HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 10, 2014

UCHAGUZI WA TASWA FEBRUARI 16
UCHAGUZI Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), utafanyika Februari 16 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Uamuzi huo ulifikiwa na kikao cha Kamati ya Utendaji ya TASWA  kilichofanyika Dar es Salaam jana kujadili masuala mbalimbali ya chama na waandishi wa habari za michezo kwa ujumla.

Kikao kilikubaliana kuwa uchaguzi ufanyike kwa katiba ya zamani, kwani mchakato wa katiba mpya unaweza kuchukua muda mrefu, hivyo kusababisha viongozi waliopo madarakani kuendelea kukalia viti kinyume cha katiba, jambo ambalo si sahihi.

Kutokana na hali hiyo viongozi wapya watakaochaguliwa moja ya kazi yao kubwa itakuwa kuifanyia marekebisho makubwa katiba ya chama chetu ili iende na wakati.

Kikao kimekubaliana kuwa wanachama wote walipie ada zao zote wanazodaiwa kuanzia mwaka 2011, hadi mwaka 2013, na mwisho wa kufanya hivyo ni Januari 31 mwaka huu na yule atakayeshindwa kutekeleza agizo hilo atapoteza haki ya kupiga kura na atahesabika si mwanachama hai.

Malipo yafanywe kwa Mhazini Msaidizi, Mohammed Mkangara, 0658-123082 na hakuna mwanachama mpya atakayekubaliwa kujiunga na chama mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu.

Pia Kamati ya Utendaji imeunda Kamati ya Uchaguzi na kumteua Mwenyekiti wa zamani wa TASWA, ambaye kwa sasa ni Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura, kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kusimamia Uchaguzi Mkuu wa TASWA, ambapo pia kutakuwa na wajumbe wengine wanne

Wajumbe hao ni Katibu Mkuu wa zamani wa TASWA, Mwina Kaduguda, aliyepata kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TASWA, Peter Mwenda na wanahabari Isakwisa Mwaifuge na Mbonile Burton ambao wote ni wanachama wa TASWA.

Pia Kamati ya Utendaji imekubaliana tuombe wawakilishi wawili wawe waangalizi wa uchaguzi huo kuhakikisha haki sio tu inatendeka bali pia ionekane inatendeka, ambapo mmoja atatoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na mwingine Idara ya Habari (MAELEZO), utaratibu wa kuwasiliana na taasisi hizo mbili unaendelea.

Fomu za kuwania uongozi zitaanza kutolewa Februari 10 hadi Februari 14 mwaka huu saa kumi alasiri, masuala mengine yahusiyo uchaguzi huo, ikiwemo mahali utakapofanyika yatatangazwa baada ya kikao cha sekretarieti ya TASWA na Kamati ya Uchaguzi kitakachofanyika Februari 3.
Si dhambi wanaotaka kuongoza kutangaza nia zao mapema wakiona inafaa.

No comments:

Post a Comment

Pages