January 01, 2013

FALCAO: SITARAJII KUHAMA ATLETICO MADRID JANUARI HII


Radamel Falcao akishangilia kufunga mabao matatu 'hat-trick' katika moja ya mechi zake akiwa na Atletico Madrid

MADRID, Hispania

“Najivunia sana kuona idadi kubwa ya klabu zikionesha kunihitaji, lakini zitalazimika kusubiri hadi mwishoni mwa msimu huu. Kisha tutaona nini kitatokea juu yangu. Siwezi kuhama Madrid Januari hii”

MSHAMBULIAJI anayepigiwa hesabu na klabu nyingi zaidi barani Ulaya kwa sasa, Radamel Falcao, amezitaka Chelsea na Manchester City kusahahu kupata saini yake katika usajili wa dirisha dogo unaonaza leo Januari 1 barani Ulaya. 

Falcao nyota wa kimataifa wa Colombia anayechezea klabu ya Atletico Madrid, amesema hawezi kuihama klabu yake katika usajili huu, kauli inayozikata maini klabu kadhaa zinazosaka saini yake, huku akitajwa kakma mmoja wa washambuliaji bora zaidi duniani.

Licha ya kuwamo kwa kipengele kinachomruhusu kuihama klabu hiyo kwa dau nono la pauni milioni 47, Falcao amesema hata kama ikitokea klabu ya kuulizia uhamisho wake Januari hii hayuko tayari kutoma jijini hapa anakoheshimika.

Falcao, 26, alisema: “Najivunia sana kuona idadi kubwa ya klabu zikionesha kunihitaji, lakini zitalazimika kusubiri hadi mwishoni mwa msimu huu. Kisha tutaona nini kitatokea juu yangu.

“Kuondoka Atletico katika usajili wa majira ya baridi ni wazi si kati ya mambo yanayoweza kutokea. Nataka kusaidia mafanikio ya klabu yangu nami kuwa sehemu ya watimizaji malengo.”

Mkali huyu amekuwa katka rada za muda mrefu za Chelsea, na ilikuwa nusura atue Stamford Bridge katika siku ya mwisho ya usajili wa majira ya baridi msimu uliopita.

Mabao yake matatu ‘hat-trick’ katika kuwania UEFA Super Cup, wakati Atletico ikiichapa Chelsea mabao 4-1, yalikuwa na mchango mkubwa wa kutibua kibarua cha Roberto Di Matteo, huku akikoleza moto wa kuwindwa na The Blues.

No comments:

Post a Comment

Pages