HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 24, 2021

WANAWAKE WAKATOLIKI KUSINI WATAKIWA KUHIMIZA UJENZI WA MAADILI

 
Na Stephano Mango, Songea

WANAWAKE  wa Kanisa Katoliki (WAWATA) kutoka majimbo ya kusini mwa Tanzania wametakiwa kutimiza wajibu wao  wa kulea familia zao katika misingi ya maadili ili taifa liweze kupata viongozi bora.

Rai hiyo ilitolewa na Naibu Askofu wa Kanisa Katoliki jimbo kuu la Songea Padre Erick Mapunda wakati alipokuwa akihubiri kwenye Ibada ya misa takatifu ya kongamano la wanawake wakatoliki kutoka jimbo la Mbinga, Songea, Tunduru Masasi,Njombe,Mtwara  na Lindi iliyofanyika katika kanisa la mtakatifu Mathias Kalemba mjini Songea.

Padre  Mapunda amewataka wanawake hao kujitambua kuwa wao ndio nguzo na tanuli la kuwalea vijana katika misingi ya maadili kwa lengo la kukabiliana na mmomonyoko wa maadili.

Naye mwenyekiti wa umoja wa wanawake wakatoliki kanda ya kusini Sabina Nkuba alisema kuwa katika kipindi cha siku tatu cha kongamano hilo wanawake hao wamejifunza mada mbalimbali ikiwemo juu ya kujua familia na malezi ya ndoa,wajibu wa mwanamke katika familia,kanisa na jamii.

Nkuba alizitaja mada nyingine kuwa wajibu wa mwanamke mkatoliki katika kujua afya ya uzazi na magonjwa ya saratani kwa akina mama,wajibu wa mwanamke katika maisha ya ndoa pamoja na jinsi ya kulea utoto mtakatifu.

Alisema kuwa katika kukabiliana na changamoto hiyo ya mmomonyoko wa maadili umoja huo wa wanawake wakatoliki umeamua kuunda umoja wa vijana na wasichana kwa lengo la kupata ndoa zilizo bora pamoja na kizazi chenye maadili.

Kwa upande wake mmoja wa washiriki wa kongamano hilo Vestina Nguruse alisema kuwa katika kipindi chote walichokuwepo kwenye kongamano hilo wameweza kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo juu ya masuala ya ujasiriamali.



No comments:

Post a Comment

Pages