HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 19, 2018

MAKAMU WA PILI WA RAIS-ZANZIBAR AMPONGEZA MKURUGENZI MKUU WA MAZINGIRA-UMOJA WA MATAIFA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akisalimiana na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa, Joyce Msuya, aliyefika kujitambulisha baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo. (Picha na OMPR-ZNZ).

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Mabadiliko ya Tabia Nchi yaliyopo Duniani yanaendelea kuiathiri pia Zanzibar  kutokana na kupanda kwa kina cha maji ya Bahari kinachosababisha hali tete katika suala zima la hifadhi ya Mazingira.
Akizungumza na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa Bibi Joyce Msuya ambaye ni Mtanzania aliyeteuliwa kushika wadhifa huo Miezi Miwili iliyopita Balozi Seif alisema hali hiyo ya mabadiliko ya Tabia Nchi ikiachiwa kuendelea inaweza kusababisha maafa makubwa kwa visiwa vya Zanzibar katika kipindi kifupi kijacho.
Balozi Seif alisema zipo jitihada kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira na Idara ya Mazingira Zanzibar za kukabiliana na changamoto hiyo lakini bado nguvu za Kimataifa zinahitajika kuunga mkono katika kuona tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Alisema Zanzibar kama zilivyo Nchi nyengine changa Duniani inahitaji misaada mikubwa katika kukabiliana na changamoto hiyo ili Nchi iendelee kubakia salama hasa katika maeneo kama Msuka, Sipwese Kisiwani Pemba na Jambiani na kilimani kwa Unguja ambayo hayako katika hali salama Kimazingira.
Alimpongeza na kumshukuru Naibu Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa kwa kushika wadhifa huo muhimu ambao Tanzania na Zanzibar kwa ujumla inaringia kutokana na rasilmali zake kuendelea kutumia katika Taasisi kubwa za Dunia.
Akitoa ufafanuzi Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira Zanzibar Nd. Juma Mjaja aliueleza Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa unaoongozwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mazingira wa Umoja huo kwamba Zanzibar ina maeneo 148 yaliyoathirika kutokana na Mabadiliko ya Tabia Nchi.
Nd. Mjaja alisema zipo juhudi zilizoanza kuchukuliwa na Taasisi hizo za Mazingira Zanzibar kwa kuwashajiisha Wana Jamii kupanda Miti katika maeneo mbali mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba ili kukabiliana na Mabadiliko hayo ya Tabia Nchini.
Alisema upandaji wa miti ya Mikoko katika Visiwa Vidogo Vidogo, uzoaji taka taka unaozingatia mfumo wa taaluma ya kisasa sambamba na utoaji Elimu ya Mazingira kwa kuwashirikisha Wanafunzi Maskulini imechangia kurejesha haiba ya Mazingira katika baadhi ya maeneo Nchini.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Zanzibar Bibi Farhat Ali Abdullah alisema hali ya mazingira ya eneo la Msuka Kaskazini ya Kisiwa cha Pemba inatisha kufuatia kupanda kwa kina cha maji ya bahari.
Bibi Farhat alisema eneo hilo hivi sasa linaendelea kuathiri majengo, Miti pamoja na baadhi ya mali kutokana na mmong’onyoko mkubwa wa ardhi unaosababishwa na kasi kubwa ya Maji ya Bahari.
Akitoa shukrani zake Naibu Mkurugenzi huyo  Mkuu wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa Bibi Joyce Msuya alisema Umoja wa Mataifa utaendelea kuunga mkono jitihada zinazochukuwaliwa na Nchi Wanachama ikiwemo Tanzania katika kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi.
Bibi Joyce alisema ziara ya Ujumbe wake Nchini Tanzania kwa kuanzia Visiwani Zanzibar imelenga kuijionea hali halisi ya changamoto zinazoikabili Zanzibar kutokana na Mabadiliko ya Tabia Nchi yaliyoikumba Dunia hivi sasa.
Alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hivi sasa lipo pendekezo moja tu la Tanzania katika maombi yake ya kuomba misaada ya Kitaalamu na uwezeshaji ndani ya Taasisi za Umoja huo katika masuala ya Mazingira ikilinganishwa na baadhi ya Nchi za Afrika ambazo tayari zimeshachangamkia fursa hizo ili kufaidika na utaratibu huo wa Umoja wa Mataifa.
Naibu Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa Mtanzania Joyce Msuya ni Mwanamke wa kwanza Barani Afrika kushikilia nafasi hiyo baada ya kuitumikia Benki ya Dunia Mjini Washington kwa takriban Miaka 10 iliyopita.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Uongozi wa Kamati Tendaji ya Jumuiya ya Milade  Nabii Zanzibar Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.`
Katika mazungumzo yao Mwenyekiti wa Kamati hiyo Sheikh Sheraly Shamsi alisema Maandalizi kwa ajili ya maadhimishio ya Maulidi ya Kitaifa ya uzawa wa Kiongozi wa Waumini wa Dini ya Kiislamu Ulimwenguni Mtume Muhammad {SAW} yamefikia hatua nzuri.
Sheikh Sheraly alisema Kamati Tendaji kupitia Wawakilishi wake katika maeneo mbali ya Visiwa vya Unguja na Pemba imeshafanya upembuzi na kuridhika na Madrasa zitakazoshiriki kwenye maulidi hayo yanayotarajiwa kufanyika mahali pake Uwanja wa Michezo wa Maisra Suleiman iwapo hakutakuwa na Mvua.
Alisema upembuzi huo umetoa fursa ya kupatikana kwa Madrasa kutoka kila wilaya ambapo zile za Kisiwa cha Pemba Wanafunzi wake wanatarajiwa kuingia Unguja mnamo Tarehe17 Novemba 2018 ambapo sherehe yenyewe itakuwa Jumatatu ya Tarehe 19 Vovemba 2018 sawa na Mwezi 11 Mfunguo Sita.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili waRais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza Kamati Tendaji hiyo ya Jumuiya ya Milade Nabii kwa umakini wake unaopelekea kufanikisha maadhimisho ya Uzawa wa Mtume Muhammad {SAW} Kila Mwaka.
Balozi Seif  maulidi ya Mfunguo Sita yanaendelea kupata umaarufu hata nje ya mipaka ya Zanzibar kutokana na mikakati inayowekwa na Uongozi wa Kamati hiyo na kupelekea kuleta faraja sio kwa Waumini wanaohudhuria viwanjani hapo bali hata wale wanaofuatilia kupitia vyombo mbali mbali vya Habari wakiwa mitaani.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
19/10/2018.

No comments:

Post a Comment

Pages