Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amewataka wajasiriamali nchini kutumia fursa za uchumi wa kidijitali kupanua masoko na kuongeza ushindani wa biashara zao, akisisitiza umuhimu wa teknolojia na ubunifu katika kukuza uchumi.
Amesema hayo Oktoba 21, 2026, wakati akifungua msimu wa nne wa Jukwaa la Instaprenyua 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Mlimani City, Dar es Salaam, huku akiipongeza Benki ya CRDB kwa juhudi zake za kuwawezesha wajasiriamali kupata mitaji, teknolojia na suluhisho za kifedha.
Kapinga amesema juhudi hizo zinaunga mkono dhamira ya Serikali ya kuweka mazingira rafiki kwa sekta binafsi na kujenga uchumi shindani unaoendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amehimiza wafanyabiashara kutumia mabadiliko ya kiteknolojia kama fursa ya kuboresha shughuli zao, kufikia wateja wengi zaidi na kuongeza ukuaji wa biashara.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Musa Kitambi, amesema jukwaa hilo ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo kuimarisha uhusiano na wajasiriamali, kubaini changamoto zao na kuwaunganisha na maarifa, mitaji na huduma zinazosaidia biashara kukua.
Jukwaa hilo la siku mbili, lenye kaulimbiu ya “Smartisha Biashara,” linajumuisha mijadala, mafunzo, maonesho na majadiliano ya kibiashara yanayolenga kuwaunganisha wajasiriamali na fursa za kukuza biashara zao.
Katika jukwaa hilo, CRDB pia inatoa huduma mbalimbali zikiwamo ufunguzi wa akaunti, mikopo, bima za biashara na suluhisho za kidijitali kama CRDB Lipa Hapa, SimBanking na Internet Banking. Jukwaa hilo linatarajiwa kuhitimishwa leo, Oktoba 22, 2026.




No comments:
Post a Comment