January 28, 2017

WALIOTAFUNA ZAIDI YA SH. BILIONI 1 ZA USHIRIKA WASHUGHULIKIWE-MAJALIWA

 Baadhi ya watumishi  wa umma , viongozi wa dini na wananchi wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa wakati alipozungumza nao katika kikao cha majumuisho ya ziara yake mkoani Njombe  kwenye ukumbi wa Hlmashauri ya Manispaa hiyo mjini Njombe, Januari 27, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na watumishi wa umma, viongozi wa dini na wananchi katika kikao cha majumuisho ya ziara yake ya mkoa wa Njombe kwenye ukumbi wa manispaa hiyo mjini Njombe, Januari  27, 2017.  Kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo, Christopher Ole Sendeka.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

XXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXXX

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Bw. Christopher Ole Sendeka kuchukua hatua kali kwa wote waliohusika na upotevu zaidi yash. bilioni moja za vyama vya ushirika.

Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Januari 27, 2017) alipozungumza na watumishi wa Mkoa wa Njombe wakati wa majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya siku saba mkoani hapa.

Alisema kati ya fedha hizo sh. milioni 532.736 zilipotea katika SACCOS ya Kurugenzi  Njombe pamoja na sh. milioni 900 zilizopotea katika Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo kiitwacho Wafanyabiashara Njombe SACCOS.

“Maofisa Ushirika nchini mmeendelea kudhoofisha jitihada za Serikali katika kuimarisha ushirika. Katika eneo hili ninahitaji Mkuu wa Mkoa ufuatilie suala hili na kuwachukulia hatua wahusiuka wote,” alisema.

Waziri Mkuu aliwaagiza Wakuu wote wa Wilaya kuwatumia warajisi wa ushirika kuimarisha ushirika Mkoani Njombe.”Tunataka ushirika ulete tija kwa wananchi na hatutaki ushirika ulioambatana na harakati za kugawa watu. Endeleeni kuwashughulikia wanaushirika wasio waaminifu,”.

Aidha, Waziri Mkuu aliwasisitiza watumishi wa umma wote nchini kuzingatia uadilifu, uaminifu, kutojihusisha na rushwa na kutumia ipasavyo fedha za umma Serikali itachukulia hatua kali dhidi ya watumishi wote wanaotumia nafasi zao kujinufaisha binafsi.

Alisema anataarifa za Watendaji wa Wakuu wa Wilaya ya Makete akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw. Francis Namsumbo, Mweka Hazina Bw. Edward Mdagachule, Ofisa Utumishi, Bw. Nicodemas Tindwa na Mkaguzi wa Ndani Bw. Michael Shija kuhusika na upotevu wa sh. milioni 71 zikiwemo sh milioni 41 za UNICEF.

Waziri Mkuu alisema kuwa watumishi hao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya utoaji wa rushwa kwa vyombo mbalimbali ili kuficha ubadhilifu huo. “Mkuu wa Mkoa hakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kuhusiana na matukio haya,”.

Pia alimuagiza Mkuu huyo wa Mkoa kuhakikisha kuwa ……..wa Wanging’ombe Bw. Edwin Kigoda anachukuliwa hatua stahiki kwa ubadhilifu wa sh. milioni 37.9 zilizotolewa kwa ajili ya kuwajengea uwezo Walimu katika stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).

Mbali na watumishi hao pia Waziri Mkuu alimtaka Bw. Ole Sendeka kumchunguza na kumchukulia hatua Ofisa Ardhi wa Mji wa Njombe, Bw. Addo Kabange ambaye anatuhumiwa kuuza viwanja mara mbili, kuchukua rushwa na kujipatia viwanja vingi kwa bei nafuu na kuviuza kwa wananchi kwa bei ya juu.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alisema atawaelekeza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG), Msajili wa Hazina na Mrajisi wa Ushirika kuanza kufuatilia malalamiko kuhusu umiliki wa kiwanda cha chai cha Lupembe pamoja na kufuatilia mwenendo wa mgawanyo wa hisa za kiwanda hicho.

Alisema alipotembelea kiwanda cha chai cha Lupembe ambapo alifarijika kukuta kiwanda hicho kimeanza kufanya kazi baada ya kusimama kwa takriban miaka nane kutokana na mgogoro uliopo baina ya mwekezaji wa Kiwanda hicho na Umoja wa Wakulima wa Chai Muvyulu.

Waziri Mkuu alisisitiza kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haitavumilia migogoro ya kuzuia ajira kwa wananchi, hivyo aliahidi kushughulikia malalamiko kutoka pande hizo mbili na kutafuta njia ya kutatua mgogoro uliopo.

Alisema baada ya kusomewa taarifa ya kiwanda na kwa upande mwingine taarifa ya wanaushirika alibaini kuwepo kwa mgogoro unaohitaji kutatuliwa ili kuwezesha shughuli za kiwanda kuendelea kwa amani na usalama.

Aidha, Waziri Mkuu alielekeza shughuli za ulimaji na uvunaji wa majani ya chai kutoka kwa wakulima na kupeleka katika kiwanda hicho iendelee na kiwanda kisisimamishe kazi ili kulinda soko la wakulima na ajira za watumishi wa kiwanda hicho,” alisema.

Alisema kwa kuwa kiwanda hicho kinamilikiwa kwa ubia, alimwelekeza Mkurugenzi wa kiwanda hicho kuhakikisha kuwa wanaweka wawakilishi wawili au watatu wa wanaushirika katika Bodi ya Kiwanda hicho.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alizungumzia suala la kuchelewa kuanza kwa mradi wa chuma cha Liganga, ambapo alisema ucheleweshaji huo si wa makusudi bali ni mpango wa Serikali wa kujiridhisha na vipengele mbalimbali vya mkataba ili uwe wa manufaa kwa Watanzania.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema baada ya kutembelea eneo ambalo uchimbaji utakapofanyika, na kujionea maendelezo ya wananchi yaliyopo, alipata mashaka na kiasi cha sh. bilioni 13 kilichotengwa na wawekezaji kwa ajili ya fidia kwa wananchi watakaopisha mradi huo.

Alisema Serikali haina budi kufanya tathmini ya kina na kujiridhisha. “Nataka nimkumbushe Mheshimiwa Mbunge (Deo Ngalawa-Ludewa) na Mwenyekiti wa NDC kujiridhisha na wahusika wanaotarajiwa kupata fidia hiyo,”.

Akizungumzia kuhusu maslahi ya watumishi, Waziri Mkuu alisema Serikali kupitia Bodi ya Motisha na Mishahara inaendelea kufanya tathmini ya uzito wa kazi ili kupanga upya viwango vya motisha na mshahara kwa watumishi wote.

Pia aliwasisitiza waajiri wote wakiwemo Wakurugenzi kutenga fedha kwa ajili ya likizo, masomo na uhamisho, kuandaa leave roster na mipango ya mafunzo kwa watumishi.

       
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, JANUARI 28, 2017.

No comments:

Post a Comment

Pages