WAKILI maarufu na
kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Avod
Mmanda ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara
huku nafasi ya Hamphrey Polepole katika Wilaya ya Ubungo ikizibwa na Kisare
Makori.
Makori amechukua
nafasi ya Polepole ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri
Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC), Itikadi na Uenezi ya CCM ikiwa ni miezi
michache tu tangu aitumikie nafasi hiyo ya Ukuu wa Wilaya.
Taarifa
iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Balozi Kiongozi John Kijazi alisema kwamba rais John Magufuli
amefanya uteuzi wa Wakuu wa Wilaya 2 na
Wakurugenzi 3 wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Wakili Mmanda
amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Khatib Kazungu ambaye hivi karibuni Rais Magufuli
alimteua kuwa Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara ya Fedha na Mipango.
Alisema mbali na uteuzi huo wa Wakuu wa Wilaya hizo pia Rais Magufuli
alimteua Ramadhan Geodrey Mwangulumbi kuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Manispaa ya Shinyanga, akichukua nafasi ya Lewis Kalinjuna
ambaye anastaafu kwa mujibu wa Sheria.
Pia Rais alimteua Rojas Romuli kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda iliyopo katika Mkoa wa Katavi akichukua nafasi
ya Ngalinda Hawamu Ahmada aliyefariki dunia na Rashid Gembe akiteuliwa kuwa Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga iliyopo katika Mkoa wa Tanga.
Gembe anachukua
nafasi iliyoachwa wazi na Mkumbo Barnabas ambaye uteuzi wake ulitenguliwa hivi
karibuni.
Alisema uteuzi huo
unaanza mara moja na kuwataka wateule
wote kuripoti Makao Makuu ya Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) mara wapatapo taarifa.
Mbali na uteuzi wa Wakuu wa Wilaya na Makatibu Tawala
uliofanyika jana pia Rais Magufuli alifanya uteuzi wa Wenyeviti 7 wa Bodi za Taasisi za Serikali
na kumteua Mhandisi Christopher Chiza Aliyewahi kuwa Waziri wa Kilimo, Chakula
na Ushirika katika Serikali ya awamu ya nne.
Chiza aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi
wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) huku Ali Mufuruki aliteuliwa
kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Dhamana ya Hifadhi ya
Mazingira.
Pia Rais Magufuli alimteua Peter Maduki kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), Yamungu Kayandabila kuwa Mwenyekiti wa
Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).
Aidha alimteua Godwin Mjema kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Kampuni ya Huduma za Fedha na Mikopo (UTT-MFI),Ernest Bupamba kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya
Chuo cha Bahari (DMI) na Aloyce Hepelwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya
Miradi ya Maendeleo ya Miundombinu (UTT-PID).
Katika uteuzi huo pia Rais Magufuli alimteua John Jingu
kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uwezeshaji wananchi Kiuchumi Tanzania, Rashid Tamatama
kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) na Zuhura Muro
kuwa Mjumbe wa Baraza la Taifa la Biashara (Tanzania National Business Council
- TNBC).
Mwishoo
No comments:
Post a Comment