Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama cha Mapinduzi kimesema kuwa kinaenda kuwasimamia maWaziri walioteuliwa na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi kutekeleza Ilani ya chama hicho katika kushughulika na shida za wananchi.
Akizungumza na wanahabari ofisi za CCM, Kisiwandui mara baada ya Rais Dkt. Mwinyi kutangaza baraza la mawaziri, Ikulu Zanzibar 13 Oktoba 2025, Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Zanzibar Idara ya Itikadi Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto Khamis alisema mawaziri na manaibu wao lazima wawe na msaada kwa Rais.
Alisema chama ndio kimeitafuta serikali wananchi wamekiamini na wakakipa ushindi hivyo lazima kiwasimamie mawaziri hao na kumshauri Rais pale ambapo mambo yatakuwa hayaendi sawa.
"Rais aliagiza na sisi tunasisitiza kuwa wateule hao ambao wanaapishwa leo Jumamosi kuwa watoke waende kwa wananchi na sio kubaki ofisini na kusubiri semina na mikutano ya ndani" alisema Mbeto.
Alisema Ikulu kuna chombo kwa ajili ya kusimamia watendaji wa serikali nao wanatakiwa kuwajibika ipasavyo na sio kusubiri kufanyia watu uchunguzi wakati wa uteuzi kisha kuanza kutoa sababu zingine za kutengeneza hivyo watafanya ya kwao nasi wenye Ilani tutafanya ya kwetu.
Mbeto alibainisha kuwa kuundwa kwa wizara mpya inayojitegemea ya Vijana, Uwezeshaji na ajira kunaenda kutimiza lengo la ajira 350,000 kwa vijana.
"Kote tulikopita tukikiombea chama kura wakati wa kampeni, changamoto kubwa tuliyokutana nayo ni ajira na uwezeshaji hususan kwa vijana hivyo tuna amini tatizo hilo linaenda kushughulikiwa na lengo linafikiwa" alisema.
Mwenezi Mbeto alisema wizara nyingine inayoenda kutoa majibu ya ajira kwa vijana katika uchumi wa kidigitali anaoujenga Dkt. Mwinyi ni Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia na Ubunifu.
Aliwataka mawaziri na manaibu wakamsaidie Rais Dkt. Mwinyi na sio vingine na wazingatie kuwa ameshasema serikali ya awamu ya nane sio ya kubembelezana hivyo wakawatumikie wananchi.



No comments:
Post a Comment