HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 24, 2021

RC Dar: NMB mkombozi wa maisha ya Wafanyakazi, Wastaafu Tanzania

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla akikaribishwa na Afisa Mkuu wa wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (katikati) na Meneja wa Kanda ya Dar es Salaam na Zanzibar, Donatus Richard wakati wa Siku ya walimu na NMB (Teachers Day) iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana. 

 

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla akiongea kwenye kongamano la siku ya walimu na NMB lililofanyika jana jijini Dar es Salaam. NMB Iliandaa siku ya walimu Dar es Salaam ambapo iliwapa mafunzo na elimu juu ya bidhaa za NMB zitakavyoweza kuwasaidia kwa Maisha ya baadae.  


Baadhi ya Walimu kutoka sehemu mbalimbali za jiji la Dar es Salaam waliohudhuria kwenye kongamano la siku ya walimu na NMB lililofanyika jana jijini Dar es Salaam. NMB Iliandaa siku ya walimu Dar es Salaam ambapo iliwapa mafunzo na elimu juu ya bidhaa za NMB zitakavyoweza kuwasaidia kwa Maisha ya baadae.

 

NA MWANDISHI WETU 


WATUMISHI wa umma nchini, hususani walimu, wamekumbushwa umuhimu wa kukopa kwa malengo, sambamba na kuepuka mikopo kandamizi, huku wakielezwa kuwa Benki ya NMB ni mkombozi, mshirika na rafiki sahihi wa maisha ya wafanyakazi kabla na baada ya kustaafu.

 

Hayo yameelezwa jana na Mkuu wa Mkoa (RC) wa Dar es Salaam, Amos Makalla, wakati akizindua kongamano la siku moja la Walimu na NMB kwa mkoa wa Dar es Salaam 'Hatua kwa Hatua,' lililofanyika Jumatano, likiandaliwa na Benki ya NMB na kushirikisha walimu zaidi ya 300 toka wilaya za mkoa huo.

 

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kongamano hilo, RC Makalla alibainisha kuwa, walimu na watumishi wengine wa umma wanapaswa kutambua umuhimu wa uwekezaji mdogo mdogo kwa ustawi wa maisha yao wawapo kazini na baada ya kustaafu na kutumia vema fursa za mikopo rafiki ya NMB.

 

"Tumieni falsafa ya 'I=C+S.' Maana yangu ni kuwa 'Income Can be Consumed or Saved.' Kwamba chochote unachopata unaweza kukitumia au kuweka akiba. Sasa tunakosea tunapogeuza pato lote kuwa 'Consumption.' Kadri unavyoweka akiba, ndivyo unavyoweza kufanya 'investment.'

 

"Ustawi wa maisha yenu ya sasa na baada ya kustaafu, unategemea na  uwekezaji mtakaofanya, ikiwamo kukopa kwa malengo, kuepuka mikopo kandamizi na kutotumia pesa za mikopo kwa anasa. Mimi mwenzenu ni shuhuda wa hili na niwaibie siri, ukiondoa NMB, taasisi nyingi za fedha hazina madirisha yanayokidhi mahitaji ya watumishi.

 

"NMB ndio benki kinara wa kuwakomboa watumishi wa umma, benki inayoongoza katika kubuni na kutoa huduma rafiki kwa walimu na watumishi wengine kwa kuwapa mikopo yenye riba na masharti nafuu. Walimu mna  fursa pana ya kunufaika na benki hii," alisema RC Makalla.

 

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, alisema walimu ni kada muhimu miongoni mwa makundi yanayo hudumiwa na benki yake, huku akiitaja kada hiyo kama iliyotoa mchango mkubwa wa kukuza pato la NMB kiasi cha kuongezeka kwa gawio lao kwa Serikali katika mwaka wa fedha uliopita.

 

"Niseme tu kwamba, walimu ni kundi muhimu kwa benki yetu, ndio maana tumeandaa Siku ya Walimu na NMB. Kupitia siku hii, tunapata fursa ya kuongea nanyi, kutambulisha huduma mpya na kupokea mawazo mazuri kutoka kwenu, kwani nyie mnayaona mengi huko kwenye jamii na mawazo yenu yana thamani kubwa.

 

"Majuzi NMB imekabidhi kwa Serikali gawio la Sh. Bilioni 21.8, mafanikio ambayo kimsingi yana mchango mkubwa wa walimu, kada ambayo bila uwepo wake, huenda NMB isingekuwa hapa ilipo. Ndio maana tuko makini kubuni huduma rafiki kwenu, zikiwamo za Kidijitali," alisema Mponzi.

 

Naye Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Donatus Richard, alisema NMB na Walimu ni jukwaa muhimu sio tu kwa kutoa elimu ya masuala ya fedha na kukusanya maoni yao, bali kunadi bidhaa mpya, ambako mwaka huu, pamoja na nyinginezo, wamekuja na Bima ya Vikundi.

 

Aidha, baadhi ya washiriki wa kongamano hilo walikiri kuvutiwa na ubunifu wa NMB sio tu katika huduma rafiki wanazotoa kwao, bali kwa namna inavyojitoa kutatua changamoto za Sekta ya Elimu, sambamba na kuwakutanisha walimu na kupokea mawazo na ushauri wao, kisha kuyafanyia kazi.

 

Mwalimu Victor Timbuka wa Shule ya Msingi Msasani, wilayani Kinondoni, aliipongeza kwa namna inavyopambana kuwaelimisha walimu nchini masuala ya uwekaji akiba, huku alikiri kuvutiwa na kauli ya RC Makalla juu ya umuhimu wa kuweka akiba na kufanya uwekezaji mdogo mdogo kwa ustawi wa maisha yao ya sasa na baada ya kustaafu.

 

"Kauli ya RC Makalla ina ukweli, kwa miaka mingi matatizo yetu yalitokana na kukosa elimu ya masuala ya fedha, madhara ya ukopaji usio na malengo, pamoja na matumizi ya pesa za mikopo kwa anasa. Lakini kupitia majukwaa kama haya, walimu hivi sasa wameelimika na hawafanyi makosa hayo tena," alisema Timbuka.

 

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Walimu Tanzania, Fatuma Kalembo, alikiri kuwa wengi wao waliingia matatizoni kwa kuvamia mikopo kandamizi, isiyo na malengo na kutojibunia miradi midogo ya maendeleo na hivyo kuishi kwa kutegemea mishahara yao, lakini kwa sasa wanafanya ujasiriamali na kuongeza uwezo wa kujikumu na kujiendeleza.

 

No comments:

Post a Comment

Pages