Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa, Joyce Msuya, aliyefika kujitambulisha baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo. (Picha na OMPR-ZNZ).
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali
Iddi alisema Mabadiliko ya Tabia Nchi yaliyopo Duniani yanaendelea kuiathiri
pia Zanzibar kutokana na kupanda kwa
kina cha maji ya Bahari kinachosababisha hali tete katika suala zima la hifadhi
ya Mazingira.
Akizungumza na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mazingira wa
Umoja wa Mataifa Bibi Joyce Msuya ambaye ni Mtanzania aliyeteuliwa kushika
wadhifa huo Miezi Miwili iliyopita Balozi Seif alisema hali hiyo ya mabadiliko
ya Tabia Nchi ikiachiwa kuendelea inaweza kusababisha maafa makubwa kwa visiwa
vya Zanzibar katika kipindi kifupi kijacho.
Balozi Seif alisema zipo jitihada kubwa
zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mamlaka
ya Usimamizi wa Mazingira na Idara ya Mazingira Zanzibar za kukabiliana na
changamoto hiyo lakini bado nguvu za Kimataifa zinahitajika kuunga mkono katika
kuona tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Alisema Zanzibar kama zilivyo Nchi nyengine changa
Duniani inahitaji misaada mikubwa katika kukabiliana na changamoto hiyo ili
Nchi iendelee kubakia salama hasa katika maeneo kama Msuka, Sipwese Kisiwani
Pemba na Jambiani na kilimani kwa Unguja ambayo hayako katika hali salama
Kimazingira.
Alimpongeza na kumshukuru Naibu Mkurugenzi Mkuu huyo
wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa kwa kushika wadhifa huo muhimu ambao Tanzania
na Zanzibar kwa ujumla inaringia kutokana na rasilmali zake kuendelea kutumia
katika Taasisi kubwa za Dunia.
Akitoa ufafanuzi Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya
Usimamizi wa Mazingira Zanzibar Nd. Juma Mjaja aliueleza Ujumbe huo wa Umoja wa
Mataifa unaoongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mazingira wa Umoja huo kwamba
Zanzibar ina maeneo 148 yaliyoathirika kutokana na Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Nd. Mjaja alisema zipo juhudi zilizoanza kuchukuliwa
na Taasisi hizo za Mazingira Zanzibar kwa kuwashajiisha Wana Jamii kupanda Miti
katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba ili kukabiliana na
Mabadiliko hayo ya Tabia Nchini.
Alisema upandaji wa miti ya Mikoko katika Visiwa
Vidogo Vidogo, uzoaji taka taka unaozingatia mfumo wa taaluma ya kisasa
sambamba na utoaji Elimu ya Mazingira kwa kuwashirikisha Wanafunzi Maskulini
imechangia kurejesha haiba ya Mazingira katika baadhi ya maeneo Nchini.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya
Mazingira Zanzibar Bibi Farhat Ali Abdullah alisema hali ya mazingira ya eneo
la Msuka Kaskazini ya Kisiwa cha Pemba inatisha kufuatia kupanda kwa kina cha
maji ya bahari.
Bibi Farhat alisema eneo hilo hivi sasa linaendelea
kuathiri majengo, Miti pamoja na baadhi ya mali kutokana na mmong’onyoko mkubwa
wa ardhi unaosababishwa na kasi kubwa ya Maji ya Bahari.
Akitoa shukrani zake Naibu Mkurugenzi huyo Mkuu wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa Bibi
Joyce Msuya alisema Umoja wa Mataifa utaendelea kuunga mkono jitihada
zinazochukuwaliwa na Nchi Wanachama ikiwemo Tanzania katika kukabiliana na
mabadiliko ya Tabia Nchi.
Bibi Joyce alisema ziara ya Ujumbe wake Nchini
Tanzania kwa kuanzia Visiwani Zanzibar imelenga kuijionea hali halisi ya
changamoto zinazoikabili Zanzibar kutokana na Mabadiliko ya Tabia Nchi
yaliyoikumba Dunia hivi sasa.
Alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba
hivi sasa lipo pendekezo moja tu la Tanzania katika maombi yake ya kuomba
misaada ya Kitaalamu na uwezeshaji ndani ya Taasisi za Umoja huo katika masuala
ya Mazingira ikilinganishwa na baadhi ya Nchi za Afrika ambazo tayari zimeshachangamkia
fursa hizo ili kufaidika na utaratibu huo wa Umoja wa Mataifa.
Naibu Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mazingira wa Umoja wa
Mataifa Mtanzania Joyce Msuya ni Mwanamke wa kwanza Barani Afrika kushikilia
nafasi hiyo baada ya kuitumikia Benki ya Dunia Mjini Washington kwa takriban
Miaka 10 iliyopita.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Uongozi wa Kamati Tendaji ya
Jumuiya ya Milade Nabii Zanzibar Ofisini
kwake Vuga Mjini Zanzibar.`
Katika mazungumzo yao Mwenyekiti wa Kamati hiyo
Sheikh Sheraly Shamsi alisema Maandalizi kwa ajili ya maadhimishio ya Maulidi
ya Kitaifa ya uzawa wa Kiongozi wa Waumini wa Dini ya Kiislamu Ulimwenguni
Mtume Muhammad {SAW} yamefikia hatua nzuri.
Sheikh Sheraly alisema Kamati Tendaji kupitia
Wawakilishi wake katika maeneo mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba imeshafanya
upembuzi na kuridhika na Madrasa zitakazoshiriki kwenye maulidi hayo
yanayotarajiwa kufanyika mahali pake Uwanja wa Michezo wa Maisra Suleiman iwapo
hakutakuwa na Mvua.
Alisema upembuzi huo umetoa fursa ya kupatikana kwa
Madrasa kutoka kila wilaya ambapo zile za Kisiwa cha Pemba Wanafunzi wake
wanatarajiwa kuingia Unguja mnamo Tarehe17 Novemba 2018 ambapo sherehe yenyewe
itakuwa Jumatatu ya Tarehe 19 Vovemba 2018 sawa na Mwezi 11 Mfunguo Sita.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili waRais wa
Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Kamati Tendaji hiyo ya Jumuiya ya
Milade Nabii kwa umakini wake unaopelekea kufanikisha maadhimisho ya Uzawa wa
Mtume Muhammad {SAW} Kila Mwaka.
Balozi Seif maulidi ya Mfunguo Sita yanaendelea kupata
umaarufu hata nje ya mipaka ya Zanzibar kutokana na mikakati inayowekwa na
Uongozi wa Kamati hiyo na kupelekea kuleta faraja sio kwa Waumini wanaohudhuria
viwanjani hapo bali hata wale wanaofuatilia kupitia vyombo mbali mbali vya
Habari wakiwa mitaani.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
19/10/2018.
No comments:
Post a Comment