Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa
(NHC), Nehemia Mchechu akizungumza katika Mkutano wa Wadau wa Uendelezaji Milki
uliofanyika jijini leo Dar es Salaam. (Picha na Francis Dande)
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Angeline Mabula akifungua Mkutano wa Wadau wa Uendelezaji Milki
uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Washika dau.
Wakifuatilia mkutano huo.
Wadau wakiwa katika mkutano huo.
NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imewataka waendelezaji milki kote nchini
kuzingatia sheria wanapokuwa katika ujenzi wa majengo mbalimbali.
Hayo yalielezwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi, Angela Mabula, alipokuwa akifungua mkutano wa wadau wa
uendelezaji milki uliofanyika Julai 12, mwaka huu, makao makuu ya Shirika la
Nyumba la Taifa, jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri huyo aliwakumbusha wajumbe wa mkutano huo kuwa
waendelezaji milki wengi hapa nchini wamekuwa wakifanya shughuli zao bila
kuzingatia sheria, hususan Sheria ya Ardhi Sura ya 13; Sheria ya Mipango Miji
Na. 8 ya mwaka 2007 pamoja na Sheria ya Umilki wa Sehenmu ya Jengo Na. 16 ya
mwaka 2008, hivyo kuwataka kila mmoja kuziheshimu.
“Wengine hubadili matumizi au kujenga majengo marefu zaidi ya kiwango kilichoidhinishwa
kwenye vibali vya ujenzi bila idhini ya
mamlaka husika. Pia wapo ambao hutumia vifaa duni vya ujenzi au hupunguza
viwango kwa makusudi kwa lengo la kujiongezea faida na hatimaye husababisha maafa. Hali Hii pia
husababisha migogoro na hasara ambazo zingeweza kuepukika. Aidha,
husababisha miji mingi kuendelezwa
katika hali isiyopendeza,” alitahadharisha Angela.
Naibu waziri huyo alizitaka
halmashauri na mamlaka zote za usimamizi wa waendelezaji milki hapa nchini kuhakikisha
zinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Aidha, alizihimiza mamlaka hizo kuongeza kasi ya usimamizi
na utekelezaji wa miundiombinu na
kuzitaka halmashauri kutoa hatimilki za ardhi na vibali vya ujenzi kwa wakati bila kusahau jukumu lao
la kusimamia na kukagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi.
Vilevile aliwapongeza
wajumbe hao kwa nia yao ya
kuanzisha umoja ili kuwa na sauti moja
na yenye nguvu, kwa kuanzisha chama ambacho kitatambulika kisheria, ambacho
kitawakilisha na kutetea masilahi yao, kusimamia maadili yao na kushawishi
wanachama kuzingatia sheria na
kushindana kibiashara ndani ya misingi
ya ushindani ulio sawa.



No comments:
Post a Comment