March 30, 2026

Huduma ya Maji Safi yawafikia wananchi wa kipato cha chini


Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Dontino Water Refilling Co Ltd, Valentino Ngeiyamu.



Upatikanaji wa maji safi na salama kwa bei nafuu ya kuanzia shilingi 200 umeanza kuwa mkombozi kwa wakazi wa kipato cha chini katika baadhi ya maeneo ya pembezoni mwa jiji la Dar es Salaam. Kwa muda mrefu, maeneo hayo yamekuwa yakikabiliwa na changamoto ya huduma ya maji, hali iliyowalazimu wananchi kutumia gharama kubwa au kutembea umbali mrefu kutafuta maji ya kunywa, hasa kutokana na uwepo wa maji ya chumvi.


Hata hivyo, hali hiyo sasa inaanza kubadilika kufuatia uwekezaji wa vituo vya kuuza maji safi (water kiosks) unaoendeshwa na kampuni ya DONTINO Water Refilling Co. Ltd chini ya mwekezaji Valentino Ngaiyamu. Kupitia vituo hivyo, wananchi wanapata maji safi na salama kwa urahisi karibu na makazi yao na kwa gharama nafuu.


Akizungumza kuhusu mradi huo, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Valentino Ngaiyamu, alisema lengo lao ni kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wananchi wa kipato cha chini kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kuchuja na kutibu maji ili yawe salama kwa matumizi ya binadamu. Alieleza kuwa wazo hilo lilitokana na uzoefu alioupata nje ya nchi, ambapo alishuhudia maji ya chumvi yakichujwa na kuwa safi na salama kwa kunywa.


Aliongeza kuwa wanakusudia kupanua huduma hiyo katika maeneo mbalimbali ikiwemo mashuleni, hospitali na vituo vya daladala ili kuwafikia wananchi wengi zaidi. Aidha, alisisitiza kuwa wanaunga mkono juhudi za serikali na wanathamini ushirikiano wanaoupata katika kuendeleza huduma hiyo, alibainisha kuwepo kwa changamoto kadhaa zinazoikabili huduma hiyo, ikiwemo kukatika kwa umeme kunakoathiri uzalishaji wa maji,


Licha ya changamoto hizo, ubora wa maji unaozalishwa umehakikishwa na mamlaka husika, hali inayowapa wananchi imani na usalama wa maji wanayotumia kila siku


Kwa upande wao, wananchi wamesema mradi huo umewaletea nafuu kubwa kwa kupunguza gharama za maji, hatari ya magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo salama. Vilevile, baadhi yao wamepata fursa za ajira kupitia uendeshaji wa vituo hivyo, jambo linalochangia kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.



Kwa ujumla, mradi huu umeleta matumaini mapya kwa wakazi wa Dar es Salaam, ukionyesha namna sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na serikali katika kutatua changamoto za msingi na kuboresha maisha ya wananchi wa kipato cha chini.

No comments:

Post a Comment

Pages