HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 25, 2015

Diamond Platnumz hazina ya sanaa Tanzania

Na Mwandishi Wetu


MKOA  wa Kigoma ni hazina kubwa ya vipaji hapa nchini Tanzania. Tangu zamani kulishuhudiwa vipaji vingi toka mkoani humo hasa vya wanamichezo na wasanii. Mfano kwa upande wa kandanda tutaona kwamba mkoa huo ulitingisha kwa vipaji vya wanasoka.

Kina Manara, Kitwana Manara, Sunday Manara, Kassim Manara na ndugu zao wengine wanatoka Kigoma. Baadaye kikafuatia kizazi cha kina Edbily Lunyamilla, Nteze John, Omari Mavumbi, Itutu Kigi na wengineo wengi.

Kwa upande wa wasanii wa muziki Kigoma imetoa watu wengi wenye majina makubwa katika sanaa hiyo,  kama Shem Karenga, Hassan Rehan Bitchuka, Marijani Rajabu, Zahir Ally Zorro, Banana Zorro, Wema Abdallah, Nyota Waziri na wengineo wengi.

Kwa upande wa muziki wa kizazi kipya Kigoma imetoa vijana wengi wa muziki huo wakiongozwa na mtaalamu wa muziki, kwa maana ya kutunga, kuimba, kucheza kila ala ya muziki na kutengeneza muziki, Emmanuel Bizimana Ntavyo ‘Bizman’. Wapo wengine kama Ally Kiba, Banana Zorro, Jacqueline Ntuyabaliwe ‘K-Lynn’ na wengineo.

Lakini pamoja na wote hao makala hii ni mahususi kwa moja ya vipaji hivyo vya mkoa wa Kigoma ikiwa imemlenga chiriku wa muziki wa kizazi kipya kwa sasa hapa nchini, Nassibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Diamond kadhihirisha kipaji cha sanaa ya muziki kutokana na mafanikio aliyoyapata kwa muda mfupi alioutumia katika sanaa. Hiyo ni tofauti na kipindi alichokitumia mfalme wa muzuki wa POP duniani, Michael Jackson, kuwa kileleni mwa mafanikio kwa zaidi ya miaka 10 kati ya 1967 – 1979.

Lakini ndani ya miaka mitatu Diamond ameweza kuibeba Tanzania na kuiweka kwenye chati ya kimataifa kwenye fani hiyo ya muziki wa kizazi kipya. Na ninaposema ngazi ya kimataifa sina maana ya kuvuka tu mipaka ya nchi na kuingia nchi za jirani kama Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia, Malawi, Msumbiji wala Kongo, kama ambavyo wameweza kufanya wasanii wengine wa muziki huo wa hapa nchini, ninamaanisha kimataifa kwa maana halisi. Nalenga nchi za mbali na Tanzania.

Muziki wa Diamond kwa sasa unapigwa kwenye nchi mbalimbali za Afrika, ukiondoa nchi za Kiarabu kwa upande wa Afrika Kaskazini, ambako sina uhakika kama muziki wa kizazi kipya una mashabiki kulingana na utamaduni wa huko.

Kwa maana hiyo Diamond kaiweka Tanzania kwenye chati ya kimataifa kwa maana halisi kimuziki. Kwa  sasa msanii huyo anakula sahani moja na wasanii wa kimataifa kama kina Peter Okoye na Paul Okoye, Wanigeria wanaounda kikundi cha P Square, ambao mara kadhaa wamemuomba watoe naye vibao vya pamoja. 
Pia yuko kwenye kiwango cha wanamuziki kama Youssou N’Ndour wa Senegal na wengine wa aina hiyo.

Kwa eneo hili la Afrika Mashariki, nashindwa kumtofautisha Diamond na Joseph Mayanja ‘Chameleone’. Kwa sasa wanamuziki hao wanafanana.

Tanzania iliwahi kuvuma sana duniani miaka ya nyuma kupitia kwa wanamichezo, hususan wanariadha, kina Filbert Bayi, aliyewahi kuwa bingwa wa mbio za mita 1500 duniani, ambaye mpaka sasa anashikilia rekodi ya mbio hizo kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola aliyoiweka mjini Christchurch nchini New Zealand mwaka 1974. Wengine ni Seleman Nyambui, Adventina Mtakyawa, Juma Ikangaa, Gidmas Shahanga na wengine wengi.

Lakini kutokana na umri kuwatupa mkono nyota hao,  jina la Tanzania limefifia katika tasinia ya michezo na kuifanya nchi yetu isahaulike kabisa kana kwamba haipo kwenye nyanja ya michezo na burudani!

Hivyo Diamond ni kijana aliyedhamiria kulipandisha tena jina la nchi yake kupitia tasnia ya burudani. 
Na niseme kwa uhakika kabisa kwamba ameweza. Hilo linashadidiwa na tuzo mbalimbali za kimataifa anazozipata kwa sasa kwa upande huo wa burudani baada ya kushindanishwa na wasanii wengine wa kimataifa toka nchi mbalimbali.

Kitu cha kipekee nilichokigundua kwa Diamond na kuhisi kwamba pengine ndicho kinachochochea mafanikio yake ni tabia yake ya kusikiliza ushauri na kuufanyia kazi.

Wakati fulani nilimpa changamoto, ambayo vilevile niliwahi kuitoa kwa Chameleone nilipokutana naye Jijini Mwanza, Mei mwaka jana, kwamba kwa kiwango alichopo hapaswi kuendelea kuimba muziki kwa kutumia mtindo wa “Play back”,  kwamba anatakiwa kuwa na vyombo vyake na kupiga muziki live. Diamond kanielewa na kusema kwamba hilo analifanyia kazi kwa bidii kubwa.

Kingine ni namna anavyoendesha mahusiano na jamii aliyomo.
 Kawaida kuna dhana ya kwamba wasanii ni watu wasioeleweka vizuri ndani ya jamii, wahuni na huo kuwa mwanzo wa neno usanii, kwamba fulani kanifanyia usanii ikiwa na maana ya kanifanyia uhuni.

Lakini hilo ni tofauti  kwa Diamond. Yeye anapenda kuwasaidia wenye mahitaji kulingana na hali halisi ilivyo. Kipindi fulani kwa mfano, kwa kuuthamini mchango wa Baba wa Muziki hapa nchini, Marehemu Muhidini Maalim Gurumo, aliamua kumpatia gari jipya. Huo ni usanii kwa upande wa pili anaouonyesha Diamond tofauti na upande uliozoeleka kwa jamii.

Diamond anasema kwamba amejipangia kila mwezi kuwa anatembelea vituo vya watoto yatima na kutoa misaada mbalimbali kadri inavyowezekana. Huo ni mchango mwingine katika jamii anaoufanya kijana huyo.

Anawashauri vijana wenzake, hasa wasanii, wanaojiingiza kwenye ulevi uliopindukia pamoja na matumizi ya dawa za kulevya waache mambo hayo mara moja. Anasema kwamba yanaharibu vipaji na wakati mwingine kupoteza maisha. Anasema ili kulinda kipaji chake yeye anahakikisha anaepukana na mambo hayo yasiyo na maana na yaliyo hatari kwa maisha ya binadamu.

Diamond anasema kwamba alizaliwa Septemba 22, 1990, Kigoma.

Anasema kwamba kilichomfanya aingie kwenye muziki ni kipaji chake kilichojitokeza tangu akiwa shule ya msingi. alikuwa akiimba kwenye kwaya ya shule na burudani nyingine za shuleni.

Huyo ndiye Diamond Platnumz, ambaye wasanii wengine vijana wanapaswa wamtumie kama kipimo ya mafanikio katika muziki wa kizazi kipya wanaoufanya. Bila shaka watakaofuata mwenendo wake watafanikiwa kama yeye alivyo.

No comments:

Post a Comment

Pages