Ikulu, Dodoma
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ameongoza kuagwa mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama, katika Ibada iliyofanyika Kanisa la Mwenyeheri Maria-Theresa Ledochowska, Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo Kuu Katoliki Dodoma.
Mbele ya familia, viongozi, Wabunge na waombolezaji waliokuwa kwenye ibada hiyo Rais Dk. Samia ameeleza masikitiko makubwa ya Taifa kufuatia msiba huo, akimwelezea marehemu kuwa alikuwa kiongozi jasiri, mwaminifu na mlezi wa viongozi wengi ndani ya Bunge na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema, Jenista alilitumikia Taifa kwa moyo wa kujitoa, nidhamu, uadilifu na hofu ya Mungu, akisimama imara kutetea haki, maendeleo na usawa wa wananchi.
Rais Dk. Samia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alikiri kutambua mchango mkubwa wa Jenista akihudumu kwa ufanisi katika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Serikali na CCM, sanjari na uwezo wake wa kubeba majukumu mazito kwa weledi.
Akigusia urithi wa uongozi aliouacha, Rais Dk. Samia alisisitiza kuwa moyo wake wa kujali maslahi ya Taifa ndio nguzo kuu ya kumbukumbu ya Hayati Jenista, na kutoa mwito kwa wabunge na viongozi wote kuiga mfano wake wa maadili na uwajibikaji aliouonesha.
Aliwataka viongozi kuuenzi mchango wa Marehemu kwa kuimarisha misingi ya uwajibikaji, mshikamano wa kitaifa na utumishi unaolenga maslahi mapana ya wananchi.
Rais Dk. Samia alitoa pole kwa familia, ndugu, wananchi wa Jimbo Peramiho, Bunge na taifa kwa ujumla, na kumuomba Mwenyezi Mungu awape faraja, nguvu na amani, huku akiiombea roho ya Marehemu pumziko la amani ya milele.
Source:
Shaaban Kissu,
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.











No comments:
Post a Comment