Rais
Samia Suluhu Hassan (kushoto) akipata maelezo kutoka kwa Afisa Mtendaji
Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna alipotembelea banda la NMB kwenye
kilele cha Maonesho ya Nanenane Nzuguni jijini Dodoma. Benki ya NMB ni
miongoni mwa wadhamini wakuu kwenye maonesho hayo yaliyofika kilele chake
Agosti 8, 2024 ambayo ni sikukuu ya wakulima nchini.
Mwandishi Wetu, Dodoma
BENKI
ya NMB imepandisha kiwango cha mikopo kwa wakulima na wafugaji kutoka
Shilingi Bilioni 730 mwaka 2021 hadi Shilingi Trilioni 1.6 mwaka huu
2024 huku ikiweka mkakati wa kuinua sekta hiyo.
Kutolewa
kwa mikopo hiyo kumesaidia kupunguza migogoro ya wakulima na wafugaji
kwani kiasi cha Shilingi bilioni 505 ni mikopo ya wafugaji kwa lengo la
kunenepesha mifugo na kuboresha maeneo ya malisho kwa kundi hilo.
Akizungumza
mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan
leo Agost 8,2024, Mtendaji Mkuu wa NMB Ruth Zaipuna amesema kutolewa
kwa mikopo hiyo ni sehemu ya mkakati wa benki katika kuunga mkono sera
nzuri za Serikali ya awamu ya sita.
Takwimu
hizo zimemfurahisha Rais Dk Samia Suluhu Hassan na akiwa kwenye banda
la maonyesho la NMB amesema ‘Kazi Iendelee’ kauli ambayo huitumia
anapokubaliana na jambo hasa kwenye miradi ya maendeleo.
“Mheshimiwa
Rais tunakupongeza sana katika maoni yako hasa ya kuwainua wakulima na
wafugaji nchini, na sisi NMB tunayo mikakati ya kusaidia sekta ya kilimo
na mifugo ambako tumeona kuna mapinduzi makubwa,” amesema Zaipuna.
Mtendaji
Mkuu ameeleza kuwa kati ya mikopo iliyotolewa,Shilingi bilioni 450
zimetolewa kwenye mpango wa riba nafuu ya asilimia 9 ambako ndiko waliko
wakulima na wafugaji.
Zaipuna
amesema benki hiyo imeanzisha mkakati maalumu wa kuwafikia wakulima na
wananchi kupitia mpango wake wa kufungua akaunti za Shilingi 1000 ambako
mamilioni ya Watanzania wamejiunga huko hivyo kuwawezesha wananchi
kupata mikopo kwa urahisi.
“Mheshimiwa
Rais akaunti hii imerahisisha wananchi na wakulima kupata mikopo kwa
njia ya mtandao (Mkopo fasta) bila kuweka foleni benki na mikopo hiyo
inaanzia kiasi cha Shilingi 1000 hadi Shilingi milioni moja,” amesema.
Kiongozi
huyo amemwambia Rais kuwa benki hiyo itaendelea kushirikiana na
Serikali katika kukuza maono na wametumia maonyesho ya wakulima Nane
Nane kutoa elimu ya fedha ambako wananchi wamekuwa na mwitikio mkubwa.
No comments:
Post a Comment