HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 13, 2016

WALIOUWA ASKARI MBANDE WAUWAWA NA POLISI KATIKA MAJIBIZANO YA RISASI

Na Mwandishi Wetu

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limewauwa majambazi wanne  wanaodaiwa kuhusika kwenye tukio la mauwaji ya  askari Polisi wanne waliokuwa lindo katika Benki ya CRDB Mbande.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo Kamishina Simon Sirro, alisema Majambazi hao waliuwawa wakati majibizano  ya risasi ya ana kwa ana na Askari kwenye Pori la Dondwe katika mpaka wa Chanika na Mkoa wa Pwani.

Alisema awali Kikosi maalumu cha kupamba na ujambazi wa kutumia silaha kilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja baada ya kupata taarifa kutoka kwa raia wema kuwa ni jambazi na ndiye aliyehusika kwenye tukio la mauaji ya askari lililotokea huko Mbande Agosti mwaka huu.

Aliongeza kuwa baada ya kumkamatwa mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na tukio hilo akiwa na wenzie saba, hivyo aliwaambia askari kwamba anawapeleka sehemu walipo wenzake huko kwenye pori la Dondwe ambapo hufanyia mazoezi ya kivita.

Sirro alisema walipofika eneo la mipakani huko Chanika kwenye pori hilo ghafla majambazi hayo yalianza kufyatua risasi uelekeo wa askari, askari walilala chini na mtuhumiwa aliyeongozana nao akapata nafasi ya kukimbia.

“Baada ya hapo askari wetu walijibu mashambulizi na mapambano yalidumu kwa dakika kadhaa na askari walifanikiwa kupata bunduki ya kijeshi aina ya SMG iliyofutwa namba za usajili ikiwa na risasi 22 ndani ya magazine” aliongeza

“Majeruhi hao wakiwa mahututi walikimbizwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, wakati wanapatiwa matibabu kwa bahati mbaya wote walifariki kutokana na majeraha ya risasi” alisema Sirro.

Pia alisema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa bunduki hiyo ndio iliyoporwa kwa askari wakiwa wanabadilishana lindo katioka benki ya CRDB Mbande.

Hata hivyo jeshi la polisi kanda hiyo limewakamata  panya road 10, waliohusika na matukio mbalimbali ya uporaji ikiwamo kupora simu na mikoba ya akina mama.

Wakisimulia jinsi walivyokuwa wakifanya uhalifu huo vijana hao walisema kutengana kwa wazazi na maisha duni ndio chanzo cha wao kudanganyika na kujiunga na vikundi vya uhalifu.

Mmoja wa vijana hao Elias Gerald ‘Kulwa’ alisema baba na mama yake walitengana miaka kadhaa iliyopita na kuongeza kuwa wamekuwa hawapati fedha za kujikimu hali iliyomfanya ajiunge na vikundi vya uporaji katika maeneo ya Serenge, Sabasaba, Kiburugwa na maeneo mengine.

Naye Frank Jumanne ‘Chura’ alisema alikuwa akifanya uporaji katika maeneo ya Kauzu mbaya na maeneo mengine ya jirani lengo likiwa ni kupata fedha za kujikimu ambapo wote walisema wameacha na kuamua kulisaidia jeshi la polisi kupamba na vikundi kama hivyo. 

Katika hatua nyingine Jeshi hilo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), limekamata Madumu 453 ya mafuta ya kula yenye lebo ya Safi na Oku yakiwa na ujazo wa lita 20 ambayo yamekwepa kodi na hayajathibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Kamanda Sirro alisema mafuta hayo yenye thamani ya zaidi ya Mil.  14 yalikamatwa Tabata Ubaya Ubaya kwenye nyumba ya Mtuhumiwa Proches Shayo, ambapo mtuhumiwa alishindwa kuthibitisha uhalali wa umiliki wa mafuta hayo kwa kushindwa kutoa nyaraka muhimu.

Akizungumzia Suala hilo Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano na Elimu kwa Mlipa kodi wa TRA, Richard Kayombo alisema mamlaka hiyo  itachukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kutaifisha, kugawa kwa wananchi, kunadi sokoni au kuyateketeza endapo yatabainika kuwa hayafai kwa matumizi ya binadamu.

Pia amewataka wananchi wanaokaa karibu na Bahari ya Hindi na kando ya Ziwa kutoa taarifa za matukio kama hayo ili kudhibiti wakwepa kodi na kulinda afya ya mlaji.

No comments:

Post a Comment

Pages