HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 20, 2016

BALOZI MDOGO WA OMAN AFARIKI DUNIA ZANZIBAR

Balozi Seif akibadilishana mawazo na Makamu Mkuu wa Mabalozi wa Oman Bwana Ahmed Mohamed Al – Muzaini wa kwanza kutoka kushoto na Afisa wa Uhamiaji wa Ubalozi huo wa kwanza kutoka kulia Bwana Hilal Ali–Dhuhli mara baada ya kutia saini kitabu cha maombolezo.

Viongozi mbali mbali wa Kitaifa, wanadiplomasia pamoja na baadhi ya wananchi wakiwemo wenye asili ya Oman wameweka saini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Balozi Mdogo wa Oman hapa Zanzibar Marehemu Ali Abdalla Al – Rashid.

Balozi Ali alifariki dunia ghafla juzi katika Hospitali ya Global iliyopo vuga Mjini Zanzibar wakati akipatia matibabu baada ya kusumbuliwa na tatizo la sindikizo la Damu { Blood Presure }.

Kitabu hicho cha maombolezo kimewekwa Ofisi ya Ubalozi wa Oman iliyopo Migombani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar Viongozi na wananchi hao waliweka saini hizo akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed.

Mwanadiplomasia huyo wa Ubalozi wa Oman aliyefanya kazi za kibalozi kwa takriban miaka miwili tayari ameshasafirishwa kutoka Zanzibar na kurejeshwa Nyumbani kwao Oman kwa shughuli za Mazishi.

Akizungumza na Maafisa wa Ubalozi Mdogo wa Oman wakiongozwa na Makamu Balozi  Mkuu wa Oman Bw. Ahmed Mohamed Al – Muzaini hapo Migombani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliwaomba watendaji hao kuwa na moyo wa subra kutokana na mtihani wa kuondokewa na Kiongozi wao.

Balozi Seif alisema licha ya kwamba kifo kimeumbwa na lazima kiiguse kila nafsi kwa mujibu wa Kitabu Kitukufu  na amri ya Mwenyezi Muungu lakini kuondoka ghafla kwa Balozi Ali Abdalla Al – Radhid kutaacha pengo sio tu kwa Oman pekee bali hata kwa Zanzibar na wananchi wake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimtaja Balozi Ali Abdalla kuwa ni Mwanidiplomasia aliyeonyesha kipaji kikubwa kilichomuwezesha kutekeleza majukumu yake kwa uweledi mzuri  uliosaidia kuunganisha uhusiano wa Kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na Oman.

Alifahamisha kwamba Zanzibar imepata mafanikio makubwa kimaendeleo na kiutamaduni kutokana na mchango wa Balozi Ali Abdalla katika kipindi chake cha utumishi hapa Zanzibar.

Balozi Seif aliyataja baadhi ya mafanikio hayo kuwa ni pamoja na ziara za wafanyabiashara mbali mbali wa Oman walioonyesha nia ya kutaka kuanzisha miradi ya kiuchumi, misaada ya mawasiliano pamoja na mikutano ya ushirikiano katika sekta za Sanaa na Utamaduni.

Naye Makamu Balozi Mkuu wa Oman Bw. Ahmed Mohamed Al – Muzaini kwa niaba ya watendaji wa Ofisi hiyo ya Ubalozi Mdogo wa Oman hapa Zanzibar ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Watendaji wake waliosaidia nguvu na mawazo katika jitihada za kuusafirisha mwili wa Kiongozi huyo.

Bwana Ahmed alisema kitendo hicho mbali ya kuleta faraja kwa Uongozi pamoja na watendaji wa Ofisi hiyo lakini pia kimepongezwa na Uongozi wa juu wa Serikali ya Oman.
Wakati huo huo Uongozi wa Shamba la Kuku Maruhubi { Zanchick } umekabidhi stakabadhi ya kuthibitisha kwamba Uongozi wa Shamba hilo tayari umeshaingiza mchango wa shilingi Milioni 10,000,000/- kwenye  akaunti ya Mfuko wa Maafa Zanzibar  kusaidia huduma za kukabiliana na maradhi ya Kipindu pindu Zanzibar.

Akimkabidhi mchango huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kiongozi wa Shamba hilo Ndugu Issa Kassim  alisema Uongozi wa Shamba hilo uko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuunga mkono juhudi za kusaidia kuimarisha huduma za Kijamii hapa Nchini.

Ndugu Issa alisema Zanchick imekusudia kuongeza mipango yake ya uwekezaji kwa kuanzisha kiwanda cha kutengeneza chakula cha kuku kitakachouzwa kwa wafugaji wadogo wadogo kwa lengo la kuimarisha mifugo yao na kupata kipato cha kukidhi mahitaji yao ya kimaisha.

Akipokea stakabadhi hiyo ya uthibitisho wa mchango wa fedha za huduma za kipindu pindu Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema agizo la Serikali la kusitisha biashara mbali mbali limesaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa ueneaji wa maradhi ya kipindupindu.

Balozi Seif alisema hali ya kipindi pindu siku chache zilizopita ilikuwa mbaya sana kiasi kwamba ilifikia wakati kambi ya maradhi hayo ikipokea wagonjwa kumi kwa siku  hali ambayo kwa sasa imeleta faraja ya kuwepo kwa wagonjwa wawili tu katika Kambi hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushukuru Uongozi wa Shamba la Kuku Maruhubi { Zanchick } kwa kuguswa na mripuko wa maradhi ya kipindu pindu ambayo yameleta maafa kwa wananchi kadhaa.

Uongozi wa Shamba la Kuku Maruhubi { Zanchick } ulikutana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wiki mbili zilizopita kuelezea mikakati yake ya kuwekeza kwa lengo la kusaidia wafugaji na wakulima wadogo wadogo ili waendeshe miradi yao ya uzalishaji katika misingi ya kitaaluma.


Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar


19/5/2016.

No comments:

Post a Comment

Pages