WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,
Dkt Steven Kebwe na kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa kwenda katika kijiji cha
Maseyu kufuatilia utendaji wa kampuni ya Zhong Fenq kama inafuata sheria,
kanuni na taratibu za nchi.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Septemba 2, 2017),
wakati akizungumza na viongozi na watumishi wa kiwanda cha Philp Morris kinachotengeneza
sigara aina ya Marlboro akiwa katika
ziara yake ya kukagua maendeleo ya viwanda mkoani Morogoro.
Agizo hilo limefuatia malalamiko ya mbunge wa Morogoro Kusini
Mashariki Mheshimiwa Omary Mgumba kuwa wawekezaji hao kutoka China wanaendesha shughuli
za uchimbaji wa mabo katika kijiji cha Maseyu wilayani Morogoro bila ya kuwa na
kibali.
Mheshimiwa mgumba amesema tangu mwaka 2011 wawekezaji hao
wameendesha shughuli zao bila kulipa
kodi za Serikali na tozo za Halmashauri, hivyo kuikosesha Serikali mapato.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu katika kijiji cha Maseyu kuna Wachina wa
kampini ya Zhong Fenq wanachimba mabo na hawana kibali na hakuna kodi yoyote
wanayolipa Serikalini tangu mwaka 2010 walipoanza uzalishaji.”
Mbunge huyo ambaye machimbo hayo yako jimboni kwake aliongeza
kwamba licha ya uongozi wa mkoa kwenda katika eneo hilo na kuizuia kampuni
kuendelea na uchimbaji hadi itakapopata vibali walikaidi na kuendelea na
shughuli.
Waziri Mkuu amesema hakuna muwekezaji anayeruhusiwa kufanya kazi
bila ya kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi. Hivyo ameagiza kesho Mkuu
wa Mkoa afuatilie Wachina hao na kuona namna gani wamezingatia sheria za nchi.
Amesema iwapo watabaini kwamba wawekezaji hao hawajafuata sheria, kanuni na taratibu hatua zichukuliwe
dhidi yao ikiwa ni pamoja na kuwaondoa katika eneo hilo chini ya ulinzi na
kuwasiliana na ubalozi wa China Nchini.
Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa watu wote
wenye nia ya kutaka kuwekeza katika miradi mbalimbali nchini Tanzania kuhakikisha
wanafuata sheria, kanuni na taratibu za uwekezaji.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema
ni faraja kuona kiwanda cha Philp Morris kikiwa kimekamilika tayari kwa kuanza
uzalishaji wa sigara aina ya Marlboro hivyo kuwezesha wakulima wa tumbaku nchini
kuwa na soko la uhakika.
Amesema miaka ya nyuma uzalishaji wa tumbaku ulipungua nchini
kutokana na wakulima kukata taama baada ya kukosa soko la uhakika pamoja na
kuchoshwa na ubadhilifu wa mali za ushirika uliokuwa ukifanywa na viongozi wa
vyama vya ushirika wa tumbaku.
Pia Waziri Mkuu alitembelea ujenzi wa kiwanda cha sukari
kilichopo katika Gereza la Mbigiri wilayani Kilosa na kukagua shamba la miwa lenye
ukubwa wa hekta 4,800 ambapo hekta 320 zimelimwa na kati yake hekta 125 tayari zimepandwa
miwa na imeshaota.
Kiwanda hicho kinajengwa kwa ushirikiano wa Jeshi la Magereza na
mifuko ya hifadhi ya Jamii ya NSSF na PPF kupitia mradi wa Mkulazi ambao
unatarajia kuzalisha tani 250,000 za sukari kwa mwaka kati yake tani 50,000
zitazalishwa katika kiwanda cha Mbigiri na tani 200,000 katika kiwanda cha
Ngerengere.
Amesema uwepo wa viwanda nchini utawezesha watanzania kulima
kilimo chenye tija kwa kuwa watauza mazao yao viwandani na mmoja atashiriki
kulima zao ambalo ataliuza katika kiwanda cha jirani.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, SEPTEMBA 2, 2017.
No comments:
Post a Comment