HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 18, 2013

MABINGWA ULAYA: BARCELONA, AJAX KIAMA NOU CAMP LEO



BARCELONA, Hispania

Kiungo Mjerumani, Mesut Ozil atakuwa akicheza pambano lake la kwanza la Mabingwa Ulaya akiwa na jezi za Gunners, iliyomsajili kwa dau la pauni milioni 42.4 akitokea Real Madrid ya Hispania

MABINGWA mara nne wa michuano ya mabingwa wa Ulaya, FC Barcelona ya hapa, leo watakuwa dimba la Camp Nou kuwaalika Ajax Amsterdam ya Uholanzi, ambayo pia imetwaa ubingwa huo mara nne, katika pambano la ufunguzi wa ‘Kundi la Kifo’ la H.

Barca walio chini ya kocha mpya, Gerardo ‘Tata’ Martino aliyerithi mikoba ya Tito Vilanova, itakuwa na shughuli pevu katika mechi hiyo kukivaa kikosi kinachonolewa na nyota wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Uholanzi, Frank de Boer.

Tayari Tata Martino amejinasibu kushinda mechi ya nyumbani, ingawa alikiri kuwa watalazimika kuwa makini na kutumia kila kosa la wapinzani ili kufanikisha nia ya kuanza vema mchakamchaka huo utakaohitimishwa Mei mwakani.

Pambano jingine la kundi H la michuano hii, linazikutanisha AC Milan ya Italia na Celtic ya Uskochi, litakalopigwa kwenye dimba la San Siro jijini Milan, ambalo wenyeji wataingia bila kiungo wake mpya Ricardo Kaka aliyerejea hapo akitokea Real Madrid.

Kwingineko, jijini London, wenyeji wa dimba la Stamford Bridge na mabingwa wa Europa League, Chelsea watakuwa nyumbani kuwaalika FC Basle ya Uswisi, katika ufunguzi wa jaribio la klabu hiyo kutwaa taji la Ulaya kama ilivyofanya mwaka jana.

Ikiwa chini ya kocha wake wa zamani Jose Mourinho aliyerejea Darajani akitokea Real Madrid, Chelsea itaingia dimbani leo ikitoka kuugulia maumivu ya kichapo katika pambano la Ligi Kuu ya England, ilikoangukia pua kwa bao 1-0 dhidi ya Everton.

Chelsea inaikaribisha Basle ikijivunia uwapo wa mshambuaji Mcameroon, Samuel Eto’o aliyeutua hapo akitokea Anzhi Makhachkhala ya Russia.

Katika mechi nyingine ya kundi hilo la E, Schalke 04 ya Ujerumani, itaialika       Steaua Bucharest ya Romania kwenye dimba la Veltins Arena.

Katika kundi la F, Washika Bunduki wa jiji la London, Arsenal watakuwa ugenini ndani ya dimba la Stade Velodrome jijini Marseille kuwava wenyeji Olympique Marseille ya Ufaransa katika ufunguzi mwingine unaosubiriwa kwa hamu.

Kiungo Mjerumani, Mesut Ozil atakuwa akicheza pambano lake la kwanza la Mabingwa Ulaya akiwa na jezi za Gunners, iliyomsajili kwa dau la pauni milioni 42.4 akitokea Real Madrid ya Hispania.

Wanafainali wa msimu uliopita, Borussia Dortmund ya Ujerumani, watakuwa ugenini San Paolo jijini Naples, kuwavaa wenyeji Napoli walio chini ya kocha Rafael Benitez na nyota kadhaa waliotua klabuni hapo kiangazi hiki.

Katika ufunguzi wa kundi G, FK Austria Vienna watakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Franz Horr kuwaalika FC Porto ya Ureno, huku Atletico Madrid ya Hispania ikiumana na Zenit St Petersburg kwenye Uwanja wa Vicente Calderon jijini Madrid.

RATIBA YA MECHI ZA LEO KWA UFUPI
KUNDI E
Schalke 04       v          Steaua              Veltins-Arena
Chelsea            v          FC Basel          Stamford Bridge

KUNDI F
Marseille          v          Arsenal Stade Vélodrome
Napoli              v          Dortmund         Stadio San Paolo

KUNDI G
Austria Wien    v          FC Porto          Ernst-Happel
Atl. Madrid      v          Zenit                 Vicente Calderón

KUNDI H
AC Milan         v          Celtic               San Siro
Barcelona         v          Ajax                 Camp Nou


Supersport.com/uefa.com

No comments:

Post a Comment

Pages