Mkurugenzi wa chuo cha Southern Colege Ilula Enock Marwa Range (kulia mwenye trakisuti ) akiwa na mwalimu wake Baraka Mkula wakipelekwa mahabusu baada ya kunyimwa dhamana juzi katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa wa Iringa ,walimu hao wanatuhumiwa kuendesha chuo bila kusajiliwa na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu zaidi ya Tsh milioni 11. (Picha na Francis Godwin)
Na Francis Godwin, Iringa
CHUO cha utalii cha Southern Colege Ilula Kilolo mkoani Iringa kimefungwa kwa muda usiofahamika baada ya mkuu wa chuo hicho na mwalimu wake mmoja kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuendesha chuo hicho bila kusajiliwa na kujipatia fedha zadi ya Tsh milioni 11 kidanganyifu kutoka kwa wanafunzi wa chuo hicho.
Mkurugenzi huyo wa chuo hicho Enock Marwa Range na mwalimu wake Baraka Mkula walifikishwa mahakamani juzi mbele ya hakimu mkazi mwandamizi mfawidhi wa mkoa Iringa Juma S. Hassan kusomewa mashitaka mawili likiwemo la kujipatia fedha kiasi cha shilingi milioni 11.468,000 kutoka kwa wazazi wa wanafunzi wanaliojiunga na chuo hicho ambacho ni chuo hewa.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya mahakama hiyo mwendesha mashitaka wa Jamhuri ,Adolf Maganga alisema kuwa walimu hao ambao wanashitakiwa kwa kesi namba 66 ya mwaka 2013 kwa pamoja wanashitakiwa kwa makosa mawili likiwemo la kujipatia kiasi chicho cha fedha kosa la pili ni kuendesha chuo bila kusajiliwa .
Maganga aliiambia mahakama hiyo kuwa watuhumiwa hao walikamatwa machi 15 mwaka huu baada ya wanafunzi wa chuo hicho kufika polisi kulalamikia mwenendo wa chuo hicho kuendeshwa kinyume na kutapeliwa fedha zao za ada .
Alisema kuwa hadi sasa chuo hicho kimefungwa hakifanyi kazi na kuwa wao kama jamhuri wameandika barua ya kiapo kwa mahakama hiyo kuomba watuhumiwa hao wasipewe dhamana kutokana na makosa kuwa na sura ya kijamii zaidi hivyo iwapo watapata dhamana jamii wakiwemo wanafunzi wenyewe wanaweza kuwazuru watuhumiwa hao .
Mwendesha mashtaka huyo alisema hadi sasa chuoni chuo hicho chenye wanafunzi zaidi ya 50 kwa sasa wanafunzi waliobaki hawazidi 10 ,na kuwa chuo hicho kilikuwa kikitoa mafunzo ya utalii ngazi ya cheti .
Maganga aliiambiwa mahakama hiyo kuwa chuo hicho kimefungwa toka machi 5 mwaka huu hakifanyi kazi kabisa na kuwa sababu za watuhumiwa hao kuomba kudhaminiwa ili kwenda kuwahudumia chakula wanafunzi hazina msingi wowote .
“Mheshimiwa hakimu naomba sana watuhumiwa wasipewe dhamana kwani wanafunzi wanawachukia sana walimu hao kwa kuwapotezea muda wao pamoja na kupokea fedha zao kwa chuo ambacho hakijasajiliwa ….sasa iwapo watapewa dhamana kwanza wanaweza kupoteza ushahidi wa jambo hili na pili usalama wao unaweza kuwa mdogo zaidi”
Awali watuhumiwa hao waliomba kudhaminiwa ili kwenda kuwahudumia chakula wanafunzi kwa madai iwapo mahakama hiyo itaendelea kuwanyima dhamana wanaweza kusababisha wanafunzi hao kufa kwa njaa.
Hata hivyo mahakama hiyo ilikubali ombi la jamhuri juu ya kunyimwa kwa dhamana kwa watuhumiwa hao na kusema kuwa mahakama hiyo italitazama upya suala hilo la kupewa dhamana kwa watuhumiwa siku ya jumatatu (leo ) ambapo watuhumiwa hao watafikishwa tena.
No comments:
Post a Comment