January 07, 2013

MOURINHO: LAMPARD BADO JEMBE MUHIMU SANA CHELSEA


MADRID, Hispania

“Mimi siamini katika umri – mfano, katika kikosi cha Inter Milan, hakuna anayekimbia zaidi kuliko Javier Zanetti na ana miaka 39! Hupaswi kumpima mchezaji kwa umri wake, bali kwa kiwango chake dimbani”
JOSE Mourinho amemtaja kiungo wake wa zamani klabuni Stamford Bridge, Frank Lampard kuwa mmoja wa nyota wakubwa wa zama zote wa Chelsea kutokana na mchango na rekodi zake.

Mourinho ambaye kwa sasa anainoa Real Madrid ya La Liga nchini Hispania, alifanya kazi kwa miaka mitatu na Lampard, alipounda kizazi cha dhahabu cha Chelsea kilichotwaa mataji sita ukiwamo ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili.

Sasa, kukiwa na utata juu ya thamani ya Lampard klabuni hapo alipotakiwa kusaka timu mpya licha ya kukubali kwake kupunguza mshahara wake, ‘Special One’ anasisitiza kuwa: “Frank Lampard daima atakuwa mmoja wa nyota muhimu katika historia ya Chelsea.

“Sijui habari hii juu yake itaenda na kuishia vipi, lakini nachotambua na kutaka kitokee ni kuwa nataka kumuona Frank na Chelsea wakimalizana vizuri.”

Mourinho, alienda mbali zaidi na kubainisha hisia zake Lampard anaweza kusukuma soka la kiwango cha juu kwa miaka kadhaa: “Mimi siamini katika umri – mfano, katika kikosi cha Inter Milan, hakuna anayekimbia zaidi kuliko Javier Zanetti na ana miaka 39!

“Nimewahi kuwa na wachezaji waliokuwa na umri wa miaka 20 ambao wengi wao walishachoka. Hupaswi kumpima mchezaji kwa umri wake, bali kwa kiwango chake dimbani,” alisisitiza Mourinho.

Kauli ya Mourinho aliitoa juzi wakati Chelsea ikijiandaa kuivaa Southampton katika raundi ya tatu ya Kombe la FA, ambayo iliisha kwa Chelsea kushinda mabao 5-1, huku Lampard akifunga moja lililomfanya aweke rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi.

Bao lake la penati mwishoni mwa mtanange huo, limemfanya Lampard afikishe jumla ya mabao 193, akiipiku rekodi ya mabao 192 iliyokuwa ikishikiliwa na Kerry Dixon.

No comments:

Post a Comment

Pages