WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema mkutano wa kimataifa uliojadili jinsi ya kupambana na rushwa duniani ni kiashiria tosha kwamba tatizo la rushwa ni kubwa sana na linataka juhudi za pamoja katika kukabiliana nalo. (It’s a serious graft that needs concerted efforts).
Ametoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na Waziri wa Nchi wa Uingereza anayeshughulikia Maendeleo ya Kimataifa, Bibi Justine Greening walipokutana kwenye mkutano huo uliofanyika Lancaster House, jijini London, Uingereza.
Waziri Mkuu ambaye alihudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, alimweleza Bibi Greening kwamba viongozi wa Serikali wa awamu ya tano wameamua kwa dhati kupambana na kila ovu linalotokana na janga la rushwa na pia wameamua kuwajibika na kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea.
“Sasa hivi nchi yetu ina utamaduni mpya wa kufanya kazi na tumeamua kufanya kazi kwelikweli na siyo tena kwa mazoea, tumeamua kuweka utamaduni mpya wa kupiga vita rushwa ili kuleta uwajibikaji na uwazi miongozi mwa watu wetu,” alisema.
Alipoulizwa ni kitu kimechangia kufanya Tanzania ing’are kimataifa katika vita hii, Waziri Mkuu alijibu kwamba Tanzania imetumia mambo manne ambayo ni kuzuia rushwa isitolewe ama kupokelewa (prevention), kampeni za kuelimisha jamii, kufanya mapitio ya sheria na kuwepo kwa utashi wa kisiasa.
“Serikali inachukua hatua za kiutawala na kisheria kama vile kuanzisha mahakama maalum ya mafisadi ambayo inatarajiwa kuanza kazi mwezi Julai mwaka huu,” alisema Waziri Mkuu.
Kwa upande wake, Bibi Greening alipongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya awamu ya tano katika kupambana na rushwa na kwamba ndiyo maana Tanzania ilipewa mwaliko maalum wa kushiriki mkutano huo kwa vile baadhi ya mataifa yanaziona juhudi zinazofanywa na Serikali.
Pia alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri Mkuu kwa nia ambayo Serikali ya awamu ya tano imeionyesha katika kuwa na mpango wa kuendeleza viwanda.
Pia alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba nchi yake iko tayari kuisaidia Tanzania kwenye mpango wake ilionao wa kupeleka umeme vijijini (Rural Electrification Programe). “Tuko tayari kuwasiidia kutekeleza mpango huu kupitia taasisi ya Energy Africa Initiative ambayo inapata ufadhili kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Uingereza (DFID),” alisema.
Wakati huohuo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia masuala ya kimataifa, Bibi Sarah Sewall ameipongeza Tanzania kwa kupiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa na kusisitiza kwamba makampuni mengi ya Marekani yana nia ya kuja kuwekeza Tanzania.
“Ninaamini uwekezahji huu utasaidia kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa watu wetu. Tunampongeza Rais Dk. Magufuli kwa juhudi anazofanya na nipende kusisitiza kwamba ushirikiano baina ya Tanzania na Marekani utaendelezwa katika maeneo yetu ya siku zote,” alisema.
Waziri Mkuu alimshukuru Bibi Sewall na kumsisitiza asiache kusaidia kuwahimiza wamarekani wengi waje kutalii Tanzania na wawekezaji zaidi waje kuwekeza nchini katika nyanja mbalimbali zikiwemo uanzishaji wa viwanda, uongezaji thamani kwenye mazao yanayozalishwa nchini na kuhakiksha kuwa Watanzania wanajifunza teknolojia mpya na za kisasa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAMOSI, MEI 14, 2016.
No comments:
Post a Comment