HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 12, 2015

Mkutano Mkuu wa Masafa wa ITU Wakubaliana Kupanga Masafa Ya Kufuatilia Ndege Angani Kuongeza Usalama wa Anga

Na Innocent Mungy, Geneva

Leo Jijini Geneva, Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa ITU wa Masafa umeamua na kukubaliana kutenga masafa maalumu kwa ajili ya kufuatilia ndege za abiria kokote zinapokuwa angani ili kuepusha majanga kama ya ya Malaysia iliyopotea na ambayo haijapatikana hadi leo. Uamuzi huu utakamilika mwaka 2017 ambapo mawasiliano na ndege zote za abiria zitakuwa zinajulikana zilipo.

Mkutano huu umekubaliana masafa ya bandi 1087.7-1092.3 MHz yatengwe kwa shughuli za usafiri wa anga (aeronautical mobile-satellite service - Earth-to-space) kwa ajili ya mawasiliano kati ya ndege zikiwa angani na vituo vya mawasiliano katika satelaiti na vituo vya mawasiliano ardhini kutoka kwenye ndege, (reception by space stations of Automatic Dependent Surveillance-Broadcast (ADS-B) emissions from aircraft transmitters)

Masafa ya bandi 1087.7-1092.3 MHz kwa sasa yanatumika kusafirisha taarifa za mawasiliano ya ndege na vituo vilivyoko ardhini katika njia inayosafiri ndege tu. Mkutano huu wa Kimataifa wa Masafa sasa umetenga masafa haya kote duniani kutumika kutoka ardhini kuelekea angani kuwezesha mawasiliano kutoka kwenye ndege na kwenye satelaiti. Hii itapelekea sasa ndege kuonekana kokote iliko hata kama iko nje ya njia yake ya safari au ikipotea. Hii ina maana ndege zote zenye kifaa hicho (Automatic Dependent Surveillance-Broadcast - ADS-B) ambapo kifaa hicho kitakuwa kinatoa taarifa popote ndege ilipo, iwe baharini, kwenye nja ya dunia au maeneo ya mbali.


Makubaliano haya yanafuatia kupotea kwa ndege ya Malaysia MH370 mwezi machi 2014 ikiwa na abiria 239 na kuleta gumzo kubwa duniani baada ya jitihada za kuitafuta kukosa mafanikio. ITU na ICAO (Shirika la Kimataifa la Usalama wa Anga ndio waratibu wa mafanikio haya.

ICAO katika mkutano wake maalumu uliojadili ufuatiliaji wa ndege zikiwa angani (global flight tracking), uliofanyika mjini Montreal tarehe 12-13 Mei 2014, ambapo ICAO iliishauri ITU kuchukua hatua za haraka kupanga masafa maalumu kwa yan kufuatilia ndege za abiria zikiwa angani kutokana na mahitaji ya usalama wa anga duniani. Hata hivyo mwezi Oktoba mwaka 2014. ITU kupitia Mkutano wake Mkuu unaofanyika kila baada ya miaka 4 (ITU Plenipotentiary Conference) uliofanyika mjini Busan, Jamhuri ya Korea Kusini, iliagiza Mkutano mkuu wa Masafa wa Dunia kuweka ajenda ya kugawa masafa maalumu kwa kufuatilia ndege za abilria zikiwa angani.

Akizungumza baada ya makubaliano haya mjini Geneva leo alasiri, Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa mataifa linalosimamia Mawasiliano,  Houlin Zhao, amesema kufikiwa kwa uamuzi huu kumewezesha dunia kutoa kipaumbele kwa maamuzi ya haraka kuhusu usalama wa ndege kwa kupanga masafa nya kufuatilia ndege angani. Aliuhakikishia Mkutano huu kuwa ITU itafanya kila inaloweza kuhakikisha usalama wa unga unafanikiwa kwa ufanisi Zaidi.

“Tutaendelea kufanya kazi na ICAO kuhakikisha ufuatiliaji wa ndege zikiwa safarini ni wa uhakika ili kuepusha majanga yaliyotokea huko nyuma” alisema Zhao. Aidha François Rancy, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya usimamizi wa msafa ya radio wa ITU. Amesema ITU itakuwa mstari wa mbele kushirikiana na ICAO kulinda usalama wa wasafiri wakiwa angani ndani ya ndege.

Naibu Mkurugenzi wa Masafa wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Eng. Khatibu Othman amesema uamuzi huu ni muhimu kwa nchi kama Tanzania kwani itawezesha sasa Wasimamizi wa Usalama wa anga Tanzania (TCIA) kuweza kufuatilian ndege za Tanzania  Tanzania na zinazopita kwenye anga letu kwa usalama Zaidi. Hali kadhalika amesema itakuwa rahisi sasa kujua ndege Fulani iko wapi kokote duniani hata ikipotea.  “Huu ulikuwa mmoja ya misimamo yetu tangu tunatoka nyumbani kuhakikisha tunapanga masafa kwa ajili ya sualka hili.

Mjumbe wa mkutano huu kutoka ~Mamlaka ya Usimamzi wa usalama wa Anga nchini (TCIA) Mrs. Valentina Kayombo, amesema kuna faida nyingi sana kwa uamuzi na makubalioano haya, ikiwa ni pamoja na kuweza kujua ndege iko wapi endapo itapata matatizo kwa ajili ya uokoaji, utawezesha kuona mahali ndege ilipo ikipta hitilafu hewani na kuweza kupanga nini cha kufanya haraka na pia kuwa na uhakika wa usalama wa ndege hata ikiwa mbali. “Hii itafanya tuweze kutekeleza kazi zetu kwa ufanisi Zaidi kama wasimamizi wa usalama wa anga” alisema mama Kayombo.


Mhandisi Samson mwela, mjumbe wa mkutano huu kutoka Tanzania amesema kuwa uamuzi huu nuliotolewa na nchinwanachama wa ITU unadhihirisha kwamba suala la usalama wa anga limepewa umuhimu mkubwa na mataifa yote. “Hii iyaimarisha mawasiliano na usalama katika sekta ya anga”, amesema Mwela.

Mkutano huu ulioanza tangu tarehe 2 mwezi Novemba unaendelea hadi tarehe 27 Novemba 2015, ambako ajenda mbalimbali bado ziko katika hatua za majadiliano na makubaliano kutiwa sahihi nan nchi wananchama wa ITU, Tanzania ikiwa mojawapo. Ujumbe wa Tanzania unaongozwa na Balozi Mwakilishi wa Kuduma wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Geneva, Uswiss, Balozi Modest Mero.

No comments:

Post a Comment

Pages