January 13, 2013

JESHI LA POLISI LAWAMANI


DAR ES SALAAM, Tanzania

BAADHI ya askari polisi wa vyeo vya chini wamelalamikia vitendo vya ubaguzi vinavyofanywa  na uongozi wa juu wa Jeshi hilo, hususan katika kusafirisha   miili ya marehemu wa vyeo hivyo vya chini.

Malalamiko hayo yametolewa kwa nyakati tofauti na baadhi ya polisi hao wa vyeo vya chini walipozungumza na mwandishi wa mtandao huu.
Kwa mujibu wa sheria na kanuni za jeshi hilo (PGO), inapotokea askari yoyote amepoteza maisha bila kujali cheo chake,  jeshi linapaswa kutoa sh milion moja  pamoja na sanduku kwa ajili ya mazishi.
Walisema utaratibu huo wa PGO  bado unaendelea kutumika na haujabadilika,  lakini uongozi wa jeshi hilo, umekuwa ukitumia ubaguzi katika kutoa msaada huo hususan kwa kuangalia vyeo.
“Ndani ya jeshi la polisi, askari anayefanya kazi kubwa ni askari wa cheo cha chini yani Kostebo, Koplo na Sajenti lakini amekuwa akidharauliwa na kutothaminiwa ukilinganisha na askari wenye vyeo ”kilalamika chanzo hicho.


Kikifafanua zaidi, chanzo hicho kilisema anapofariki askari wa cheo cha chini kama Konstebo, Koplo, Sajenti na Meja wa Jeshi hilo wanatoa gari ndogo (Defender), kwa ajili ya kusafirishia familia ya askari huyo hadi kwao kitendo ambacho kinakwenda kinyume na taratibu za jeshi hilo.
Hata hivyo, inapotokea kifo cha askari wa cheo cha juu kuanzia nyota moja jeshi hilo linatoa gari lenye uwezo wa kuchukua watu 30 (Costa), hali inayoleta mkang’anyiko.
“Askari hao wa vyeo chini wanajiuliza kuwa hivi askari anayetambulika ni askari wa kuanzia nyota moja na kuendelea, huku sisi tukiwa kama tambala la kupigia deki, tunajua kila tunachosema wanakikanusha japo ndiyo ukweli wenyewe”kilieleza.
Alipoulizwa msemaji wa Jeshi hilo, Advera Senso kuhusu malalamiko hayo, alisema inaoneka askari hao hawazifahamu vema taratibu za serikali.
Alisema ni vema askari hao wakawauliza viongozi wao  kile wasichokijua ili waweze kupatiwa ufafanunuzi kuliko kukimbilia kwenye vyombo vya habari kwani havitawasaidia kutatua kile wasichokijua kuhusu taratibu za jeshi lao.

No comments:

Post a Comment

Pages