HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 21, 2017

BARABARA YA NJOMBE-MAKETE KUJENGWA KWA KIWANGO CHA LAMI-MAJALIWA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika mwaka huu wa fedha Serikali imetenga sh. bilioni 19 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Njombe-Makete yenye urefu wa kilomita 109.4 kwa kiwango cha lami.

Ametoa kauli hiyo jana  (Ijumaa, Januari 20, 2017) wakati akizungumza na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete alipowasili katika kata ya Mtamba wilayani hapa akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Njombe.

Waziri Mkuu amesema usanifu wa kina wa barabara ya Njombe-Makete kwa ujenzi wa kiwango cha lami umekamilika hivyo amewataka wananchi waendelee kuwa na subira.

Amesema barabara nyingine inayotarajiwa kujengwa ni ya kutoka Makete hadi Mbeya kupitia Isyonji yenye urefu wa kilomita 96 ambayo imetengewa sh. milioni 50 kwa ajili ya kufanyiwa usanifu.

Waziri Mkuu amesema wananchi waendelee kushirikiana na Serikali kwani imedhamiria kuwatumikia kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka wahandisi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanawasimamia vizuri wakandarasi wanaojenga miradi mbalimbali katika halmashauri zao kuhakikisha kama viwango vinalingana na thamani halisi ya fedha zinazotolewa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka wakuu wa Idara katika halmashauri kupambana na vitendo vya rushwa na wahakikishe watumishi hawatowi huduma kwa kuomba rushwa.

“Kwanza watumishi watambue kwamba rushwa ni dhambi. Pia kiutumishi ni makosa makubwa hivyo wajiepushe na vitemdo hivyo,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Makete Bi. Veronica Kessy amesema kujengwa kwa barabara hizo kwa kiwango cha lami kutaimarisha ukuaji wa uchumi wa wilaya hiyo na Mkoa wa Njombe kiujumla hivyo wananchi kupata tija.

“Mfano barabara ya kutoka Makete hadi Mbeya kupitia Bulongwa, Iniho, Kikondo na Isyonje itasaidia wilaya kufunguka hivyo kurahisisha usafirishaji wa mazao ya misitu kama mbao,” amesema.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya amesema barabara hii pia itaunganisha Wilaya hiyo na kiwanja cha ndege cha kimataifa cha Songwe hivyo watapata fursa ya kuanzisha kilimo cha maua. Awali walishindwa kulima maua kwa sababu hakukuwa na usafiri wa uhakika.

Awali Waziri Mkuu alitembelea shamba la mifugo la Kitulo linalomilikiwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi lenye jumla ya Ng’ombe 750 wakiwemo ndama 61, majike 212, mitamba 273, madume 21, na madume wadogo 183.

Shamba hilo linazalisha wastani wa lita 450,000 za maziwa kwa mwaka kutokana na ng’ombe 123 wanaokamuliwa. 


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JANUARI 21, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages