HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 13, 2022

Fahamu UTT AMIS inavyowezesha wawekezaji wadogo, wakubwa kuwekeza kwa ufanisi

Na Mwandishi Wetu
 
 
UTT AMIS ni taasisi ya Serikali ya Tanzania iliyo chini ya Wizara ya Fedha ambayo dhumuni lake kuu ni kuanzisha na kuendesha mifuko ya uwekezaji wa pamoja hapa nchini ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kujiwekea akiba na kuwekeza katika masoko ya fedha na mitaji.

Changamoto kubwa iliyopo ni kwamba bado hali ya utamaduni wa kuweka akiba na kuwekeza katika masoko ya fedha na mitaji bado iko chini  kwa sababu za kihistoria, kijamii, kiuchumi na wakati mwingine sababu huwa ni kipato kidogo  na mahitaji ni mengi. Ukweli unabaki ya kuwa hakuna siku fedha zinaweza kutosha. 
 
 
Hivyo inamlazimu kujenga nidhamu na tabia ya kujiwekea akiba ya fedha kutokana na kipato anachapata.
 
Siyo jambo rahisi kuweza kuweka akiba ya fedha, lakini ili uweze kufanya hivyo ni muhimu kujenga nidhamu katika matumizi yetu.  
 
Afisa Masoko na Uhusiano wa UTT AMIS, Rahim Mwanga anasema “Suala si kuweka akiba na kuwekeza tuu, ila tunatakiwa kuweka akiba na kuwekeza kwa ufanisi ambao ni Uwekezaji unaozingatia kuwa na malengo, kuweka mpango wa kufikia malengo na muda. Mfano lengo ni kuwa na milioni 5, kwa muda wa miaka 3 na utawekeza kila mwezi. Hiyo ndiyo itakayo kuwa dira ya kukuwezesha kufika malengo.
 
 
Afisa Masoko na Uhusiano wa UTT AMIS, Rahim Mwanga anasema, "Siku zote ukiwa na akiba ya fedha unatakiwa kuziwekeza. Uwekezaji ni dhana pana, kwa mfano, mwingine anataka kununua kiwanja, mwingine aanzishe biashara, mwingine ampeleke mtoto shule, mwingine akasome yeye mwenyewe, lengo likiwa ni kwamba ile fedha ya akiba ilete matokeo chanya kwake. Hata hivyo, inatakiwa ieleweke kwamba kuna muda kati ya kuweka akiba, kuwekeza na kutimiza lengo. 
 
 
Kwa mfano, ninataka kuweka akiba kwa ajili ya elimu ya mwanangu ambaye ana mwaka mmoja sasa, kwa hiyo kuna miaka miwili au mitatu baadaye aanze chekechea, kwa hiyo nikiweka akiba tu katika sehemu ambayo haikuwi katika  miaka mitatu hiyo maana yake itakuwa haina tija kwa sababu hapo katikati lazima kutakuwa na mfumuko wa bei na mambo mengine, kwa hiyo kinachotakiwa ni kuwekeza fedha hizo za akiba kabla ya kuja kufanya uwekezaji wa kumpeleka mtoto shule.
 
 
Kwa hiyo hapa katikati niwekeze wapi sehemu ambayo ipo salama au itanipa tija nzuri na haitanihitaji kuhangaika sana. Sasa sehemu hizi watu wengi hawajazichangamkia. Sehemu hizo ni katika masoko ya fedha na masoko ya mitaji."
 
 
Anasema, "Tunapozungumzia masoko ya mitaji mfano wake ni Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), kwani katika soko hili kuna makampuni yamejiorodhesha yakiuza mitaji na kutafuta mitaji kwa kuuza hisa, kwa hiyo ni sehemu mojawapo ambayo watu wanaweza kwenda kuwekeza pia katika dhamana za serikali za muda mrefu.
 
 
Dhamana za kapuni(Corporate bonds) na katika Vipande. Sehemu nyingine ni katika masoko ya fedha huku kuna akaunti za muda maalumu (fixed deposit accounts) na akaunti ambazo hazina muda maalumu (call deposit accounts), pia kuna dhamana za Serikali.
 
 
Mwekezaji anaweza  kuwekeza moja kwa moja katika dhamana hizo hapo juu, lakini kuna changamoto za mwekezaji mmoja mmoja kufikia soko na kunufaika kikamilifu, kama vile elimu ya kutosha, urahisi wa kuwekeza na kutoka na faida nzuri. 
 
 
Lakini kupitia UTT AMIS changamoto hizo zinapungua kupitia kuwekeza kwenye mifuko ya uwekezaji wa pamoja. Mifuko ya uwekezaji wa pamoja ni fursa inayomuwezesha mtu mmoja mmoja au taasisi, kampuni kuwekeza rasilimali fedha zao kupitia UTT AMIS(Meneja) na UTT AMIS kazi yetu  ni kuwekeza kwa niaba yao yaani mtu mmoja mmoja, taasisi au makampuni katika dhamana hizo kulingana na sera ya Uwekezaji ya mfuko."
 
 
Anasema, " Umiliki wa Uwekezaji katika  katika mfuko wa uwekezaji wa pamoja huitwa kipande (unit). Miongoni ya faida kubwa ambayo mwekezaji anaipata kwa kujiunga na mifuko ya uwekezaji wa pamoja badala ya kuwekeza mmoja mmoja katika masoko ya fedha na masoko ya mitaji ni  faida shindani ukilinganisha na baadhi ya bidhaa za aina hiyo sokoni."
 
 
Mwanga anasema, "Kwa mfano, katika benki tukitumia akaunti ya muda maalumu (fixed deposit accounts), katika akaunti hii benki inamlipa mwekekezaji anayewekeza katika akaunti hiyo kulingana na muda na kiasi anachowekeza na kiwango cha chini cha kuwekeza katika benki ni milioni moja au laki tano. 
 
 
Kwa mwaka huwa benki zinatoa riba ya asilimia tatu hadi sita au saba, lakini kama ukiwekeza kiasi kikubwa katika mabenki unakuwa katika nafasi ya kupata riba nzuri, kwa mfano kuanzia milioni 500 na kuendelea unaweza kupata riba ya kuanzia asilimia 10 hadi 11  kulingana na kiwango cha fedha , uhitaji wa ukwasi wa benki na hali ya uchumi."
 
 
Anasema, "Hapo ndipo inapokuja dhana ya uwekezaji wa pamoja, kwamba kila mtu kutokana na uwezo wake anaweza kupeleka fedha katika mfuko na hivyo kwa pamoja meneja wa mfuko yaani UTT AMIS kuwa na kiwango kikubwa. Kwa mfano kikifika kiwango cha bilioni 2, mfuko unakuwa na uwezo wa kuweza kuzungumza na benki na kupata riba nzuri. 
 
 
Kwa mfano benki inaweza kukubali kutokana na uwekezaji wa kiasi hicho cha fedha na kutoa riba ya asilimia 10 kwa mwaka, kwa hiyo ina maana kila aliyewekeza naye atafaidika kwa asilimia 10. 
Yaani aliyewekeza Sh 20,000 atatapata faida ya asilimia 10, aliyewekeza Sh. 30,000 atapata faida ya asilimia 10 na aliyewekeza 20 milioni atapata faida ya asilimia 10."
 
 
Kwa kifupi ni kwamba, faida ya kwanza ya dhana ya uwekezaji wa pamoja ni kuwawezesha wawekezaji wadogo, wa kati na wawekezaji wakubwa kuweka nguvu pamoja na kuwekeza ili kupata faida nzuri na shindani zaidi kuliko soko lingeweza kuwapa wawekezaji mmoja mmoja.
 
 
Faida ya pili ambayo wawekezaji wanaipata kwa kutumia mifuko ya uwekezaji wa pamoja ni uwekezaji mseto. UTT AMIS inawekeza katika masoko ya fedha na masoko ya mitaji, pia haiwekezi fedha zote katika kapu moja ili kuhakikisha kunakuwa na usalama wa fedha za mwekezaji, kupata faida nzuri na ukwasi (liquidity) yaani mtu akiihitaji fedha yake aweze kuipata kwa uharaka na pia kwa uhakika.
 
 
Mwanga anasema, "Sasa ukiyatazama masoko ya fedha na masoko ya mitaji utaona kwenye masoko ya mitaji ambapo ndiyo kwenye hisa kunakuwa hakuna uhakika kwamba nikiwekeza katika kampuni fulani mwisho wa mwaka nitapata faida kwa hiyo inategemea na ufanisi ila faida ikipatikana huwa ni kubwa. Katika masoko ya fedha faida siyo kubwa ila kuna uhakika wa kuipata hiyo faida."
 
 
Kwa hiyo UTT AMIS inachokifanya ni kutawanya inachokipita, kwamba kama wanapata Sh. 100 basi Sh. 60 wataipeleka katika sehemu salama zaidi kwenye masoko ya fedha, yaani Sh 30 kwenye akaunti ya muda maalumu (fixed deposit accounts), Sh 10 akaunti ambazo hazina muda malumu (call deposit accounts), Sh. 10 treasury bills (dhamana za muda mfupi), Sh 10 treasury bonds (dhamana za muda mrefu). 
 
 
Sh 40 iliyobaki itatawanywa kwenye makampuni katika soko la hisa, yaani Sh 3 zitapelekwa labda DCB, Sh 8 TBL, Sh 10 TCC, Sh 4 Twiga. Kwa hiyo kama kutatokea mdororo kwenye sehemu moja basi sehemu nyingine itaibeba sehemu nyingine katika kuhakikisha usalama wa mali na ndiyo maana uwekezaji unatawanywa.
 
 
Kampuni ya UTT AMIS inasimamia mifuko sita ya uwekezaji wa pamoja ambayo ni Mfuko wa Umoja, Mfuko wa Wekeza Maisha, Mfuko wa Watoto, Mfuko wa Kujikimu, Mfuko wa Ukwasi na Mfuko wa Hati Fungani.  

MFUKO WA UMOJA
Umoja ni mfuko wa wazi wenye uwiano sawa wa uwekezaji unaoufanya kuwa mfuko bora wenye hatari za uwekezaji wa kiwango cha kati.
 
 
Mfuko wa Umoja unawekeza kiwango kisichozidi asilimia 50 ya fedha zake kwenye hisa zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa la Dar es salaam na asilimia 50 nyingine huwekezwa kwenye dhamana zenye kutoa mapato ya kudumu.
 
 
Sera ya uwekezaji kwa upande mmoja ni mpango madhubuti uliowekwa na mfuko ili kutawanya rasilimali zake. Kwa upande mwingine ni mpango mkakati na ni kinga endapo eneo moja la uwekezaji likifanya vibaya. 
 
 
Aidha, uwekezaji kwenye hisa huwekezwa kwa kiwango cha chini ikilinganishwa na eneo lenye mapato cha kudumu.
 
 
Ni mfuko wa kwanza kuanzishwa na umekuwa sokoni tangu mwezi wa tano mwaka 2005. Kwasasa mfuko unathamani inayozidi bil. 291 na wawekezaji zaidi ya 95,000. Kwa muda mrefu sasa mfuko umekuwa ukitoa faida nzuri iliyo kati ya asilimia 10 mpaka 20 (baada ya makato ya kodi).
 
 
Mwekezaji wa mfuko wa Umoja anaweza kuuza vipande vyake muda wowote, pesa ataipata ndani ya siku kumi za kazi toka alipowasilisha maombi. Hakuna kipindi cha kizuizi.
 
 
Gharama za kuuza vipande vya mfuko ni asilimia 1 ya thamani ya kipande ambayo ni nafuu zaidi sokoni kwa kulinganisha na asilimia 10 ya kodi atakayokatwa mteja anayetoa fedha zake alizoweka kwenye akiba ya muda maalumu ya benki.
 
 
Tathmini ya thamani halisi ya mfuko itakokotolewa kila siku ya kazi na thamani ya kipande kutangazwa.
 
Usalama wa fedha za mwekezaji ni mkubwa kwasababu mfuko unasimamiwa na taasisi ya serikali yenye kuaminika. Pia mfuko unatoa faida shindani,ukwasi na usalama kwa fedha za mwekezaji. Kwa kuzingatia maelezo hayo, unaweza kuwekeza kiwango cha kawaida kabisa katika mfuko wa Umoja na utawezeshwa kufuatilia maendeleo yake kwa ukaribu.


MFUKO WA UWEKEZA MAISHA
Wekeza Maisha ni mfuko wa kwanza wa uwekezaji wa pamoja kuanzishwa na kampuni ya UTT AMIS nchini wenye faida za bima ya maisha ndani yake.
 
Zaidi ya asilimia 99 za fedha za wawekezaji wa mfuko wa Wekeza Maisha huwekezwa kwenye masoko mbalimbali ya fedha na asilimia 1 kwa ajili ya malipo ya bima.

Mambo muhimu kuhusu mfuko wa wekeza maisha.
Madhumuni: Mfuko huu ni mpango wa wazi na wa muda mrefu unaokusudia kukuza mtaji na kwa wakati huo huo kutoa kinga ya bima ya maisha, bima ya ajali/ulemavu wa kudumu na gharama za mazishi.
 
Chaguo la mpango wa uwekezaji: Mfuko unatoa fursa mbili za uwekezaji: (a) Mpango wa Uwekezaji kwa Awamu na (b) uwekezaji wa mkupuo.

Nani anaruhusiwa Kuwekeza:  Mfuko uko wazi kwa Mtanzania aliye ndani au nje ya nchi na awe mwenye umri kati ya miaka 18 hadi 55.
 
Ukomo wa Uwekezaji: Uanachama wa mwekezaji katika mfuko huu utakoma baada ya miaka 10.

Ukwasi: Uuzaji wa sehemu ya uwekezaji (vipande) katika mfuko) unaruhusiwa baada ya miaka mitano.

Thamani ya mwanzo ya kipande:  Thamani ya mwanzo ya Kipande (face value) ilikuwa Sh.100.

Bei ya kipande: Bei ya Kipande wakati wa mauzo ya mwanzo, yaani kuanzia tarehe 16 Mei, 2007 hadi Julai 31, 2007 ilikuwa ni Sh.100/= na baada ya hapo Kipande kinauzwa kulingana na thamani halisi. Mfano thamani ya bei ya kipande kwa tarehe 31 mwezi wa nane ilikuwa ni sh. 719.1915.
 
Kiwango cha kuwekeza: Kiwango cha chini kwa uwekezaji kwa miaka kumi ni Sh1 milioni na hakuna kiwango cha juu cha kuwekeza (isipokuwa mafao ya bima ya maisha yatatolewa mpaka kufikia kiwango cha Sh 25 milioni tu).

Milioni hii moja inaweza kuwekezwa kwa awamu au kwa mkupuo.  Kiwango cha chini cha uwekezaji wa awamu ni Sh.8,340/= kwa kila mwezi.

Mafao ya bima ya maisha Kifo au ulemavu wa Kudumu;

Mpango wa kuwekeza kwa Awamu: Kinga ya bima ya maisha ina thamani sawa na kiasi kisicholipwa na mwekezaji kwa muda uliosalia katika mpango wake wa uwekezaji. 

Mpango wa Kuwekeza kwa Mkupuo: Kinga ya Bima ya Maisha ina thamani sawa na kiwango alichochagua mwekezaji. (Muhimu: kiwango cha juu cha kulipwa ni Sh. milioni 25).

Mafao ya bima ya ajali: Mwekezaji atalipwa asilimia 20 ya kiwango kilichokusudiwa katika mpango wa uwekezaji, hata hivyo kiwango cha juu ni Sh5 milioni tu.

Mafao ya gharama za mazishi: Kila mwekezaji atalipwa Sh.500, 000/= kwa ajili ya mazishi endapo atafariki bila kujali kiwango alichowekeza. 

Mkono wa Pongezi:  Mfuko utatoa mkono wa pongezi kwa mwekezaji ambaye atakamilisha miaka kumi ya mpango wake wa uwekezaji au kama atafariki ndani ya mwaka wa mwisho wa mpango wake wa uwekezaji.

 

MFUKO WA WATOTO

Mfuko huu ni mpango uliowazi kwa watoto unaokusudia kukuza mtaji kwa muda mrefu kupitia uwekezaji wa mseto kwa kuwekeza kwenye hisa zilizoorodheshwa kwenye soko la hisa na dhamana.

Umriwa Mtoto wa Kujiunga na Mfuko: Uwekezaji unafanywa kwa jina la motto aliye chini ya miaka18.

Nani anaruhusiwa kuwekeza

Mfuko uko wazi kwa watanzania walio ndani na nje ya nchi kama watubinafsi, kampuni, taasisi, benki, asasi za kiraia.  Uwekezajiufanywe kwa manufaa ya mtoto.
 
Uwiano wa Rasilimali: Mfuko utawekeza katika uwiano wa dhamana zenye mapato ya  kudumu asilimia 0 hadi asilimia 100 na hisa zilizoorodheshwa asilimia 0 hadi asilimia 50.

Chaguo la mpango wa uwekezaji: Mfuko unatoa fursa za kukuza mtaji. kiwango cha chini cha kuwekeza:(a) kiwango cha chini cha kuwekeza ni Sh.10,000 na (b) kiwango cha chini cha uwekezaji wa nyongeza utakuwa Sh.5,000. Hata hivyo hakuna kima cha juu cha kuwekeza.

Ukwasi:Uuzaji wa vipande vyote /sehemu ya vipande vilivyowekezwa unaruhusiwa pale mtoto mnufaika anapotimiza miaka 12.

Hata hivyo uuzaji wa vipande vyote au baadhi unaweza kuruhusiwa pale inapolazimu, mfano mahitaji ya fedha kwa ajili ya matibabu kwa ajili ya mototo mnufaika au kwa ajili ya sababu nyingine ya msingi.

MFUKO WA JIKIMU

Madhumuni

Mfuko huu ni mpango uliowazi wenye lengo la kukuza na kutoa gawio kutokana na mapato ya ziada katika vipindi tofauti na pia kukuza mtaji kwa mwekezaji wa muda mrefu.

Chaguo la mpango wa uwekezaji

Mfuko unatoa fursa mbili za uwekezaji-Mapato ya robo mwaka na mapato ya mwaka yaliyoambatanishwa na ukuaji wa vipande.

Nani anaruhusiwa kuwekeza: Mfuko uko wazi kwa watanzania waliondani na nje ya nchi, watu binafsi, kampuni / taasisi,mabenki, asasizakiraia (NGO) kama inavyoonyeshwa kwenyewaraka huu.

Kiwango cha chini cha kuwekeza: Ni Sh. milioni 2 kwa mpango wa mapato ya robo mwaka na Sh milioni 1 kwa mpango wa gawio kwa mwaka na Sh. 5,000 kwa mpango wa ukuaji wamtaji kwa mwaka.

Uwekezaji wa nyongeza: Kiwango cha chini cha uwekezaji wa nyongeza/unaofuata ni Sh 15,000 kwa mpango wowote wa gawio na Sh 5,000 kwampango wa ukuaji wa mtaji kwa mwaka, hakuna ukomo wa kiwango cha kuwekeza.

Makato ya kodi: Kulingana na sheria za sasa, kodi ya mapato haitotozwa kwenye gawio litokanalo na uwekezaji kwenye mfuko huu.

Uhamishaji wa Vipande: Uhamishaji wa vipande kutoka kwenye mfuko mmoja kwenda mwingine kati ya mifuko inayoendeshwa na Dhamana ya Uwekezaji Tanzania unaruhusiwa. Uhamishaji huu utatumia thamani halisi ya kipande kwa wakati huo bila gharama yoyote.

Uhamishaji huo utafanywa kwa mauzo ya vipande kutoka kwenye mfuko mmoja na kuviwekeza kwa kununua vipande kwenye mfuko mwingine, ilimradi sifa za kuwekeza kwenye mfuko mwingine zimezingatiwa.

MFUKO WA UKWASI

Madhumuni: Mfuko huu ni mpango ulio wazi unaotoa njia nyingine ya uwekezaji kwa wawekezaji wanaotaka kuweka fedha zao kwa kipindi cha muda mfupi na katika kiwango kilichopo kwenye ushindani. Hatari/athari kidogo katika uwekezaji na ukwasi wa hali ya juu ndio dhumuni hasa la mfuko huu.

Sera ya uwekezaji: Kiwango cha chini cha uwekezaji katika masoko ya fedha na dhamana zenye kutoa mapato ya kudumu 100%

Chaguo la mpango wa uwekezaji: Mfuko huu unatoa fursa ya kukuza mtaji na mwekezaji anaweza kujitoa katika Uwekezaji wakati wowote pasipo na gharama.

Nani anaruhusiwa kuwekeza: Mfuko uko wazi kwa mtanzania aliye ndani au nje ya nchi, inahusisha watu binafsi (ikijumuisha watoto), na wawekezaji wasio watu binafsi kama mifuko ya pensheni, benki/mashirika taasisi za serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, asasi zisizo za kiserikali na Mashirika mengineyo n.k

Kiwango cha chini cha uwekezaji: a) Uwekezaji wa mwanzo= Shs 100,000 mauzo yanayofuata, Shs 10,000

Kiwango cha juu cha uwekezaji: Hakuna kiwango cha juu cha kuwekeza.

Umiliki wa Vipande: Umiliki wa mtu mmoja na umiliki wa pamoja unaruhusiwa katika mfuko huu. Hata hivyo, umiliki wa pamoja hauzihusu taasisi/kampuni.

Ukwasi: Baada ya kipindi cha utulivu kumalizika, uuzaji wa vipande utafanyika kila siku ya kazi. UTT AMIS itatuma malipo ya mauzo ya vipande ndani ya siku tatu za kazi baada ya kupokea fomu za maombi. Fedha za mauzo zitatumwa moja kwa moja katika akaunti ya benki ya mwekezaji.

Tozo la kujiunga na kujitoa: Mwekezaji hatotozwa gharama yeyote ya kujiunga au kujitoa katika mfuko

Kigezo: Dhamana za Serikali za siku 35.

Ulinzi wa mtaji: Lengo kuu ni kulinda mtawanyo wa uwekezaji ili kutoathiri thamani ya vipande huku mtazamo mkuu ukiwa ni kipato cha uhakika.
 

MFUKO WA HATI FUNGANI

Huu ni mfuko unaowekeza katika hati fungani za serikali, makampuni na katika masoko ya fedha. Hivyo hutoa faida ya uhakika kulingana na hali ya soko. Kiwango cha chini cha kuanza kuwekeza ni  50,000 kwa mpango wa kukuza mtaji ,10,000,000 kwa mpango wa gawio kila mwezi na shilingi 5,000,000 kwa mpango wa gawio kila baada ya miezi sita. Nyongeza kwa mipango yote mitatu shilingi 5000 au zaidi.

Kuwekeza kwa kutumia simu kwa kubonyeza namba *150*82#, Kufahamu zaidi tembelea www.uttamis.co.tz au piga bure; 00800112020.

No comments:

Post a Comment

Pages