January 25, 2013

WASHIKA BUNDUKI WAWALIPUA WAGONGA NYUNDO

Beki wa Arsenal Bacary Sagna kulia akimkagua yoso Dan Potts wa West Ham United baada ya kugongana naye na kupoteza fahamu wakati wa mechi ya Ligi Kuu ambayo Arsenal ilishinda 5-1
Jack Wilshere wa Arsenal kulia akichuana na nyota wa West Ham United katika mechi ya Ligi Kuu iliyoisha kwa Gunners kushinda mabao 5-1.
LONDON, England

Mabao mawili ya Olivier Giroud na moja moja kutoka kwa Lukas Podolski, Santi Cazorla na Theo Walcott, yalitosha kuwapa Gunners ushindi wa mabao 5-1

BAADA ya kupoteza pambano la mahasimu wa jiji la London ‘London Derby’ dhidi ya Chelsea kwa mabao 2-1, Arsenal juzi usiku ilirejea nyumbani Emirates na kufanya mauaji makubwa dhidi ya ‘Wagonga Nyundo’ West Ham katika mechi ya Ligi Kuu.

Mabao mawili ya Olivier Giroud na moja moja kutoka kwa Lukas Podolski, Santi Cazorla na Theo Walcott, yalitosha kuwapa Gunners ushindi wa mabao 5-1, baada ya kutangulia kufungwa na Collison wa Hammers kunako dakika ya 18.

Ushindi huo umeifanya Arsenal ipande kwa hatua moja na sasa kushika nafasi ya sita ikiwa na pointi 37, baada ya mechi 23 za Ligi Kuu, 15 kuelekea mwishoni mwa msimu.

Katika mechi hiyo, yoso Dan Potts aliumia vibaya na kutibiwa uwanjani hapo kwa dakika tisa, baada ya kugongana na beki wa kulia wa Gunners, Mfaransa Bacary Sagna.

Baada ya matibabu hayo kwenye dimba la Emirates, Potts alikimbizwa katika Hospitali ya Whittington, ambako mara moja aliingizwa katika chumba cha uchunguzi kujua ukubwa wa tatizo lake, ingawa hakukuwa na habari zaidi hadi jana asubuhi.

…..Daily Mail/The Sun……

No comments:

Post a Comment

Pages