Na: Lilian lundo - MAELEZO
Serikali ndiyo yenye mamlaka ya kutangaza ikiwa nchi inakabiliwa na janga la njaa na wala si taasisi, asasi za kiraia au wanasiasa.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Chama cha UDP John Cheyo wakati wa mahojiano na mwandishi wa habari hii alipokuwa akitoa maoni yake kuhusu mijadala mbalimbali inayoendelea katika vyombo mbalimbali vya habari kwamba Tanzania imekabiliwa na tatizo la njaa.
Cheyo alisema kuwa, huwezi kusema nchi ina njaa wakati vyakula vipo katika masoko mbalimbali hapa nchini.
Amewataka watanzania kutofautisha kupanda kwa bei za vyakula na janga la njaa.
Aidha, Cheyo alisema kuwa tatizo hilo tayari limetatuliwa na Serikali kwa kutoa tani milioni 1.5 za mahindi ambazo zitasambazwa nchi nzima kwa ajili ya wananchi kununua.
Aliendelea kwa kusema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa mahindi hayo kuuzwa kwa uangalifu kwani gharama yake itakuwa ni ya chini, hivyo kuna watu ambao watajitokeza kununua kiasi kikubwa na kwenda kukihifadhi kwa ajili ya kukiuza kwa gharama ya juu baadae.
Vile vile aliwataka watanzania kuwa na tabia ya kutunza vyakula badala ya kuuza vyakula vyote mara wanapovuna, ili vyakula hivyo viweze kuwasaidia pale ambapo mvua zinakuwa zimechelewa kama ambavyo imekuwa kwa mwaka huu.
No comments:
Post a Comment