May 20, 2016

MEYA AZINDUA ZOEZI LA UKARABATI NA UCHONGAJI WA BARABARA MANISPAA YA KINONDONI LEO

Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Mhe. Boniface Jacob leo Alhamisi 19/05/2016, amezindua mkakati wa ukarabati na uchongaji wa barabara za Manispaa ya Kinondoni.

Baada ya mvua kunyesha na kuharibu Miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali katika Manispaa ya Kinondoni, Mstahiki Meya ametoa greda la Manispaa ya Kinondoni kwa ajili ya kuanza operesheni maalum ya ukarabati na uchongaji wa barabara zilizoharibika.
Ukarabati na uchongaji wa barabara hizo umeanza leo Alhamisi 19/05/2016 katika Kata ya Mbezi.

Mstahiki Meya amesema ili kupata greda hilo inatakiwa Waheshimiwa Madiwani na Wenyeviti wa Serikali za mitaa kuchukua jukumu la kuwahamasisha wananchi wao waweze kuchangia fedha kwa ajili ya mafuta kwa ajili ya kuweka kwenye greda ili kufanya zoezi hilo la ukarabati na uchongaji wa barabara.

Greda kwa siku 1 linatumia lita 100 za mafuta (diesel) kiwango ambacho ni Shilingi 160,000/=.
"Mwananchi yeyote au Kamati inaweza kulipata greda baada ya kulipia kiasi hiko cha pesa, greda linapatikana muda wowote kwa mtu yeyote, ni kufanya malipo kwanza kisha unapata greda" ameongeza Meya Boniface.

Wananchi wanatakiwa kuhakikisha wanaandika barua na ipitishwe na diwani au Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa eneo husika.

Kwa kuanza leo Alhamisi 18/05/2016, Mhe. John Mnyika (MB) Madiwani na wananchi wake wa Goba wameomba greda lianze ukarabati na uchongaji wa barabara kwenye jimbo la Kibamba, litakuwepo huko kwa siku 10.

Leo tarehe 19/05 ni Mbezi, tarehe 20/05/ - 22/05/2016 ni Msigani, tarehe 22/05 - 24/05/2016 ni Kwembe, tarehe 26/05 - 28/05/2016 ni Goba na tarehe 28/05 - 2/06/2016 ni Saranga na Kimara.


Baada ya hapo Majimbo yatakayofuatia ni Majimbo ya Kawe, Ubungo na Kinondoni pamoja na Kata zake.
Ukarabati na uchongaji huu maalum wa barabara za Manispaa ya Kinondoni hazihusiani na miradi ya Maendeleo ya matengenezo ya barabara kwa bajeti iliyotengwa 2016/17 kama njia ya kudumu ya Uboreshaji wa barabara zote za Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni.

Akizungumza wakati wa Uzinduzi wa zoezi la ukarabati na uchongaji wa barabara za Manispaa ya Kinondoni diwani wa Kata ya Mbezi Mhe. Humphrey Samba amemshukuru Mstahiki Meya kwa kuzindua mpango huo, pia na kumshukuru Mbunge wa jimbo la Kibamba Mhe. John Mnyika kwa kuliona tatizo hilo, kwani limekuwa ni kero ya muda mrefu, pindi mvua tu zinaponyesha basi hupelekea barabara za eneo hilo kuharabika. Maeneo ambayo tayari barabara zimeshachongwa ni Msakuzi,Makabe, Mshikamano na sasa wapo eneo la Mbezi Lous na baada ya hapo wataelekea mtaa wa Msamii.

Naye M/kiti wa mtaa wa Mbezi Lous Mhe. Isidori Mushi amemshukuru Meya wa Manispaa ya Kinondoni Mhe. Boniface, kwa hatua hiyo madhubuti ya kupambana na barabara korofi za eneo hilo, pia amewashukuru wananchi wa eneo hilo kwa kuelewa, kwani Maendeleo yanakuja pale kila mmoja atakapokubali kushiriki katika kuleta Maendeleo hayo, kila Kaya inachangia Shilingi 2,000 wakiwamo wapangaji katika mitaa jambo ambalo linafanya kupatikana pesa nyingi  ambazo zinatumika kulipia greda.

Pesa hizo zikibaki zinahifadhiwa kwa ajili ya awamu nyingine ya kukarabati na kuchonga barabara hizo pindi zitakapo haribika tena, kuhusu urasimu katika pesa hizo, Mwenyekiti amesisitiza mtu ambaye atabainika kufuja pesa hizo zilizochangwa na wananchi, mtu NB ni adui na hatakiwi.

No comments:

Post a Comment

Pages