KIKOSI cha Yanga kinachonolewa na Mreno Pedro Goncalves, kimeendelea kulinda rekodi ya kutofungwa katika mechi za hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL 2025/26), baada ya usiku huu kuvuna sare tasa ugenini walikowafuata JS Kabylie ya Algeria, katika mechi ya pili Kundi B.
Yanga, imemaliza dakika 90 kwenye dimba la Hocine Ait Ahmed mjini Tizi Ouzou, hivyo kufikisha pointi nne, huku ikisubiri matokeo kati ya AS FAR Rabat ya Morocco, ambao usiku huu wanaumana na Al Ahly ya Misri, kujua kama watabaki kileleni mwa msimamo wa Kundi B hadi mwakani mechi hizo zitapoendelea tena au watashushwa?
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa ngazi ya klabu barani Afrika, mechi zijazo zitachezwa mwishoni mwa Januari 2026, ambako Yanga ambao walishinda 1-0 wiki jana, wao watakuwa ugenini Cairo, Misri kuwavaa Al Ahly kati ya Januari 23 na 24, kisha kurudiana dimbani New Amaan Complex, Zanzibar kati ya Januari 30 na 31.
Aidha, katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF CC), Waoka Mikate wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC, wameendelea kugawa pointi, baada ya leo kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Wydad Athletic ya Morocco, bao pekee likifungwa dakika ya 57 na Nordin Amrabat.
Wawakilishi wengine wa Tanzania katika CAF CC, Singida Black Stars, kesho Jumapili watakuwa dimbani New Amaan Complex Zanzibar kuwaalika Stellenbosch ya Afrika Kusini, katika siku ambayo Wekundu wa Msimbazi nao watakuwa ugenini kuwavaa Stade Malien ya Mali katika mechi za Kundi D CAF CL.




No comments:
Post a Comment