Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya sala ya Ijumaa kwenye Msikiti wa Kichangani, Magomeni jijini Dar es salaam Novemba 18, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Waislamu nchini waendelee kushirikiana na Serikali kulinda na kudumisha amani na utulivu uliopo nchini.
Aidha, amewasihi waislam kuimarisha umoja ,upendo ,mshimano miongoni mwao kwa kushirikiana na jamii zinazowazunguka bila kujali tofauti zao za kiimani.
Ametoa wito huo leo mchana (Ijumaa, Novemba 18, 2016) wakati akishiriki sala ya Ijumaa katika msikiti wa Kichangani, Magomeni jijini Dar es Salaam.
Amesema uwepo wa dini umewezesha nchi kuendelea kuwa na amani na utulivu hivyo kila mmoja ahakikishe suala hilo linaendelezwa.
Pia amewashauri waumini na viongozi wa dini kuzingatia maadili ya dini ili kuepusha migongano isiyo ya lazima hasa taasisi zinapokuwa na miradi.
Waziri Mkuu alitolea mfano msikiti huo wa Kichangani chini ya Sheikh Walid umeweza kusuluhisha hitilafu wenyewe bila kukimbilia Serikalini au mahakamani kusuluhishwa.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Waislamu wana jukumu la kuwafunza elimu ya dini watoto wao na kuhakikisha wanakua kwenye imani na kujengeka katika maadili mema.
Amesema dini inajenga maadili mema kwa mtoto na kumwezesha kukua katika misingi ya uvumilivu na inamuwezesha kumtambua Mwenyezi Mungu.
“Nimefarijika kuona vijana wengi wameshiriki katika sala hii ya Ijumaa. Nawaomba wazazi waendelee kuelimisha watoto umuhimu wa kufanya ibada,” amesema.
“Tuendelee kuwafundisha vijana wetu umuhimu wa kushiriki kikamilifu kwenye masuala ya kidini ili wakikua waweze kuiendeleza kwa vizazi vijavyo,” amesema.
Waziri Mkuu amewaomba waumini hao waendelee kuwaombea viongozi wa kitaifa ili waweze kutekeleza vizuri majukumu yao na kufikia malengo yanayotarajiwa na wananchi.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
IJUMAA, NOVEMBA 18, 2016.
No comments:
Post a Comment