Kaimu Meneja Kiongozi Uhusiano na huduma kwa wateja wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bi. Theopista Muheta (Kulia) akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 15, Meneja Uhusiano wa kampuni ya Capital Plus International, Bw. Geoffrey Nangai (kushoto) ikiwa ni sehemu ya udhamini wa mbio za Rock City Marathon za mwaka 2013. Wakishuhudia ni Afisa uhusiano mwandamizi wa NSSF, Juma Kintu (wapili kulia) ni Ofisa Uhusiano wa mfuko, Bi Carolyne Newa. Makabidhiano hayo yalifanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Na Mwandishi Wetu
SHIRIKA la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limeelezea jitihada zake za kuendelea kusaidia aina mbali mbali ya michezo nchini ikiwa na lengo la kuiwezesha nchi kushiriki katika michezo ya kimataifa.
NSSF ambayo ni mdhamini mkuu wa mbio za Rock City Marathon 2013 kukiwa na wadhamini wengine African Barrick Gold (ABG), Precision Air, Airtel kupitia Airtel Money, Bank M, Nyanza Bottling, New Mwanza Hotel Sahara Communication na Umoja Switch, imedhamiria kushirikiana na viongozi wa chama cha Riadha Tanzania ili kukuza mchezo huo nchini.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki mara baada ya kukabidhi hundi ya shilingi milioni 15 kwa ajili ya udhamini wa mbio za Rock City Marathon 2013 zinazoandaliwa na kampuni ya Capital Plus International, Afisa uhusiano mwandamizi wa NSSF, Bw. Juma Kintu aliwaeleza viongozi wa chama cha Riadha Tanzania kukaa na NSSF na kujadili ni jinsi gani wanaweza kuchangia ili kufufua mchezo wa riadha Tanzania.
“Ni wakati wa kufanyakazi kwa ukaribu ili kusaidia kukuza mchezo huu ambao ni kama vile unakufa. Nchi yetu inauwezo mkubwa wa kufanya vizuri kimataifa katika riadha. NSSF ipo tayari kuunga mkono jitihada za kuufufua mchezo wa riadha nchini. Viongozi wa RT watuone na tujadili tufanyeje ili tupate ufumbuzi,” alisema.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Kiongozi Uhusiano na huduma kwa wateja wa NSSF, Bi. Theopista Mheta alisema kuwa mchango huo umelenga kukuza mchezo wa riadha wa ndani, ambao ni moja kati ya michezo inayoungwa mkono na mfuko huo.
“NSSF inatambua umuhimu wa mchezo wa riadha katika kukuza utalii wa ndani nchini lakini kwa wakati huo huo nafasi hii pia inaweza kutumika kuendeleza vipaji vipya katika riadha, na ndiyo sababu tumeamua kusaidia pia mbio za mwaka huu za Rock City Marathon,” alisema Mheta.
Naye, Meneja Uhusiano wa kampuni ya Capital Plus International (CPI), Bw. Geoffrey Nangai aliyepokea hundi kwa niaba ya waandaaji, aliipongeza NSSF kwa mchango wao na kutoa wito kwa makampuni mengine kujitokeza kusaidia na kuwa sehemu ya mkakati wa kufufua mchezo wa riadha nchini.
“Mchango huu utatuwezesha kuboresha maandalizi katika mbio hizi ambazo viwangi vyake vimeendelea kukua ukilinganisha na miaka minne iliyopita. Mbali na kusaidia kukuza utalii wa ndani, Rock City Marathon inatoa fursa kwa vyama vya riadha kutambua vipaji vipya katika riadha vinavyoweza iwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa,” alisema Nangai.
Alisema kuwa mbio za Rock City Marathon za mwaka huu zimepangwa kufanyika katika uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza tarehe 27, Oktoba 2013, ambazo zitajumuisha mbio za kilometa 21 – nusu marathon, kilometa 5 mbio kwa washiriki toka katika makampuni, kilometa 3 kwa watu wenye ulemavu, kilometa 3 kwa wazee na kilometa 2 kwa watoto walio kati ya umri wa miaka 7 mpaka 10.
No comments:
Post a Comment