January 20, 2013

MFUMO MPYA WA DIJITALI WAMKWAMISHA BEN POL


Na Elizabeth John

MKALI wa muziki wa RnB Tanzania, Benard Paul ‘Ben Pol’ amesema amelazimika kuchelewa kutoa video ya wimbo wake wa ‘Yatakwisha’ aliomshirikisha Estelina Sanga ‘Linnah’ kutokana na mabadiliko ya mfumo wa Analogia na kwenda Digitali.

Akizungumza na Habari Mseto jijini Dar es Salaam, Ben Pol alisema amelazimika kufanya hivyo kutokana na mabadiliko hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yanawaumiza Watanzania wengi kutokana na gharama za kugharamia Digitali ili uweze kuangalia vipindi mbalimbali katika televisheni yako.

Ben Pol alisema, video ya wimbo huo anatarajia kuiachia mwanzoni mwa mwezi Aprili ambapo anaamiki kwa kisi kikubwa Watanzania watakua wameizoea hali hiyo.

“Unajua Ving’amuzi vinapatikana kwa bei ya juu sana sio kila mtu ambaye anauwezo wa kukipata, kwasasa nikiachia video hii najua haitapokelewa vizuri na mashabiki wangu kwasababu asilimia kubwa watakua wanasimuliwa kuliko wanaoangalia,” alisema.

Pia alisema, kutokana na kazi yake ya ‘Pete’ kufanya vizuri katika vituo mbalimbali vya redio, anaona haina ulazima wa kuifanyia video kazi hiyo ila amewapa vionjo kidogo ndani ya video ya ‘Yatakwisha’.

“Unajua audio ikifanya vizuri inakua inatosha hamna ulazima wa kuangaika na video kwaupande wangu naona kama itakuja kuharibu kwasababu yenyewe inaweza isipokelewe vizuri, ila nimeweka baadhi ya vionjo katika wimbo wa ‘Yatakwisha’ nnhivyo mashabiki wangu hawataikosa kabisa,” alisema Ben Pol.

No comments:

Post a Comment

Pages