HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 17, 2013

Chuo cha utali cha 'mfukoni 'Chafungwa Iringa mmiliki na mwalimu wafikishwa mahakamani kwa kujipatia Tsh milioni 11 kidanganyifu

Mkurugenzi  wa chuo cha  Southern Colege Ilula Enock Marwa Range (kulia mwenye trakisuti ) akiwa na  mwalimu  wake Baraka Mkula wakipelekwa mahabusu baada ya  kunyimwa  dhamana juzi katika mahakama ya hakimu mkazi mkoa  wa Iringa ,walimu hao  wanatuhumiwa kuendesha  chuo bila kusajiliwa na kujipatia  fedha kwa njia ya udanganyifu  zaidi ya Tsh milioni 11. (Picha na  Francis Godwin)

Na Francis  Godwin, Iringa 
CHUO  cha utalii cha Southern Colege Ilula  Kilolo  mkoani  Iringa kimefungwa kwa muda  usiofahamika baada  ya mkuu  wa chuo  hicho na  mwalimu wake  mmoja  kukamatwa na  kufikishwa mahakamani kwa tuhuma  za  kuendesha  chuo  hicho bila kusajiliwa na kujipatia  fedha  zadi ya Tsh milioni 11  kidanganyifu  kutoka kwa  wanafunzi  wa chuo hicho.
Mkurugenzi  huyo wa chuo hicho Enock Marwa Range  na mwalimu  wake Baraka Mkula  walifikishwa mahakamani  juzi  mbele ya hakimu mkazi mwandamizi mfawidhi  wa  mkoa  Iringa  Juma  S. Hassan kusomewa mashitaka  mawili likiwemo la kujipatia fedha  kiasi cha  shilingi  milioni 11.468,000 kutoka kwa wazazi  wa wanafunzi  wanaliojiunga na  chuo  hicho ambacho ni chuo hewa.

Akisoma mashtaka  hayo  mbele ya mahakama  hiyo  mwendesha mashitaka wa Jamhuri ,Adolf Maganga alisema  kuwa  walimu hao ambao  wanashitakiwa kwa kesi namba 66 ya mwaka 2013  kwa pamoja  wanashitakiwa kwa makosa mawili likiwemo la  kujipatia  kiasi chicho  cha fedha  kosa la  pili ni kuendesha  chuo bila  kusajiliwa .
Maganga  aliiambia  mahakama  hiyo  kuwa  watuhumiwa hao   walikamatwa machi 15 mwaka huu  baada ya wanafunzi  wa  chuo  hicho  kufika  polisi  kulalamikia mwenendo wa  chuo  hicho  kuendeshwa  kinyume na kutapeliwa  fedha zao za ada .
Alisema  kuwa hadi  sasa  chuo  hicho  kimefungwa hakifanyi kazi na  kuwa  wao kama  jamhuri  wameandika barua ya  kiapo kwa mahakama hiyo  kuomba watuhumiwa hao  wasipewe dhamana  kutokana na makosa  kuwa na sura ya kijamii zaidi hivyo iwapo watapata dhamana jamii wakiwemo wanafunzi wenyewe wanaweza kuwazuru watuhumiwa hao .

Mwendesha mashtaka huyo alisema hadi sasa chuoni chuo hicho chenye wanafunzi zaidi ya 50 kwa sasa wanafunzi waliobaki hawazidi 10 ,na kuwa chuo hicho kilikuwa kikitoa mafunzo ya utalii ngazi ya cheti .
Maganga aliiambiwa mahakama hiyo kuwa chuo hicho kimefungwa toka machi 5 mwaka huu hakifanyi kazi kabisa na kuwa sababu za watuhumiwa hao kuomba kudhaminiwa ili kwenda kuwahudumia chakula wanafunzi hazina msingi wowote .
Mheshimiwa hakimu naomba sana watuhumiwa wasipewe dhamana kwani wanafunzi wanawachukia sana walimu hao kwa kuwapotezea muda wao pamoja na kupokea fedha zao kwa chuo ambacho hakijasajiliwa ….sasa iwapo watapewa dhamana kwanza wanaweza kupoteza ushahidi wa jambo hili na pili usalama wao unaweza kuwa mdogo zaidi”
Awali watuhumiwa hao waliomba kudhaminiwa ili kwenda kuwahudumia chakula wanafunzi kwa madai iwapo mahakama hiyo itaendelea kuwanyima dhamana wanaweza kusababisha wanafunzi hao kufa kwa njaa.
Hata hivyo mahakama hiyo ilikubali ombi la jamhuri juu ya kunyimwa kwa dhamana kwa watuhumiwa hao na kusema kuwa mahakama hiyo italitazama upya suala hilo la kupewa dhamana kwa watuhumiwa siku ya jumatatu (leo ) ambapo watuhumiwa hao watafikishwa tena.

No comments:

Post a Comment

Pages