Usajili
wa timu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Ligi Daraja la Kwanza na
Ligi Daraja la Pili kwa msimu wa 2017/18, umekamilika kwa timu 62 tu na
timu mbili zimeshindwa kufanya usajili.
Tayari
toleo la awali (First Draft) la majina ya timu zote na namna
zilivyosajili, tumebandika katika mbao za matangazo za Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Karume Dar es Salaam tangu jana kadhalika
nimeunganisha (attach) usajili huo kwenye taarifa hii kwa vyombo vya
habari kwa timu zote kwa kufuata alphabeti.
Kubandikwa
huko na kusambaza kwenye vyombo vya habari kunalenga kuwapa fursa timu
zote kukagua majina ya wachezaji wa kila timu ili kuona kama kuna klabu
au mchezaji amefanya udanganyifu wa kusajili wa timu zaidi ya moja,
ziweze kuona.
Kama
kuna dosari hiyo, TFF imefungua milango ya kupokea pingamizi la usajili
wa wachezaji hao kuanzia leo Agosti 8, 2017 hadi Jumatatu Agosti 14,
mwaka huu saa 10.00 jioni (16h00).
Kamati
ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji inatarajiwa kuwa na kikao ama
Agosti 16 au 17, mwaka huu kupitia mapingamizi hayo pamoja na usajili wa
timu za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. Usajili wa timu za Daraja la
Kwanza na Pili, utapitiwa baadaye mwezi huu.
Timu
hizo 62 kati ya 64 zimefanya usajili na kuingiza majina ya wachezaji,
viongozi wa benchi la ufundi kwenye mfumo wa mtandao wa TMS - Transfer
Matching System.
Timu
ambazo zimeshindwa kufanya hivyo yaani usajili kwa mfumo wa TMS ni za
Ligi Daraja la Pili (SDL) ambazo ni Pepsi ya Arusha na Bulyanhulu ya
Shinyanga.
Na
kwa msingi huo, timu hizo za Pepsi na Bulyanhulu zimejitoa kushiriki
ligi kwa msimu wa 2017/18 na zinashushwa daraja hadi ligi ya wilaya
kuanza upya kutafuta nafasi za juu kupanda daraja.
……………………………………………………………………………… ……….
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
No comments:
Post a Comment