.

Kulingana na tafsiri ya kaulimbiu hiyo, ni kwamba Kikao kazi hicho kitalenga kwenda kuhimiza taasisi na mashirika ya umma kuangalia zaidi fursa za kuwekeza au kupanua wigo wa huduma nje ya Tanzania.

Maana kwa mujibu wa Mchechu kikaokazi hicho kitajadili fursa za kikanda na kimataifa kwa ajili ya Taasisi na Mashirika kuwekeza nje ya nchi sanjari na kupata uzoefu wa kiutendajikazi kutoka kwa wataalamu wa ndani na nje ya nchi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi.

“Uboreshahi wa mitaji ya Mashirika haya ni kupelekea ujuzi na utendaji kazi katika ushindani, na kuweza Kubadilisha mitazamo na kufanya Taasisi na Mashirika hayo kuwa vichocheo vya maendeleo ya kiuchumi.

Tunatakiwa kukumbuka mambo muhimu ambayo Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wanapaswa kuzingatia katika usimamizi wa utendaji kazi ikiwemo miongozo mbalimbali ya Uendeshaji wa Mashirika ya Umma na umuhimu wake katika kutekeleza malengo ya Serikali kwa ufanisi", nasema Mchechu.

Mchechu anasema, kikao hicho kitaenda kutatua changamoto zilizopo katika uendeshaji wa Taasisi na kuweza kuainisha mikakati iliyopo, na kwamba katika kikaokazi hicho taasisi zinazofanya vizuri katika nyanja mbalimbali za utendaji kazi zikiwemo kutengeneza faida na kufanya mageuzi ya utendaji na hivyo kuboresha utoaji wa huduma zitatambuliwa na kupewa tuzo.

RAIS SAMIA
Katika kuonyesha kuwa Rais Dk. Samia ana dhamira ya kuhakikisha usimamizi wa Mashirika na taasisi za umma unakuwa imara zaidi Juni 11, 2024 alitoa kauli 'nzito' kwa Msajili wa Hazina Mchechu na Waziri wa Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo wakati akipokea Gawio la Serikali kutoka kwa Mashirika ya Umma na Taasisi ambazo Serikali ina hisa kidogo.

“Kwenye mageuzi haya Mchechu na Waziri wako lazima muwe 'unpopular'. Sijawahi kusikia Waziri wa Fedha akasifiwa hata siku moja, siku zote Waziri wa Fedha analaaniwa, kwahiyo Mchechu na wewe utalaaniwa tu hapa, na lawama nyingine zitakuja 'personal', nyingine kikazi, lakini hii ndiyo kazi niliyokupa, simama na ifanye,” akasema Rais Dk. Samia.

Rais Samia, alitoa kauli hiyo wakati akirejelea takwimu zilizotolewa siku hiyo wakati anapokea gawio la jumla ya Sh. 637,122,914,887.59 ikijumuisha gawio la Sh. 278,868,961,122.85 kutoka katika mashirika ya biashara na michango Sh. 358,253,953,764.74 kutoka katika taasisi nyingine, yakiwa ni makusanyo kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Mei 2024.

Kushajihisha kauli aliyowapa Mchechu na Prof. Mkumbo Rais Dk. Samia aliweka wazi kwamba ndiyo maana ndiyo sababu yeye binafsi anatukanwa sana mitandaoni, lakini amejigeuza chura anajifanya hasikii na wala hatojibu bali anachotaka yeye ni mageuzi ya kiuchumi ili kuipeleka Tanzania mbele.

Sanjari na hilo Rais Samia akatoa mifano ya jitihada zake namna zinavyozaa matunda, huku Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ambayo wengi walimbeza na kuzua taharuki alipokaribisha uwekezaji wa Kampuni ya DP World kutoka Dubai, ikiwa kinara katika ongezeko la gawio mwaka huu (2024).

"Wale waliopiga kelele Mama kauza bahari, Mama kauza bandari, Mama kauza nini - mauzo yale faida yake ni hii leo (TPA kuongeza mapato). Huu ni mwanzo, tunatarajia mtapata faida kubwa zaidi kwa bandari zetu kubwa zote ambazo ziko nchini," akasema Rais Dk. Samia katika hafla hiyo ya kupokea Gawio.

Katika utoaji Gawio TPA iliongoza kundi la taasisi zisizo za biashara lilonajumuisha Mashirika ambayo kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina na Sheria ya Mashirika ya Umma zinawajibika kutoa michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi baada ya kutoa gawio la Sh. bilioni 153.9.

TPA iliifuatiwa kwa mbali mno na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliyotoa Sh. bilioni 34.7, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) iliyotoa Sh. bilioni 21.3, Wakala wa Huduma za Meli (TASAC) iliyotoa Sh. bilioni 19.1, na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) uliotoa Sh. bilioni 18.9.

Kwa kundi la taasisi za kibiashara linalojumuisha Mashirika na Kampuni ambazo kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma na Sheria ya Makampuni, zinawajibika kutoa gawio kwa wanahisa, Benki ya NMB ndiyo iliyoongoza kwa kutoa Sh. bilioni 54.5, ikifuatiwa na Twiga Minerals (ya ubia baina ya Serikali na Barrick Gold) iliyotoa Sh. bilioni 53.4, Airtel Tanzania (Sh. bilioni 40.8), Puma Energy (Sh. bilioni 12.2), na Kiwanda cha Sukari cha TPC Moshi kilichotoa Sh. bilioni 10.2.

Licha ya kumkabidhi Msajili wa Hazina kuhakikisha anayasimamia Mashirika ya Umma na Taasisi kuleta mabadiliko chanya, Rais Dk. Samia alionya wale ambao watathubutu kumkera kwa kumkanyagia uchumi wake anaoupambania, akisema; “Anayetaka kunikera anikanyagie uchumi wangu. Kwenye mageuzi haya wapo wengi watakaokanyagwa na kupiga kelele nyingi, lakini msikate tamaa, kachapeni kazi,”

Katika muktadha huo Rais Dk. Samia akasisitiza, ataendelea kusimamia mageuzi katika uendeshaji wa Mashirika ya Umma ili kuyawezesha kujiendesha kibiashara na kwa tija zaidi kwa manufaa ya Watanzania na Jukumu hili la usimamizi liko chini ya Msajili wa Hazina na akayasihi mashirika ya Serikali kujiangalia upya katika utendaji kazi wao ili waweze kutoa gawio kwa Serikali.

Ni wazi kwamba, upokeaji gawio ni ishara kuwa mazingira yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia yanafanya kazi na kuwezesha kupatikana kwa fursa ya kufanya bishara na kupata faida.

Miongoni mwa mazingira ni kuwekwa wazi majukumu ya Msajili wa hazina kishria ikiwemo kwamba analo jukumu kisheria katika kusimamia mageuzi kwenye mashirika ya umma.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 8(f) cha Sheria ya Mamlaka na Majukumu ya Msajili wa Hazina SURA 370, ikisomwa pamoja na Kifungu cha 11(3) cha Sheria ya Fedha za Umma SURA 348 vimeweka wajibu kwa Wakala wa Serikali, Mashirika na Taasisi za Umma kuchangia asilimia 15 ya mapato ghafi katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Pia, kifungu cha 7 cha Sheria ya Mashirika ya Umma SURA 257, pamoja na mambo mengine, kimeelekeza Mashirika ya Umma kujiendesha kwa misingi thabiti ya kibiashara na kupata rejesho la mtaji lisilopungua asilimia 5, na kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

Halikadhalika, Sheria ya Mamlaka na Majukumu ya Msajili wa Hazina, kifungu cha 10(2)(i) kinatoa wajibu kwa Msajili wa Hazina kufuatilia na kuhakikisha michango na gawio kutoka katika Mashirika ya Umma inalipwa kwa wakati.

Na kifungu cha 10A(1) cha Sheria ya Mamlaka na Majukumu ya Msajili wa Hazina kimeweka masharti ya mashirika ya umma kupunguza matumizi ambapo mashirika hayo yanatakiwa kutumia siyo zaidi ya asilimia 60 ya mapato baada ya kutoa gharama ya mishahara na bakaa inayopatikana baada ya matumizi hayo kuwekwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali.

HALI MBAYA YA GAWIO
Nikirejea nilivyoandika mwanzo, pamoja na jitihada kubwa anazofanya Msajili wa Hazina, ukweli ni kwamba bado hali siyo nzuri kwa Mashirika na Taasisi za Umma kwa sababu Mchechu anasema, mwaka huu (2024) kati ya mashirika 304, ni mashirika 145 tu yaliyotoa gawio la Sh. bilioni 637 kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali ilhali mashirika 159 hayakutoa kitu kabisa.

Japokuwa mwaka huu (2024) kuna ongezeko kidogo la mashirika yaliyotoa gawio, ikilinganishwa na mwaka mwaka jana 2023 ambapo jumla ya mashirika 109 ndiyo yaliyotoa gawio, na hivyo mwaka huu kuwa ongezeko la mashirika 36, Mchechu anasisitiza kuwa bado ni hali hiyo haitoshi kuridhisha, ni mbaya.

Miongoni mwa jambo la kutafakari na kufanyiwa kazi kubwa na Msajili wa Hazina kwa kunoa zaidi rungu lake la kusimamia maboresho kwenye Mashirika ya Umma, ni kwamba wakati katika mashirika 304, mashirika 248 ambayo Serikali ina hisa nyingi yanatoa hisa chache wakati mashirika 56 ambayo Serikali ina hisa chache ndiyo yaliyoongoza kwa kutoa gawio kubwa!

Mchechu anasema taswira hiyo ni somo ambalo Serikali ina kila sababu ya kujifunza namna taasisi zake zinavyoendeshwa kwa sababu uwekezaji wa Serikali katika kampuni na mashirika hayo ni Sh. 3 trilioni. Kwa ujumla, Serikali imewekeza Sh. 76 trilioni kwenye mashirika na taasisi mbalimbali.

Anasema, mwaka 2019/2020, 2020/2021 na 2021/2022 Mashirika ya Umma yalichangia Sh. 255 bilioni, Sh. 161 bilioni na Sh. 207 bilioni, mtawalia, huku Kampuni na Mashirika ambayo Serikali ina hisa chache yakichangia gawio dogo la Sh. 44 bilioni, Sh. 147 bilioni na Sh. 10 bilioni mtawalia.

Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu

Lakini anasema, kwa miaka miwili 2022/2023 na 2023/2024 Gawio kwa mashirika ya umma yanayofanya biashara lilikuwa Sh. 109 bilioni na Sh. 110 bilioni mtawalia; huku ambako Serikali ina hisa chache yakichangia Sh. 219 bilioni na Shs. 168 bilioni kwa kipindi hicho.

“Matokeo haya kwetu yanaleta fikra mchanganyiko, ni habari njema kwa kuwa inaonyesha uwezeshaji unaofanywa na Serikali kuendeleza mazingira wezeshi ya biashara, kampuni binafsi inapofanya kazi na kupata faida, mazingira ni mema,” anasema Mchechu.

Anasema, faida katika biashara ya sekta binafsi ni kipimajoto cha mafanikio ya Serikali kuboresha mazingira ya biashara na sera za kiuchumi huku akiwataka viongozi waliochaguliwa kuongoza mashirika ya umma kufanya vizuri zaidi kwa faida ya Taifa na wananchi.

“Kama tutazingatia Sh. 850 bilioni mwaka hadi mwaka inawezekana tukawa na furaha, lakini kama tutaangalia kiwango hiki tunachotoa sasa kwa malengo tuliyopatiwa tukiwa Arusha ya mapato yasiyo ya kikodi yafikie asilimia 10 ya kikodi tuko mbali sana, mwaka jana tulikuwa asilimia tatu na mwaka huu tupo asilimia tatu,” akasema.

Mchechu anasema ni lazima ukuaji uwe wa wastani wa asilimia kati ya 60 hadi 70 ili kufikia malengo ya mapato yasiyo ya kikodi kwa asilimia 10.

“Hali si nzuri kwa sababu bado hatuendani na kasi na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuleta maendeleo kwa kasi nchini, maendeleo yote yanategemea fedha, chanzo cha fedha ni vitu vitatu, Serikali kukopa, kukusanya kodi au kupata mapato yasiyo ya kikodi. Asilimia 90 ya mapato yasiyo ya kikodi hupatikana kupitia gawio,” anasema.

Akieleza baadhi ya mafanikio ambayo Ofisi ya Msajili wa Hazina imeyapata Mchechu anasema, imeendelea kushawishi kufanyika kwa mabadiliko katika sheria yake ili kuanzishwa kwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma, muswada ambao ulipelekwa Bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza Novemba 10, 2023.

“Ni wazi kuwa tunahitaji sheria inayojitosheleza itakayoweza kusaidia kuleta tija katika uwekezaji mkubwa wa zaidi ya Shs. 76 trilioni uliofanywa na Serikali kwa niaba ya Umma wa Watanzania,” akasema Mchechu.

Mchechu anasema, katika kuimarisha utawala bora na tija ya mashirika ya umma, Ofisi ya Msajili imezindua na kuanza kutumia mfumo wa kidijitali wa kufanya tathmini ya bodi hali ambayo imewezesha kukamlisha tathmini kwa wakati na kwa mawanda tarajiwa.

Anasema, Ofisi imeanza kutumia vigezo vipya vya uendeshaji wa mashirika (Key Performance Indicators) vilivyoingiwa kwa njia ya mikataba baina ya wenyeviti wa Bodi na Msajili wa Hazina, vigezo ambavyo vimeboreshwa zaidi na vimezingatia mgawanyo wa kisekta na majukumu ya msingi ya taasisi.

“Tupo katika hatua za mwisho za kuwa na mfumo thabiti wa kuripoti (dashboard) taarifa za kiutendaji za wakuu wa taasisi kwa wakati na za kuaminika ili kuwezesha kufanyika maamuzi sahihi kwa wakati (informed decision making) kwa mamlaka za uteuzi.

Ofisi pia imefanikiwa kupitia mikataba mbalimbali ya kibiashara na pia kufanya mazungumzo na wabia wetu kwenye sekta nyeti za uchumi; kwenye sekta ya madini kumekuwa na mzungumzo mbalimbali tukishirikiana na Wizara ya Madini na tumeweza kuongeza hisa za serikali katika baadhi ya kampuni, mathalani, tumeongeza hisa za serikali katika kampuni ya madini ya Sotta kutoka 16% hadi 20%, jambo litasaidia sana katika majadiliano ya mikataba mingine ambayo tupo katika mazungumzo.

Pia tumekamilisha majadiliano na kuingia mikataba mipya ya wanahisa na makampuni kama NMB, NBC na MCCL kati ya mikataba mingi inayofanyiwa kazi, na kampuni ya MCCL imeweza hatimaye kupata faida mwaka huu na kutoa Gawio kwa wanahisa mwaka huu baada ya kipindi cha miaka 10,” akafafanua Mchechu.

PROF MKUMBO.
Katika hafla hiyo ya utoaji Gawio, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, naye alisema miongoni mwa mambo wanayosimamia ni mchango wa taasisi kwenye uchumi kuhakikisha unaongezeka na kupunguza mzigo kwa Serikali unaotokana na kuhudumia taasisi hizo.

“Hapa Rais ni pagumu pia kwa sababu ulituelekeza tufanye tathmini ya mashirika ya umma ili yale ambayo yamepitwa na wakati tukushauri uyafute na mengine tuyaunganishe, tumefanya kazi hiyo kwa awamu ya kwanza tunaenda kuunganisha mashirika 16 na mengine manne yanaenda kufutwa,” akasema Prof. Mkumbo.

Prof, Mkumbo akasema, hilo ni gumu kwa kuwa alinyooshewa vidole kuwa anakwenda kuua mashirika ya umma, lakini akasisitiza kuwa, mashirika yatakayounganishwa, wenyeviti wa bodi ama mmoja atabaki au wote wataondoka na haiwezekani wote wawili wafanye kazi.

“Mashirika hayo ndiyo yanafanya kazi na mashirika binafsi, hivyo kuwa na mashirika ambayo hayaangalii biashara vizuri, mazingira ya biashara yatakuwa magumu,” akasema.

Katika kuwapa shime, Rais Dk. Samia aliwataka wachape kazi na akahimiza viongozi wa mashirika, wakiwemo wenyeviti na wakurugenzi wa Bodi, kusimamia mashirika ili mwakani zipatikane fedha nyingi zaidi.

Akasema, licha ya mashirika mengi kutopeleka gawio serikalini, kuna mageuzi ambayo yanafanyika huko na akawaagiza Wenyeviti wa Bodi kuyasimamia mashirika hayo.

Akarudia onyo lake kwa viongozi wa Wizara wenye mashirika, kwamba waache kuagiza fedha kutoka kwenye mashirika hayo na kuwataka wawe wabunifu kuangalia vyanzo vya fedha ili wakuze mashirika hayo.

Akawataka kufanya kazi ili kukuza mashirika yao kutokana na serikali kuweka mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao na si kubaki nyuma huku akisisitiza kwamba, mageuzi kwenye mashirika lazima yaendelee ili kuendelea kukuza uchumi ambapo nchi itafanyiwa tathmini ya uchumi wake ili kuingia uchumi wa kati.

No comments:

Post a Comment

Pages