January 01, 2013

FRANK LAMPARD ASHANGAA CHELSEA KUMCHUNIA LICHA YA KIWANGO


 Frank Lampard akishangilia moja ya mabao yake mawili aliyofunga na kuipa Chelsea ushindi wa mabao 2-1
 Shabiki akionesha bango la kumuomba mmiliki wa Chelsea kutomuacha kiungo Frank Lampard

LONDON, England

"Hatujazungumza lolote juu ya mkataba mpya na klabu katika wiki za karibuni. Kwa wakati huu hakuna kinachosemwa kuhusu hilo na mkataba wangu unafikia tamati kiangazi kijacho na hili linajulikana ndani na nje ya klabu"

KIUNGO wa Chelsea, Frank Lampard amesema hakuna mchakato wowote wa nyongeza ya mkataba wake na klabu hiyo ya Stamford Bridge, licha ya kiwango cha juu anachoonesha katika siku za karibuni.

Lampard, 34, nyota wa kimatauifa wa England, ambaye mkataba wake wa sasa unafikia tamati kiangazi kijacho, yuko huru kuingia mkataba wa awali na klabu yoyote ya nje katika kipindi hiki hiki cha usajili wa majira ya baridi unaonza leo barani Ulaya.

"Hatujazungumza lolote juu ya mkataba mpya na klabu katika wiki za karibuni," alisema Lampard ambaye alifunga mabao yote mawili ya Chelsea katika ushindi wake wa mabao 2-1 dhidi ya Everton, Jumapili.

"Kwa wakati huu hakuna kinachosemwa kuhusu hilo na mkataba wangu unafikia tamati kiangazi kijacho na hili linajulikana ndani na nje ya klabu."

Mabao mawili ya Lampard katika ushindi wa Blues huko Goodison Park, ina maana kuwa mkali huyo yuko nyuma kwa bao moja dhidi ya Kerry Dixon aliyefunga mabao 193 na kushikilia rekodi ya klabu hiyo ya mfungaji wa muda wote, ambayo inaongozwa na Bobby Tambling aliyefunga mabao 202.

Baada ya kuanza kwa kuwekwa benchi na kocha wa sasa Rafael Benitez, Lampard ameonesha zinduko la aina yake akicheza na kufunga kwa kiwango cha juu – akifunga katika mfululizo katika mechi tatu zaa Ligi Kuu zilizopita alizoanza kikosi cha kwanza.

Lampard amesisitiza kuwa ana furaha kuwa sehemu ya timu hiyo iliyocheza na kushinda mechi nne mfululizo za Ligi Kuu chini ya Benitez.

"Nina furaha mno kucheza, nafanya kazi ngumu, kwa bidii mazoezini, ninapenda kuwa sehemu ya timu hii," aliongeza Lampard.

"Yote kwa yote naweza kukwambai kwamba ni jambo jema na nina furaha kwamba naendelea kucheza vema kikosini kama nilivyoonesha leo katika mechi hii," alimaliza Lampard ambaye anawindwa na LA Galaxy kujaza pengo la David Beckham.

No comments:

Post a Comment

Pages