HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 18, 2017

KESI YA LEMA YAAHIRISHWA

Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (Chadema), akiwa na wake, Neema, kwenye  Mahakamani ya Hakimu Mkazi Arusha, baada ya kuahirishwa shauri  la kumtolea Lugha za Kuudhi Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.  (Picha na Grace Macha).
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (Chadema), akiwa na wake, Neema, wakitoka kwenye  Mahakamani ya Hakimu Mkazi Arusha, baada ya kuahirishwa kwa kesi inayowakabili. 
 Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (Chadema), akiwa na wake, Neema, wakitoka kwenye  Mahakamani ya Hakimu Mkazi Arusha, baada ya kuahirishwa kwa kesi inayowakabili. 
 Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (Chadema), akiwapungia mkono wafuasi wake wakati akitoka kwenye  Mahakamani ya Hakimu Mkazi Arusha.

Na Grace Macha


MAWAKILI wa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (CHADEMA),  wameiomba mahakama ya hakimu mkazi Arusha kuhamishia shauri la kuhamasisha watu kuandamana kinyume cha sheria, septemba mosi, mwaka jana lihamishiwe mahakama Kuu likasikilizwe  na majaji watatu kutokana na hati ya mashtaka kujumuisha masuala ya kikatiba.

Ombi hilo llililowasilishwa na Wakili, John Mallya, mbele ya Hakimu Mkazi, Bernad Nganga, anayesikiliza shauri hilo namba 352 ambapo ombi hilo lilisababisha  shahidi wa kwanza  wa Jamhuri,  Mkuu wa Upelelezi mkoani hapa, (RCO), George Katabazi aliyekuwa mahakamani hapo kushindwa kuanza kutoa ushahidi wake kama ilivyokuwa imepangwa.

Wakili Mallya , alisema wanaomba shauri hilo liende mahakama Kuu likasikilizwe na majaji watatu kwani kuna  masuala ya kikatiba kwenye hati ya mashtaka ambayo mashahidi  hawataweza kuyatolea majibu endapo shauri hilo litaendelea kwenye mahakama ya hakimu Mkazi.

"Kuna masuala ya Kikatiba yamejumuishwa kwenye hati ya mashitaka, mashahidi watakapoletwa hapa tukiwauliza masala ya kikatiba hawatakuwa na mamlaka ya kisheria ya kutujibu.

"Shitaka analoshitakiwa nalo mteja wetu, (Lema) linahusiana na masuala ya kisiasa na haki ya mawasiliano ambazo zinalindwa na katiba yetu ibara ya 18 kwenye katiba ya mwaka 1977 inatoa haki kwa mshtakiwa na Watanzania wote kutoa maoni, mawazo,  kuhamasisha  na kufanya maandamano," alisema huku akinukuu vipengele mbalimbali vya katiba kueleza majukumu ya wanasiasa.

Alidai vifungu vya sheria vilivyotumiwa na mwakili wa Serikali kwenye hati ya mashtaka vinakinzana na haki za kikatiba zinazotoa uhuru wa kufanya maandamano na kuhamasishana huku akipinga mteja wao, Lema kushtakiwa kwa kuandamana kinyume cha sheria kabla hata tarehe ya tukio haijafika.

" Hiyo kuandamana kinyume cha sheria isingeweza kuthibitika kabla ya septemba mosi, 2016. wao (Jamhuri)  kwenye hati ya mashtaka wanasema kwenye siku isiyojulikana kati ya Agosti moja na 16, mwaka 2016 Lema alitenda kisa hilo, wanajuaje kama asingefuata taratibu za kisheria za kutoa taarifa polisi," alihoji Mallya.

Alirejea uamuzi wa shauri la Kikatiba namba 32/2016 la Gebra dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, (AG) ambapo alisema kuwa mahakama ilipiga marufuku Jamhuri kuingilia mawasiliano ya watu kwenye mitandao ya jamii.

Kwa upande wake Wakili wa Serikali, Alice Mtenga aliieleza mahakama kuwa shauri hilo si la kikatiba na kusisitiza kuwa mashitaka ni kama yanavyoonekana kwenye hati ya mashitaka huku akiiomba mahakama impr muda wa kuleta hoja za majibu.

Hata hivyo Wakili,  Mallya alipinga ombi hilo la wakili wa Serikali, Mtenga la kutaka kuongezewa muda ili awasilishe hoja za majibu kwa kile alichoieleza mahakama kuwa tayari alishajibu hivyo hakuna sababu ya kuongezewa.

Hakimu Mkazi, Nganga alikubaliana na hoja ya kutokuongezewa muda kwa wakili wa Serikali hivyo kuahirisha shauri hilo mpaka Februari 8, mwaka huu atakapotoa uamuzi endapo shauri hilo likasikilizwe mahakama Kuu na majaji watatu au aendelee kulisikiliza.


Awali  ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Lema alihamasisha watu kufanya maandamano yasiyo na kikomo kuanzia septemba 1, mwaka huu kwa ,ujumbe wa sauti aliousambaza kupitia mtandao 'what's up'.

kuwa Lema anadaiwa kutenda kosa hilo la kuhamasisha watu kutenda kosa katika tarehe  isiyojulikana  kati ya tarehe 1  na 26 Agosti mwaka huu.

"Katika tarehe isiyojulikana kati ya  1/08/2016 na 26/08/2016 mtuhumiwa alitengeneza  nakurekodi ujumbe mfupi wa sauti na kuusambaza kwa mtandao wa 'What's Up" akihamasisha watu kutenda kosa la jinai.

"Kwenye ujumbe huo alikuwa akihamasisha watu kukusanyika na kufanya maandamano yasiyo na kikomo kuanzia tarehe 1/09/2016. Baada ya taarifa hizo kumfikia RCO aliamrisha kukamatwa kwa mtuhumiwa na upelelezi kuanza mara moja," alisema wakili wa Serikali Fortunatus Mhalila.

Lema alikana shitaka hilo huku akidai kuwa ametengeneza na kusambaza jumbe zaidi ya 10 hivyo kwa kuwa hiyo sauti haijaletwa mahakamani hapo hawezi kujua.

Upande wa Jamhuri unatazamia kuleta mahakamani hapo mashahidi watano akiwemo Mkuu wa upelelezi wa mkoa, (RCO), George Katabazi, Mkuu wa upelelezi wilayani Arusha, (OC-CID), Damas Massawe, mpelelezi, Adam Nyamiti, polisi Ester Yohana na Mtaalam,  Ezekike Denis kutoka Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Pages