January 04, 2013

RAFA BENITEZ ATETEA KICHAPO CHELSEA, LIVERPOO YAUA


LONDON, England

KOCHA wa Chelsea, Rafael Benitez, ametetea uamuzi wake wa kubadili kikosi kilichokwaana na QPR katika mechi ya juzi iliyoisha kwa timu yake kulimwa bao 1-0.

Kwa kipigo hicho kutoka kwa timu inayoburuza mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya England, kocha huyo amejikuta katikati ya lawama kwa kupanga kikosi dhaifu.

Kikisi cha juzi kilikuwa ni tofauti na kile kilichocheza na Everton mwishoni mwawiki na kushinda mabao 2-1.

Nyota ambao hawakucheza mechi ya mwishoni mwa wiki na kupangwa katika mechi ya juzi, ni Ryan Bertrand, Marko Marin, Victor Moses, Oscar  na Ross Turnbull.

Hata hivyo, Benitez ametetea uamuzi wake kwa kusema ni vigumu kuchezesha kikosi kimoja kwa kipindi chote cha krismas na mwaka mpya.

Alisema alichofanya katika mechi hiyo ni kuwapa nafasi wengine na kuwapumzisha wengine kama Juan Mata na Eden Hazard.

"Tumecheza vizuri tena kwa kujiamini, alisema Benitez  na kuongeza: "Tulibadili baadhi ya wachezaji, lakini ni Marko Marin ndiye pekee ambaye amekuwa hachezi mara kwa mara.

Katika mechi ya mwisho (dhidi ya Everton), Moses alicheza kama ilivyo kwa Oscar. 

"QPR wao walicheza kwa kuvizia na kupiga pasi fupifupi. Hii ndio ilikuwa tofauti kubwa kati yetu na wao hasa kuelekea mwishoni mwa mechi.

"Huwezi kuchezesha kikosi kimoja kila mechi. Unapocheza ugenini na timu inayoburuza mkia, unapaswa kuwaamini wachezaji ako, nami nawaamini,” alisema Benitez katika hali ya kutetea kipigo hicho.

Kwa kipigo hicho, Chelsea imebaki nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa na pointi 38, ikitanguliwa na Man Utd 52 na Mam City(45) na Tottenham yenye pointi 39.

Tangu Benitez atwae mikocha ya timu hiyo kutoka kwa Roberto Di Matteo, amekuwa hapati  sapoti kubwa ya mashabiki wa timu hiyo, hivyo kipigo cha juzi kimeibua mengi.

Bao lililowapa wenyeji pointi tatu, lilifungwa dakika ya 78 na Shaun Wright-Phillips, ukiwa ni ushindi wa pili kwa timu hiyo katika msimu huu.

Wakati Chelsea wakipata kichapo, Liverpool wakicheza nyumbani walivuna ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Sunderland.

Mabao mawili ya Liverpool yalifungwa na nyota wa kimataifa wa Uruguay, Luis Suarez, baada ya kinda  Raheem Sterling kuifungia la kwanza dakika ya 19.

Suarez sasa amefikisha mabao 15, akiwa nyuma kwa bao moja dhidi ya kinara Robin van Persie wa Manchester United.

Liverpoo sasa wamefikisha pointi 31 baada ya kucheza mechi 21, hivyo kuwa nafasi ya nane kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

No comments:

Post a Comment

Pages