HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 16, 2025

MCC - RAJABU AKABIDHI HUNDI YA SH. MIL. 13 KWA BODA BODA PANGANI

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi Mkoani Tanga, Rajab Abdurahman amekabidhi mfano wa hundi ya zaidi ya Sh. Mil. 13 kwa kikundi cha Hatupoi Boda Group ikiwa ni ishara ya kuthamini juhudi zao na kuwapa nguvu ya kuendelea na shughuli zao bila mzigo wa madeni.



Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Ferry, wilayani Pangani ambapo kulihudhuriwa na kamati za siasa Wilaya,Mkoa,wanachama wa ccm,bodaboda na wananchi kwa ujumla ambapo wote wakiwa na sababu moja kuu ya kushuhudia tukio la mfano linaloonesha namna mikono ya vijana inavyoweza kuinua jamii pale inapopewa fursa na kusimamiwa vyema.

Komred Rajab ambaye pia ni Mjumbe wa Kati Kuu CCM Taifa alikuwa mgeni rasmi katika ghafla hiyo, aliwasili kwa lengo moja mahsusi la kuwatia moyo na kuwaunga mkono vijana wa Hatupoi Boda Group wa Wilayani hapa ambao wamekuwa kielelezo cha nidhamu, uwajibikaji na matumizi sahihi ya mikopo ya Serikali.

Akisalimia wananchi, Mwenyekiti Rajab aliwakumbusha changamoto za nyuma ambapo mikopo ya asilimia 10 (4% vijana, 4% wanawake na 2% watu wenye ulemavu) iliwahi kusitishwa kutokana na matumizi mabaya, baadhi ya viongozi kuunda vikundi hewa, na wengine kuona fedha hizo kama zawadi isiyohitaji kurejeshwa.

Rais alisimamisha mikopo hiyo kwa lengo la kuweka utaratibu mpya ili fedha hizo ziwafikie wanaostahili na zitumike kama mtaji wa maendeleo, si chanzo cha ubadhirifu.

Lakini leo, Pangani imekuwa kata ya mfano kwa mkoa mzima wa Tanga sio kwa bahati, bali kwa sababu kuna vikundi kama Hatupoi Boda Group vinavyoonesha kuwa vijana wana uwezo mkubwa wakipewa nafasi na kusimamiwa vizuri.

Kutokana na uaminifu wao, Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Rajab Abdurahman, aliahidi kumalizia deni lililobakia la zaidi ya Shilingi Milioni 13.4 na leo, mbele ya wananchi na kamati zote za siasa, ahadi hiyo imetimia.

Mwenyekiti Rajab aliwasisitiza vijana na wananchi wote kwamba maendeleo hayawezi kupatikana bila amani. Aliwakumbusha hotuba ya Rais Bungeni, akisema kwamba kila mmoja anapaswa kuwa mwalimu wa mwenzie katika kulinda amani msingi mkuu wa uchumi na ustawi.

Afisa Maendeleo ya Jamii, Stella Sekela, alisimama kueleza kwa fahari kuwa kikundi cha Hatupoi kimekuwa darasa tosha kwa vikundi vingine. Walipokea mkopo wa Shilingi Milioni 27 kwa muda wa miezi 16 ambapo pesa hizo zimekuwa daraja lao la kujikwamua kiuchumi.

Kwa miezi 8 pekee, tayari walirejesha zaidi ya Shilingi Milioni 14.59, hatua ambayo iliwavutia viongozi na kuthibitisha kuwa vijana hawa wanajitambua, wanaheshimu fedha za Serikali na wanaelewa dhana ya mikopo isiyo na riba.

Akisoma risala yao, Mwenyekiti wa kikundi hicho Alhaj Kidau, alisema kuwa mkopo huo uliwawezesha kununua pikipiki 8 na kuongeza kipato kwa wanachama 10 na alitumia fursa hiyo kwa kuishukuru Serikali ya Rais Samiah kwa kutoa mikopo isiyokuwa na riba ambapo imekuwa mkombozi kwa jamii.

Hata hivyo alitoa shukrani za dhati kwa niaba ya kikundi hicho kwa Mwenyekiti Komred Rajab kwa kwa huruma yake ya kumaliza deni lililobakia ili wanakikundi waweze kujipambania zaidi katika maisha yao.





No comments:

Post a Comment

Pages