HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 19, 2016

BOSI WA JAMII FORUM AACHIWA KWA DHAMANA

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mtendaji wa Mtandao wa Jamii Forum, Maxence Melo (40) ameachiwa kwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, huku akiwatoa hofu watumiaji wa mtandao huo kuwa upo salama na hakuna taarifa ambazo zitadukuliwa.

Kuachiwa kwa Melo kuna kuja ikiwa ni siku saba baada ya kusota lumande tangu alipokamatwa na Jeshi la PolisiDesemba 13 na kufikishwa mahakamani Desemba 16 mwaka huu na kusomewa mashtaka manne kwa mahakimu watatu tofauti.

Melo aliyasema hayo baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh. Milioni kwa kila mmoja mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa.
.
Akizungumza na waaandishi wa habari, Melo alisema anashukuru jamii ya mitandao na vyombo vya habari kutokana na kuibua mijadala iliyoishinikiza serikali imuachie kwa dhamana.

Alisema hatua ya kufikishwa mahakamani ilitokana na msimamo wake wa kulinda siri za watumiaji wa mtandao huo wa Jamii Forum ambao Polisi walitaka kuudukua.

“Muelewe kuwa kufikishwa kwangu mahakamani ni mfano tu, kwani mshishangae mkaona wengine wanafikisha lakini hatupaswi kuhofia wala kuogopa kikubwa ni kulinda siri za watumiaji wa mitandao,” alisema.

Pia Melo alisema kuwa waandishi wa habari wanapaswa kupambania uhuru wa kujieleza ambao upo kwenye hatari kubwa ya kuangamizwa, kutokana na sheria mpya ya mitandao kuwa kandamizi.

“Hivyo kukamatwa kwangu ni kama shambulizi kwa Uhuru wa vyombo vya habari, hii ndio mara ya kwanza mtu kuwekwa ndani kwa kulinda uhuru wa kuongea, Hivyo hii…ni ishara mbaya sana kwa waandishi wa habari,” alisema.
Mbali na hilo, pia alieleza kuwa anawahakikishia watumiaji wa mtandao wa Jamii Forum kwamba upo salama na hakuna taarifa zozote zilizochukuliwa wala zitakazochukuliwa na mtu yoyote.

“Sina maana kama tunaipinga serikali, isipokuwa tunapinga sheria dharimu ya ukandamizaji ambayo tukiendelea kuiachia itatuangamiza wote ikiwe kama ilivyoanza na mimi,” alisema.

Mahakamani

Jana mbele ya Hakimu Mkazi, Godfrey Mwambapa wakili wa Serikali Mwandamizi, Salum Mohammed alieleza shauri hilo la Melo namba 457 la mwaka 2016 limetajwa kwa ajili ya kukamilishwa kwa masharti ya dhamana.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mwambapa alisema mshtakiwa huyo anapaswa kukamilisha masharti ya kuwa wadhamini wawili watakaosahini bondi ya Sh.milioni 5 kwa kila mmoja. Melo alitimiza masharti hayo na kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 29, mwaka huu.

Katika kesi hiyo ambayo Melo anatetewa na Wakili Jebra Kambole na Jeremiha Ntobesya, Wakili Mohammed alidai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kosa moja la kuzuia taarifa za upelelezi.

Inadaiwa mshtakiwa alitenda kosa hilo katika tarehe tofauti kati ya Aprili 1 na Desemba 13, mwaka huu kinyume na kifungu 22 (2) cha sheria ya mitandao namba 14 ya mwaka 2015.

Inaelezwa kuwa kosa hilo alilitenda maeneo ya Mikocheni wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media inayoendesha mtandao wa Jamiiforum, akijua kuwa Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa makosa ya chapisho za taarifa za mtandao wa elektroniki kupitia tovuti yake, alishindwa na alizuia upelelezi wa tovuti hiyo.Baada ya kusomewa shtaka hilo, Melo alilikana.

Mbali ya kesi hiyo, pia Melo anakabiliwa na kesi nyingine ya kuzuia upelelezi kwa jeshi la polisi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Thomas  Simba.

Inadaiwa alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti kati ya Aprili 1 na Desemba 13, mwaka huu katika maeneo ya Mikocheni wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam. Inaelezwa kuwa akijua kuwa Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa makosa ya chapisho za taarifa za mtandao wa elektroniki kupitia tovuti yake, alishindwa na alizuia upelelezi wa tovuti hiyo.

Katika kesi hiyo, Melo alikana kosa hilo na kupewa masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh.milioni 10 kwa kila mmoja, ambayo aliyatimiza.
Pia katika kesi nyingine namba 458 ya mwaka 2016, Melo anakabiliwa na makosa mawili likiwemo la kuendesha mtandao usiosajiliwa nchini mbele ya Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa.

Inadaiwa kosa la kumiliki mtandao ambao haujasajiliwa nchini, ambapo inadaiwa alilitenda Desemba 9 na 13 mwaka huu katika maeneo ya Mikocheni Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Inadaiwa akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media Co. Ltd iliusajili mtandao huo chini ya kifungu 212 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002 uliopewa cheti namba 66333, ambapo anaendesha tovuti ya Jamii Forums.com bila kusajiliwa nchini kwa mujibu wa sheria za mtandao(Tanzanian Country code Top Level Domain-ccTLD) na masuala ya Posta.

Pia kosa jingine la kuzuia upelelezi kwa Jeshi la Polisi, inadaiwa alilitenda Januari 26 na 13 mwaka huu, ambapo akiwa Mkurugenzi wa Jamii Media Co Ltd unaoendesha mtandao wa Jamiiforums, akijua kwamba Jeshi la Polisi lipo kwenye uchunguzi wa makosa ya kimtandao zilizochapishwa kwenye tovuti yake, kinyume na sheria alishindwa kutoa ushirikiano na kuzizuia taarifa za mtandao huo.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, Melo alikana kuhusika na kosa hilo na kuachiwa kwa dhamana ya kuwa na wadhamini wawili waliosaini bondi ya Sh.milioni moja kwa kila mmoja.
 Mshtakiwa wa kesi ya kuzuia taarifa ya upelelezi wa Jeshi la Polisi na kuendesha mtandao ambao haujasajiliwa Tanzania, Maxence Melo akisindikizwa na askari Magereza wakati akiingia katika ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo. (Picha na Habari Mseto Blog).
 Melo akiingia Mahakamani.
 Melo akipanda ngazi kuelekea mahakamani.
 Akiingia mahakamani.
 Melo
 Wapigapicha wakichukua tukio hilo.
 Melo akitoka baada ya kupata dhamana.
 Mshtakiwa wa kesi ya kuzuia taarifa ya upelelezi wa Jeshi la Polisi na kuendesha mtandao ambao haujasajiliwa Tanzania, Maxence Melo (katikati), akitoka katika ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo baada ya kukamilisha masharti ya dhamana.

Melo akizungumza na mawakili wake wakati akitoka mahakamani.

No comments:

Post a Comment

Pages