HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 03, 2016

MWAMUZI WA KIKE TANZANIA KUCHEZESHA AFCON YA KINAMAMA

Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF), limemteua Jonesia Rukyaaa - Mwamuzi wa soka kutoka Tanzania kuwa miongoni mwa waamuzi wa kati 10 watakaochezesha mechi za Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake zitakazofanyika kwa wiki mbili kuanzia Novemba 19, mwaka huu.
Kwa uteuzi huo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), amempigia simu Jonesia kumpongeza kwa hatua hiyo ambayo ni sehemu kubwa ya mafanikio ya soka la Tanzania kufanya vema katika medani za kimataifa.

Rais Malinzi amesema kwamba Mwamuzi Jonesia ameliletea heshima taifa la Tanzania kwa kujijengea heshima ya kuaminika mbele ya Kamati ya Ufundi ya CAF – Waratibu na Waandaaji wa fainali hizo zitakazofanyika Cemaroon ambako mechi za mechi ya mwisho ya fainali itafanyika Desemba 3, mwaka huu.
“Namtakia kila la kheri, naamini kwamba Jonesia atafanya vema. Nina uhakika kwamba hii ndiyo njia yake pekee ya kufanikiwa zaidi kwani ipo siku atateuliwa kuchezesha hata fainali za Kombe la Dunia,” yalikuwa ni maneno ya Malinzi akimwelezea Jonesia kwenye simu leo mchana.
Jonesia anafanya idadi ya waamuzi watakaochezesha mchezo huo kutoka nchi za Afrika Mashariki kuwa watano kwani wengine kwa mujibu wa orodha ya CAF ni  Salma Mukansanga (Rwanda), Lydia Tafesse (Ethiopia), Carolyne Wanjala (Kenya) na Suan Ratunga (Burundi).
Waamuzi wengine ni Maria Packuita wa Mauritius, Gladys Lengwe (Zambia), Akhona Zennith Makalima (Afrika Kusini), Jeanne Ekoumou (Cameroon) na Aissata Amegee (Togo). Katika orodha hiyo pia yumo Mary Njoroge wa Kenya ambaye mwamuzi wa pembeni pekee.
Katika fainali hizo, timu shiriki ni Cameroon, Afrika Kusini, Misri na Zimbabwe zipo kundi A wakati Nigeria, Ghana, Kenya na Mali zimo kundi B.
Jonesia ambaye jana Jumanne alirejea kutoka Cameroon kwenye kozi ya uamuzi ngazi ya juu, kesho Alhamisi anatarajiwa kuwa mwamuzi wa kati kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pale Mtibwa Sugar ya Morogoro itakapokaribishwa na Mwadui kwenye Uwanja wa Mwadui. Mchezo mwingine utakuwa ni kati ya Mbao Fc na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.

No comments:

Post a Comment

Pages