Dande Contact

TEMBELEA BLOG HII KWA MATUKIO YA KILA SIKU-MOBILE +255 713 623 958 / +255 784 623 958 EMAIL dande15us@gmail.com

Halotel


CRDB

CRDB
.

Pages

WAZIRI MKUU AKEMEA MAHUSIANO MABAYA YA WATUMISHI KAHAMA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akisalimiana na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Fadhili Nkulru wakati alipowasili kwenye viwanja vya ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama  kuzungumza na watumishi wa Umma. Hii ilikuwa jana Julai 14 na leo Julai 15 Rais John Magufuli ametengua uteuzi wake. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekemea mahusiano mabaya baina ya watumishi wa wilaya ya Kahama na kusema wanapaswa kubadilika mara moja.

Ametoa onyo hilo leo (Jumapili, Julai 15, 2018) wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa Halmashauri za Wilaya za Ushetu, Msalala na Kahama Mji, wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

“Hali ya mahusiano hapa Kahama ni mbaya kuliko Kishapu na Shinyanga. Mnachapa kazi vizuri lakini tatizo kubwa kila mmoja anaenda kivyake, hakuna anayemsikiliza Mkurugenzi wa Halmashauri wala Mkuu wake wa idara,” amesema.

Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye ziara ya siku tano ya kikazi mkoani humo, amewaeleza watumishi na viongozi hao kwamba Serikali haitavumilia kuona watumishi wa aina hiyo wanaendelea kufanya kazi.

“Serikali haitavumilia kuona watumishi wakifanya mambo ya hovyo. Kahama ni wilaya yenye majaribu na Shinyanga nayo ni wilaya yenye majaribu makubwa. Kwa hiyo watumishi inabidi muwe makini, kuweni waangalifu msije mkaingia kichwakichwa kwenye majaribu haya.”

“Migogoro niliyoisikia ambayo iko hapa ni kwa sababu ninyi mmeingia kwenye biashara na kutake sides. Hapa Kahama, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Wilaya hamuelewani, Mkurugenzi na wakuu wa idara hamuelewani, wakuu wa idara na wasaidizi wao nao pia hawaelewani,” alisema.

“Napenda kusisitiza kwamba ninyio ni viongozi wa umma, kwa hiyo ni lazima mzingatie itifaki za kiuongozi, mzingatie mahusiano mema mahali pa kazi. Hatupendi viongozi muwe chanzo cha matatizo hapa Kahama,” aliwaasa.

Alisema Kahama ina fursa kubwa na nzuri kwenye kilimo, madini, mifugo na biashara na akawataka viongozi wanaoletwa kwenye wilaya hiyo wawe makini. “Kiongozi ukiletwa hapa inabidi uwe na kichwa kilichotulia. Inabidi uwe mwaminifu sana ili uweze kudumu kwenye wilaya kama hii,” alisisitiza.

“Kama kiongozi ulizoea kwenda disco inabidi uache, kama ulizoea kwenda baa inabidi ununue kreti uweke ndani kwako. Kama ulizoea kushabikia mpira kwa kujichora chaki, sasa basi. Kaa sebuleni kwako, angalia mpira kwenye luninga yako, ndiyo dhamana ya uongozi hiyo,” alisema.

Aliwataka watumishi wa umma wawasaidie wananchi kuboresha utendaji wao kwenye kilimo, uvuvi na ufugaji ili kila kuleta tija kwenye kila sekta.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake wilayani Kahama kwa kukagua shughuli za maendeleo na kuzungumza na wananchi.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 15, 2018.

UFARANSA YATWAA KOMBE LA DUNIA 2018, YAICHAPA CROATIA 4-2

 Wachezaji wa Ufaransa wakimrusha juu kocha wao, Didier Deschamps.
 Wachezaji wakishangilia baada ya kukabidhiwa kombe lao.
Wachezaji wa Ufaransa wakishangilia na kombe lao baada ya kulikosa kwa kipindi cha miaka 20. Ufaransa imeifunga Croatia mabao 4-2 katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia 2018.
Mario Mandzukic (katikati), akiruka juu kupiga mpira wa kichwa katika harakati za kuokoa na kujifunga mwenyewe katika mchezo wa Fainali ya Kombe la Dunia unaoendelea kwenye Luzhniki mjini Moscow. (Picha na Daily Mail).
 
 Wachezaji wa Ufaransa wakishangilia bao la kwanza la timu yao.
 
 Mshambuliaji wa Croatia, Ivan Perisic, akiifungia timu yake bao.
 
 Antoine Griezman akijiandaa kupiga penalti.

 Antoine Griezmann akiifungia timu yake kwa mkwaju wa penalti.
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappe, akishangilia na wanchezaji wenzake bao la 4 aliloifungia timu yake.

 
 Croatia wakishangilia bao lililofungwa na Ivan Perisic.

 Beki wa Croatia, Ivan Strinic (kushoto), akichuana na mshambuliaji wa France, Kylian Mbappe.
Mshambuliaji wa Croatia, Mario Mandzukic (kushoto), akimtoka Paul Pogba wa Ufaransa.
 Paul Pogba akishangilia baada ya kuifungia Ufaransa bao la tatu.
 Kylian Mbappe akiifungia timu yake bao la nne.

TAMUFO YAZIONYA KAMPUNI ZA KUUZA MUZIKI ZA NCHINI KENYA

 Wadau wa muziki kutoka Tanzania na Kenya wakiwa katika mkutano na  viongozi wa Umoja wa Wanamuzi Tanzania (TAMUFO), ulioshirikisha vikundi mbalimbali vya Kwaya ili kuwajengea uelewa na kuhakikisha wanafaidika na kazi zao za muziki unaoendelea jijini Arusha. Kushoto mbele mwenye tai ni Rais wa TAMUFO Dk. Donald Kisanga.

Na Dotto Mwaibale

UMOJA wa Wanamuziki Tanzania (TAMUFO) umeyataka makampuni ya Kenya yanayouza nyimbo za wanamuziki wa Tanzania bila kufuata utaratibu kuacha kufanya hivyo mara moja.

Ombi hilo limetolewa na Rais wa TAMUFO Dk.Donald Kisanga mjini Arusha juzi wakati  viongozi wa TAMUFO walipofanya mkutano na Vikundi mbalimbali vya Kwaya ili kuwajengea uelewa na kuhakikisha wanafaidika na kazi zao za muziki na kuwaunganisha na fursa za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kwa gharama nafuu kupitia  umoja huo.

"Natoa onyo kali kwa makampuni ya Kenya yanayouza nyimbo zilizoimbwa na watanzania na kurekodiwa na Tanzania kuuzwa kenya Kinyume cha Taratibu na kuwakosesha wanamuziki wa Tanzania Kufaidika na kazi zao na serikali kukosa mapato kupitia kodi" alisema Kisanga
Alisema katika mkutano huo Kampuni ya Kenya ya Africha ilikiri kosa na Kuahidi kuwalipa Wanamuziki  Wa Tanzania Pesa zao bila masharti yoyote baada ya kiziuza bila ya kufuata taratibu na kuwa TAMUFO na kampuni hiyo watatiliana saini za makubaliano kwenye mkutano huo. 

Katibu Mkuu wa TAMUFO, Stellah Joel alivitaja Vikundi vilivyohudhuria mkutano huo kuwa ni Kwaya Kuu Habari Njema na Kwaya ya UinjilistI za Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mjini kati Arusha, Kwaya kongwe za Ulyankulu Mapigano na Ulyankulu Barabara ya 13 zote za Tabora.

“LAMBALAMBA MARUFUKU MKOANI SONGWE”-CHIKU GALLAWA

 Mkuu wa Mkoa wa Chiku Gallawa akizungumza katika kikao cha wadua wa Afya kilichofanyika katika chuo cha Uuguzi Mwambani Mkwajuni-Songwe, Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Songwe Samwel Jeremia na Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Ileje Joseph Mkude.
Na Mwandishi Wetu, Songwe
Waganga wote wa jadi wanaopiga ramli chonganishi maarufu kama Lambalamba wamepigwa marufuku kufanya shughuli hizo mkoani Songwe huku wenyeviti wa vijiji ambavyo lambalamba watabainika kuendelea na shughuli hizo, hatua kali dhidi yao zitachukuliwa.
Marufuku hiyo imetolewa mapema leo na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa katika kikao cha wadau wa Afya mkoani hapa ambapo ameeleza kuwa changamoto mojawapo ya sekta ya afya ni uwepo wa waganga wa jadi ambao huwapotosha wananchi kwa imani zisizo za kweli.
Gallawa amesema, “Hatutaki kuona wala kusikia hivi vikundi vya vya lambalamba, kazi yao kubwa ni ulaghai na kuwaibia fedha wananchi, na ninaagiza, mwenyekiti yeyote wa kijiji atakayebainika kuwaendekeza hawa watu tunaanza naye kumchukulia hatua kali za kisheria”.
Ameongeza kwa kuwaagiza wakuu wa wilaya zote mkoani hapa wasimamie kuhakikisha wananchi hawatapeliwi na lambalamba hususani wilaya za Mbozi na Ileje ambako lambalamba wameonekana mara kwa mara.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Waganga wa Jadi na Machifu Mkoa wa Songwe Mwenenzunda Mteleshwa amesema kuwa yeye hawatambui lambalamba hivyo serikali iwachukulie hatua za kisheria kwakuwa wanaenda kinyume na taratibu za utoaji wa huduma za jadi.
Wakati huo huo Gallawa amezitaja changamoto nyingine katika sekta ya afya mkoani hapa ni uwepo wa ugonjwa wa ebola nchi jirani ya Congo, upungufu wa vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na uwepo wa magonjwa yanayosababishwa na uchafu kama vile kipindupindu.
Gallawa amefafanua kuwa serikali imeweka mikakati ya kuboresha sekta ya Afya Mkoa wa Songwe kwa kutoa shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya uboreshaji wa vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na Kuimarisha huduma za kitabibu kwa kuipandisha hadhi Hospitali ya Wilaya ya Mbozi ili itumike kama Hospitali Teule ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe.
Ameongeza kuwa mkoa unatarajia kuzindua mkakati wa usafi na mazingira ukiwa na kauli mbiu ya “Kataa uchafu Songwe” lengo likiwa ni kupambana na magonjwa yanayosababishwa na uchafu na kutunza mazingira.

WAZIRI MKUU: MUWAFUATE WANANCHI VIJIJINI

*Ataka watenge siku tatu hadi nne waende waliko wananchi
*Asema Serikali hii haitaki mambo ya urasimu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wote wa Serikali za Mitaa nchini watenge theluthi mbili ya muda wao wa kazi kwa kuwasikiliza wananchi na kuwahudumia.

Ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Julai 15, 2018) wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa Halmashauri za Wilaya za Ushetu, Msalala na Kahama Mji, wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

“Jukumu la watumishi ni kuwatumikia wananchi, Serikali hii hatutaki urasimu na wala hatutarajii kuwa mtatoa huduma kwa urasimu. Lugha ya ‘njoo kesho, njoo kesho’ siyo ya kwa awamu hii.”

Amesema Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya wana jukumu la kusimamia agizo hilo kwa kuhakikisha kuwa wanatoa usafiri kwa watumishi hao ili waweze kufika vijijini kwa haraka. “Wakurugenzi wa Halmashauri simamieni zoezi hilo kwa kupanga ratiba na kutoa gari ili maafisa wanne au watano watumie gari hilo kwenda vijijini wakawahudumie wananchi.”

Amesema wananchi wengi hawana uwezo wa kusafiri kutoka vijijini hadi mijini ili kuleta matatizo yao, kwa hiyo wakifanya hivyo, watumishi watakuwa wamewapunguzia matatizo wananchi.

Waziri Mkuu ambaye yuko kwenye ziara ya siku tano ya kikazi mkoani humo, amewataka watumishi wa idara ya ardhi wapime ardhi kwa wingi na watoe hati mapema ili wananchi wazitumie kuongeza mitaji.

“Pimeni ardhi na kutoa hati ili wananchi wazitumie kukopa na kupata mitaji ya kujiendeleza kiuchumi. Pia muweke mipango mizuri ya ardhi ili kuepusha migogoro baina ya wananchi.

Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake wilayani Kahama kwa kukagua shughuli za maendeleo na kuzungumza na wananchi.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 15, 2018.

WAZIRI MKUU AONGOZA HARAMBEE YA PAPO KWA PAPO

*Achangisha mifuko 2,000 ya saruji ujenzi wa uzio wa sekondari

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amechangisha mifuko 2,000 ya saruji na sh. milioni 50 kwenye harambee ya papo kwa papo kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa sekondari ya Mwendakulima wilayani Kahama.

Waziri Mkuu ameendesha zoezi hilo leo (Jumapili, Julai 15, 2018) wakati akizungumza na walimu na wanafunzi wa sekondari ya Mwendakulima, wilayani Kahama mkoani Shinyanga ambako alienda kupokea mabweni mawili ya wasichana.

Ujenzi wa mabweni hayo yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 126, umegharimu sh. milioni 560 na umefadhiliwa na kampuni kuchimba madini ya ACACIA kupitia fedha za Corporate Social Responsibility. Mabweni ya awali yaliteketea kwa moto.

Waziri Mkuu ameendesha harambee hiyo baada ya kuombwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mwendakulima, Bi. Neema Mfunya. Kwa wastani, mfuko mmoja wa saruji unagharimu sh. 16,500.

Katika harambee hiyo, Waziri Mkuu alichangaia mifuko 500 ya saruji, huku kampuni ya ACACIA ikichangia mifuko 400 kutoka kwa watumishi wake. MNEC wa Simiyu, Bw. Emmanuel Nsangali aliahidi kuchangia mifuko 200.

Ahadi nyingine zilizotolewa na Naibu Mawaziri, wabunge, na wakuu wa taasisi waliombatana na Waziri Mkuu kwenye ziara yake zilikuwa ni za mifuko 50 hadi 100.

Shule ya sekondari ya Mwendakulima ina wanafunzi 336 wa kidato cha tano na cha sita. Lakini kwenye kidato cha kwanza hadi cha nne, shule hiyo ina wanafunzi 771 ambao kati yao, wavulana ni 423 na wasichana ni 348.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 15, 2018.

WATANZANIA WANG’ARA MAJIMAJI SELEBUKA MARATHON

 Kamanda Camillius Wambura (kushoto), akiwa na Abdurhaman Hamis wakishiriki Majimaji Selebuka Festival mjini Songea.
Wanariadha Mohamed Dulle na Geofrey Korosi wakichuana katika mbio za Kilomita 21 Majimaji Selebuka Marathon mjini Songea.

NA MWANDISHI WETU
TAMASHA la Majimaji Selebuka 2018 limekata utepe jana mjini hapa kwa mbio za Marathon huku ikishuhudiwa Nestory Hudu kutoka Singida akiwatoa nishai Wakenya.
Hudu aliibuka kidedea katika mbio za Kilomita 42 kwa Wanaume akitumia saa 2:21:25 akifuatiwa na John Leonard wa Arusha saa 2.22:09 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Simon Lelei kutoka Kenya saa 2.22:54.
Kwa upande wa Wanawake Kilomita 42 mshindi aliibuka Purity Biwott wa Kenya alishinda akitumia saa 2.43:59 akifuatiwa na  Dorcus Chesang pia wa Kenya aliyetumia saa 2.45:21 huku nafasi ya tatu ikienda kwa  Angel John wa Arusha aliyetumia saa 2:53.44.
Kwa upande wa Kilomita 21 Wanaume  Pascal Sarwat wa Manyara alishinda akitumia saa 1.11:58 akifuatiwa na  Samson Lyimo wa Songea saa 1.12:13 huku Mohamed Dulle wa JWTZ Ruvuma akikamata nafasi ya tatu akitumia saa 1:12:34 wakati kwa Wanawake Tabitha Kibeth wa Kenya alishinda akitumia saa 1.21: 34 kutoka Kenya akifuatiwa na Violeth Adam wa Njombe akitumia 1.22:43 huku nafasi ya tatu ikikosa mshindi
Kwa upande wa Walemavu Kilomita 21 mshindi aliibukaDavid Mabula akifuatiwa na John Stephano huku nafasi ya tatu ikinyakuliwa na Mathias Jollo wote kutoka Dar es Salaam.
Pia kulikuwa na Mbio za Mita 800 kwa wanafunzi ambao walitia for a kwa mwitikio mkubwa na vipaji, kwa wavulana Felix Ndunguru alishinda akitumia dakika 2.46:00 akifuatiwa na Bashiru Ngonyani dakika 2:49.2 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Franco Justine aliyetumia dakika 2:52.
Kwa wasichana Magreth Thadei alitumia 2:58.53 akifuatiwa na Hadija Mohamed dakika 2:58.55 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Maisha Mwera dakika 2:59.03.
Mbali na washindi kujizolea zawadi ya fedha taslimu na medali, pia walipata ofa ya kutembelea Mbamba Bay Beach.
Majimaji Selebuka Festival imeandaliwa na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Songea-Mississippi (SO-MI), kwa kushirikiana na Tanzania Mwandi chini ya udhamini wa Bakhresa Group of Companies, Premier Bet, BIT Tech Ltd/Meridian Bet.
Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa Riadha Mkoa wa Ruvuma, Christian Matembo, alielezea kufurahishwa na muitikio wa washiriki mwaka huu ambao walifikia zaidi ya 200 walijitokeza huku watoto wakitia for a.
Baada yam bio, tamasha linaendelea leo kwa maonyesho ya wajasiriamali, mashindano ya ngoma za asili.

TULIA CUP 2018 YAZINDULIWA RASMI JIJINI MBEYA

NA KENNETH NGELESI,MBEYA
LIGI ya soka na Netiboli Tulia Cup 2018 imezinduliwa rasmi juzi katika Viwanja vya shule ya Msingi Ruanda Nzovwe jiji Mbeya huku mdhamini wa michuano hiyo Naibu Spika Dk Tulia Ackson akizitaka timu za ligi kuu zikiwemo Tanzania Prisons na Mbeya City FC kutumia michuano hiyo kusaka vipaji vya wachezaji watakao weza kuwatumia katika michezo mbalimbali ikiwemo ligi kuu.
Akizungumza mara baada ya ufunguzi wa Michuano Dk.Tulia alisema kuwa ligi hiyo itaanzia ngazi ya mitaa na baadaye kata 36 za jiji la Mbeya ,ngazi ya sita bora nusu fainali na hatimaye fainali zinazotarajiwa kupigwa Semptemba mwa huu.
Dk Tulia alisema ni fursa kwa timu za ligi kuu,daraja la kwanza na pili lakini pia ni fursa kwa wachezaji kuonyesha uwezo wao wa kucheza soka ili waweze kuonwa na timu kubwa .
‘Ni fursa kwa timu kusaka wachezaji lakini pia ni fursa kwa kwa vijna kuonyesha uwezo wao kwani mpira kwa sasa ni ajira na si soka tu lakini pia hata netibali itaenda sambamba kuanzi ngazi za mitaa na hatiamiye kata’
Michuano hiyo ilizinduliwa kwa kuzikutanisha timu ya Ilemi FC na Mbeya Youth mchezo uliomalizika Ilemi kuibuka na ushindi wa bao 1-0 Dk Tulia alisema michujo utaanzai ngazi mitaa kwa ajili ya kuoputa bingwa wa kata ambapo Tasisi yake “Tulia Trust” itatoa jezi pamoja na mpira kwa ajili ya michezo ligi hiyo timu zote za
Katika hatua nyingine Dk. Tulia alibainisha zawadi kuwa Bingwa katika michezo yote kila timu ataondoka na Bodaboda boda moja,Kombe,Medali kila mchezaji,Seti ya Jezi,na mpira,washindi wa pili medali kwa kila mchezaji,fedha taslimu sh.milioni 1.5,kombe,seti ya Jezi na Mpira.
Mshindi wa tatu ataondoka na fedha tasilimu milioni moja,seti ya Jezi,mpira na medali kwa kila mchezaji,huku mshindi wan ne akiondoka na shilingi lakini saba,700,000/ na watano shilingi laki tano na medali pia.
Pia Naibu Spika Dk Tulia alitangaza rasmi kugharamia masomo ya ziada Binti Diana Lucas wa kidato cha nne kutoka shule ya Sekondari Nzondahaki ya jiji Mbeya baada ya kufanya vizuri nafasi yan Ushambuliaji katika mchezo wa soka wasichina kwenye Mashindano ya UMISETA 2018 yaliyiomalizika hivi karibuni jiji Mwanza.
Kwa upande wake Mdau wa mchezo wa soka jiji Mbeya James Mwampondele alipongeza uamuzi uliofanywa na Naibu Spika huku akiahidi kutoa seti moja ya Jezi kwa timu zitakazo shika nafasi ya kwanza hadi ya nne.
“Mimi naunga mkono kazi hii ya Naibu Spika hivyo nikiwa kama mdau wa michezo nitatoa jezi seti moja kwa kila timu kuanzia ile ya kwanza hadi itakayo shika nafsi ya nne”

MAJALIWA APEWA HESHIMA YA KUWA MZEE WA KISUKUMA NA WAZEE WA TINDE MKOANI SHINYANGA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi wakati alipowasili kwenye uwanja wa Kituo cha Afya cha Tinde mkoani Shinyanga kuhutubia mkutano wa hadhara, Julai 14, 2918. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiufanyia majaribio  upinde aliozawadiwa na wazee wa mila wa Kisukuma katika kijiji cha Tinde mkoani Shinyanga kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Kituo cha Afya cha Tinde Julai 24, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Wazee wa Mila wa Kisukuma wakimsikiliza Waziri Mkuu ,Kassim Majaliwa wakati alipohutubia mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Kituo cha Afya cha Tinde ya Tinde mkoani Shinyanga, Julai 14, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Wazee wa Mila wa Kisukuma   baada ya wazee  hao kumpa heshima ya kuwa Mzee  mwenzao  katika mkutano wa hadhara aliouhutubia katika uwanja wa Kituo cha Afya cha  Tinde mkoani Shinyanga, Julai 14, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Tigo Yazindua Kampeni mpya ya ‘Tigo Pesa ni Zaidi ya Pesa’

Dar es Salaam, Tanzania

Tigo Pesa, Huduma ya Kifedha ya Kampuni ya Tigo Tanzania, imezindua kampeni ya ‘Tigo Pesa ni Zaidi ya Pesa’, kama uthibitisho kuwa huduma hiyo sasa ina hadhi ya huduma kamili ya kifedha ambayo inawapa wateja huduma za kipekee, bora na  nyingi zaidi kupitia mtandao wa simu.

Tigo Pesa ni Zaidi ya Pesa’ inazingatia sifa ya Tigo kuwa mtandao pekee unaobuni huduma na bidhaa kulingana na mahitaji ya wateja ili kuboresha na kurahisisha maisha yao.

‘Tigo Pesa imepanua wigo wa bidhaa na huduma zake na kuibua njia bora zaidi kwa wateja kufurahia huduma za haraka, uhakika na salama za kifedha popote walipo nchini Tanzania,’ Hussein Sayed, Afisa Mkuu wa  Huduma za Kifedha wa Tigo aliwaambia waandishi wa habari.

Kama sehemu ya kampeni hii, Tigo Pesa inajivunia kuwa mtandao pekee na wa kwanza wa simu unaotoa huduma inayowezesha wateja wa Tigo kurudisha miamala ya fedha zilizotumwa kimakosa kwenda kwa wateja wenzao wa Tigo.  Huduma hiyo inayopatikana kupitia menu ya Tigo Pesa  *150*01# inawapa wateja wa Tigo uwezo wa kurudisha kwa haraka miamala yoyote ya kutuma hela ikiwa watagundua kuwa wamekosea miamala hiyo, bila ya kuhitaji msaada wa moja kwa moja kutoka kitengo cha huduma kwa wateja.

‘Huduma hii ya kipekee ya kurudisha miamala iliyokosewa kwa haraka inajibu mahitaji ya wateja wengi ambao kwa sababu moja au nyingine wanafanya makosa pindi wanapotuma pesa. Ni huduma ya aina yake ambayo inawapa wateja uwezo zaidi juu ya miamala wanayofanya na imeundwa kwa kuzingatia vigezo vya hali ya juu vitakavyozuia matumizi mabaya ya huduma hii,’ Hussein alifafanua

Hivi karibuni, Tigo Pesa ilifungua ukurasa mpya wa maisha yasiyotegemea pesa taslim nchini, baada ya kuwa kampuni ya simu ya kwanza na pekee kuzindua huduma ya Tigo Pesa Masterpass QR. Huduma hii inawezesha wateja kulipia huduma na bidhaa haraka, kwa urahisi na usalama zaidi kwa njia ya kuscani nembo ya Masterpass Quick Response inayopatikiana katika maeneo tofauti ya manunuzi/huduma.

Tigo pia imeingia katika ushirikiano wa kipekee na kampuni ya teknologia ya Uber yanayowezesha wateja wa Tigo kutumia huduma za usafiri za Uber kwa bei ya punguzo na bila gharama za data. Ushirikiano huu ni muhimu kwa madereva na wasafiri wa Uber kwani unawezesha wateja zaidi kutumia Uber App kupitia simu zao na kupata usafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa urahisi na kwa bei ya punguzo. Kupitia Tigo Pesa pekee, wateja wa Tigo pia wana fursa ya kupata usafiri wa Uber bure kila mara wanapofanya miamala ya fedha kati ya akaunti zao za benki na akaunti zao za Tigo pesa. 

Tigo Pesa ndio huduma ya kifedha kwa njia ya mtandao inayokuwa kwa kasi zaidi nchini, ikiwa na wateja waliosajiliwa zaidi ya milioni saba, mtandao wa waanya biashara (merchants) zaidi ya 40,000 na mawakala zaidi ya   85,000 walioenea kote nchini.

Tigo ndio kampuni inayoongoza maisha ya kidigitali katika soko la mawasiliano ya simu nchini kwa miaka mingi. Tigo Pesa ndio huduma ya kwanza ya fedha kutoa gawio la faida kwa wateja wake. Tigo pia iliongoza juhudi za kuunganisha mitandao ya simu na mabenki ili kuunda mfumo wa kwanza duniani wa kifedha baina ya mabenki na mitandao ya simu. Mfumo huu umeongeza idadi ya miamala pamoja na kukuza ongezeko la idadi ya watu wanaotumia huduma rasmi za kifedha nchini.  Tigo pia ilikuwa kampuni ya kwanza ya simu za mkononi nchini na Afrika Mashariki kutoa huduma inayowezesha wateja kutuma na kupokea pesa kutoka nchi moja hadi nyingine kwa thamani ya sarafu ya nchi husika, hivyo kurahisisha na kuongeza wigo wa huduma za uhamishaji fedha baina ya nchi.

‘Kupitia kampeni ya ‘Tigo Pesa ni Zaidi ya Pesa’, Tigo inawaalika kutathmini hatua kubwa ambazo Tigo pesa imepiga katika kipindi hiki cha miaka michache. Kampeni hii pia inamkaribisha kila mtu kujiunga katika safari hii ya kipekee itakayowawezesha wananchi na biashara nyingi zaidi kuongeza idadi ya wanaotumia huduma rasmi za kifedha, kuboresha mazingira ya kidigitali na kufungua ukurasa upya wa maisha yasiyotegemea pesa taslim,’’ Hussein alibainisha.

PADRI AUGUSTINO RAMADHAN AONGOZA IBADA YA KUMBUKUMBU YA KIFO CHA MKE WA PROFESA SHABA

Padri wa Kanisa la Anglikana, Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhan akiongoza ibada ya kumbukumbu ya marehemu Elizabeth Shaba mke wa Profesa James Shaba aliye patwa na mauti Julai Mosi mwaka huu na kuzikwa Julai 7, Chicago, Marekani. Ibada hiyo imefanyika leo kwenye Kanisa la St Albano Angilkana, jijini Dar es Salaam.

Marehemu ambaye alikuwa anaishi na mumewe nchini Marekani mpaka anakutwa na mauti alikuwa Muuguzi Mshauri wa Ubalozi wa Canada. Alioana na Profesa Shaba mwaka 1963. PICHA NA RICHARD MWAIKENDA
 Baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki wakishiriki kwenye Ibada hiyo
Ibada ikiendelea.
 Anna Nyerere ambaye ni mtoto wa Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere, akishiriki katika Ibada hiyo
Kusoma neno la Mungu.
 Wakiimba wimbo wakati wa ibada.
 Wakishiriki kutoa sadaka wakati wa ibada hiyo.
 Ndugu wa marehemu Elizabeth Shaba, Grace Shaba akitoa sadaka.
 Padri Augustino Ramadhan akiwapatia waumini chakula cha bwana
 Wakishiriki kumuombea marehemu Elizabeth Shaba
 Charles Shaba ambaye ni mmoja wa viongozi wa familia akielezea wasifu wa marehemu Elizabeth Shaba.
 Baadhi ya wanafamiia wakiwa katika picha ya pamoja
 Wakipata chakula cha mchana baada ya ibada kumalizika