Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli, akimkabidhi vyakula kwa ajili ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani pamoja na Sikukuu ya Eid el Fitr, Mkuu wa Kituo cha New Life Orphanage cha Boko, Hajat Mwanaisha Magambo, kwa niaba ya viongozi wa vituo vinane vya kulelea yatima na watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu jijini Dar es Salaam. (Picha na Ikulu).
Na Jacquiline Mrisho–MAELEZO
Mke wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Janeth Magufuli ametoa msaada wa futari kwa vituo nane vya watoto yatima vilivyopo Jijini Dar es Salaam mahsusi kwa ajili ya kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani.
Mama Magufuli ametoa msaada huo leo Jijini hapa kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu vikiwemo vya Newlife, Charambe Islamic Centre, Chakuwama, Mwandaliwa Yatima Centre, Al Madina Children Home, Alzam Orphanage Centre, Hiari Orphanage Centre pamoja na Ijangozaidia Orphanage Centre.
Aidha alisema kuwa msaada huo alioutoa umejumuisha Sukari mifuko 100 yenye jumla ya Kilogramu 2000, Mchele mifuko 40 yenye jumla ya Kilogramu 2000 pamoja na Tende pakiti 100 zenye jumla ya Kilogramu 800.
“Ninayo furaha kuweza kuwasaidia zaidi ya watoto yatima 600 ambao wamenuia kufunga katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani ikiwa ni muendelezo wa huduma za kujitolea kwa jamii kwa kuwasaidia watoto wanaoishi katika vituo vya kulelea Watoto yatima”, alisema Mama Magufuli.
Mke huyo wa Rais alifafanua kuwa kituo cha Newlife chenye watoto 121 kimepewa Mchele kilo 363, Sukari Kilo 363 na Tende Kilo 144, Charambe Islamic Centre chenye Watoto 54 kimepewa Mchele Kilo 162, Sukari Kilo 162 na Tende Kilo 64, Chakuwama chenye Watoto 64 kimepewa Mchele Kilo 192, Sukari Kilo 192 na Tende Kilo 64 na Al Madina Children Home chenye Watoto 65 kimepewa Mchele Kilo 195, Sukari Kilo 195 na Tende Kilo 64 .
Vituo vingine ni Mwandaliwa Yatima Centre chenye Watoto 94 kimepewa Mchele Kilo 282, Sukari Kilo 282 na Tende Kilo 64, Alzam Orphanage Centre chenye Watoto 51 kimepewa Mchele Kilo 153, Sukari Kilo 153 na Tende Kilo 64, Hiari Orphanage Centre chenye Watoto 41 kimepewa Mchele Kilo 123, Sukari Kilo 123 na Tende Kilo 40 pamoja na Ijangozaidia Orphanage Centre chenye Watoto 103 kimepewa Mchele Kilo 309, Sukari Kilo 309 na Tende Kilo 104.
Kwa upande wake mwakilishi wa viongozi wa vituo vya kulelea watoto yatima, Mama Kuluthum Juma alisema kulea watoto yatima si jambo la mtu mmoja au Serikali peke yake hivyo ni lazima wananchi wote wajumuike katika kuwasaidia watoto hao kwa hali na mali ili wajione kuwa wako sawa na Watoto wengine wanaoishi na wazazi wao.
“Tunamshkuru sana Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli kwani msaada huu alioutoa kwetu sio mdogo na hakuna kitu kikubwa kama kutoa sadaka hivyo natoa rai kwa wananchi tujitahidi kuwasaidia na kuwafariji Watoto hawa kwa sababu ni Watoto wa watu wote na hakuna aliyependa kuwa hivyo alivyo,” alisema Mama Kuluthumu.
Misaada kwa Watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu ni muendelezo wa huduma za kujitolea kwa Jamii anazofanya Mke wa Rais ambazo hufanyika kila mwaka.
No comments:
Post a Comment