January 11, 2013

MAANDALIZI YA SHEREHE ZA MAPINDUZI ZANZIBAR YAKAMILIKA


 Kamanda wa Brigedia nyuki Brigedia General Sharif Sheikh, akiwa pamoja na Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif, wakifurahia mwenendo mzima wa matayarisho ya gwaride  la Vikosi vya Ulinzi yaliyokuwa yakifanyika katika uwanja wa amani MJINI Zanzibar.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya Taifa ya sherehe na mapambo Balozi seif, akiwa na Waziri wake Kulia Mh. Mohd Aboud Mohd na Kamanda wa Brigedia Nyuki Brigedia General Shjarif Sheikh wakiangalia matayarisho ya mkwisho ya gwaride la sherehe za mapinduzi katika uwanja wa amani Mjini Zanzibar.
 'Watoto wa Kazi' Kikosi Maalum cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ }, Kikionyesha umahiri wake ndani ya Uwanja wa amani wakijiandaa na sherehe za maapinduzi zinazofanyika kesho Jumamosi Tarehe 12 Januri 2013, katika uwanja huo.
 Msanii wa Kikundi cha Utamaduni cha Hiari ya Moyo kutoka Mkoani Domoma kikipasha moto kujiandaa na utoaji burdani kwenye sherehe za maaadhimisho ya kutimia miaka 49 ya mapinduzi ya Zanzibar zitakazofikia kilele chake januari 12 2013.
 Kikundi cha Utamaduni ya mchanga mdogo kisiwani Pemba kikitoa burdani ya ngoma ya msewe katika matayarisho ya maadhimisho ya sherehe za kutimia Mikaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar hapo Uwanja wa Amani.
***************************

Wakati harakati za shamra shamra za maadhimisho ya kutimia miaka 49 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 zikikaribia kufikia kileleni matayarisho ya mwisho ya gwaride la kuhitimisha sherehe hizo zimekamilika rasmi.
Matayarisho  ya Gwaride hilo ambalo ndilo linalopamba maadhimisho ya sherehe hizo za Mapinduzi ya Zanzibar yamefanyika katika uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya sherehe na Mapambo ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa na Wajumbe wa Kamati hiyo pamoja na Baadhi ya maafisa wa Vikosi vya ulinzi walishuhudia matayarisho hayo.
Vikosi vya ulinzi vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania { JWTZ } Polisi, KMKM, Mafunzo, JKU, Valantia na Zimamoto na uokozi vilianikiza ndani ya uwanja wa Amani wakati  vilipokuwa vikitoa burdani ya gwaride la aina yake vikiongozwa na Vikosi vya Bendi.
Wakipita mbele ya mwenyekiti huyo wa Sherehe na Mapambo Balozi Seif Askari hao walionekana kuwa katika hali ya ukakamavu baada ya kufanya mazoezi ya pamoja kwa kipindi cha mwezi Mmoja.
Staili ya mwendo wa pole na ule wa haraka zikimalizia kwa heshima mbele ya Viongozi hao ilionekana kukubalika vyema na walioshuhudia matayarisho hayo kutokana na makofi ya vigeregere wakati wakitoa heshima zao.
Raha zaidi ilionekana kuwakonga moyo walioshuhudia zoezi hilo wakati maafandi hao walipomalizia kwa hatua 15 zilizofuatiwa na ule wimbo maarufu unaomuhusu kila mwanafunzi anayepata elimu ya dunia katika maskuli wa sisi sote tumegomboka.
Matayarisho hayo yalifuatiwa na burdani za vikundi vya utamaduni vya Msewe kutoka Mchanga mdogo Kisiwani Pemba, Mkunguru kutoka Kaskazini Unguja na Hiari ya Moyo kutoka Mkoa wa Dodoma Tanzania Bara sambamba na Vijana wa halaiki kutoka Skuli ya Sekondari ya Nyerere.
Akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Taifa ya Sherehe Zanzibar mara baada ya kumalizika kwa matayarisho ya Gwaride hilo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Balozi Seif Ali Iddi amewashukuru na kuwapongeza Makamanda na askari wa vikosi vya ulinzi kwa juhudi zao za matayarisho makini.
Balozi Seif alielezea matumaini yake kutokana na matayarisho hayo kwamba sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia Miaka 49 mwaka huu zitakuwa nzuri na za aina yake.
Wakichangia kwenye kikao hicho cha mwisho baadhi ya wajumbe wa Kamati hayo wamewaomba wanachi watakaobahatia kuingia katika uwanja wa sherehe waache kuchukuwa mikoba ambayo inaweza kuwaletea usumbufu wakati wanapotaka kuingia uwanjani hapo.
Hata hivyo wajumbe hao wamependekeza kwamba kikundi au taasisi itakayopangwa kwa tukio lolote kiwanjani hapo wakati wa sherehe hizo wakazingatia zaidi wakati ili kwenda vizuri na ratiba iliyopangwa.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

No comments:

Post a Comment

Pages