Na Mwandishi Wetu
UONGOZI wa wakali wa muziki wa dansi nchini Extra Bongo ‘Next
Level Wazee wa Kimbembe’ umemrejesha kundini aliyewahi kuwa rapa bendi hiyo
Greyson Semsekwa sambammba na kumnyakuwa mnenguaji Asha Sharapova kutoka bendi
ya African Stars Twanga Pepeta.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Msemaji wa bendi hiyo
Juma Kasesa, alisema, kurejea kwa Semsekwa mmoja ya wanamuziki waasisi wa Extra
Bongo kutaimarisha safu ya 'kufokafoka' kuelekea kwenye uzinduzi wa albamu yao
mpya ya 'Mtenda Akitendewa.'
Kwa mujibu wa Kasesa, Mtenda Akitendewa inatarajiwa
kuzinduliwa Februari 22 mwaka huu kwenye Ukumbi wa Dar Live, uliopo Mbagala
Zakhiem jijini Dares Salaam.
Semsekwa alishiriki kwa kiwango katika albamu ya 'Mjini
Mipango' mwaka 2009 kabla ya baadae kutimkia Twanga Pepeta na sasa amerejea
kundini akiwa na rapu mpya ambazo atazimbulisha Jumamosi hii katika onyesho maalumu
la Utambulisho wao litakalofanyika katika Ukumbi wa Meeda Sinza.
Alisema, wameamua kumchukua Sharapova baada ya kutambua
kipaji alichonacho katika unenguaji hivyo kukidhi vigezo vya kunengua kwenye
bendi hiyo inayoundwa na wanenguaji wakongwe kama Maria Salome na Otilia Boniface
chini ya ukufunzi wa Super Nyamwela.
"Tunaendelea na mikakati ya kujiimarisha kwakuwa kila
maboresho tunayofanya kwenye bendi pia tunazingatia maoni na ushauri wa wapenzi
na wadau wa Extra Bongo ili kuendelea kuwapa burudani inayowasuuza nyoyo zao,"alisema
Kasesa.
Aliwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi Jumamosi hii kwenye
onyesho la bendi hiyo Meeda kuona muonekano mpya wa Semsekwa na Sharapova baada
ya kutoka Twanga Pepeta.
No comments:
Post a Comment