KE wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa amewataka
watoto wanaojiandaa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu, waongeze bidii
kwani dunia ya sasa hivi inataka wasomi.
Mama Majaliwa ametoa wito huo jana (Jumamosi, Septemba
2, 2017) wakati
akizungumza na wahitimu 166 wa darasa la saba wa shule ya msingi ya Martin
Luther, kwenye sherehe za mahafali ya 10 zilizofanyika shuleni hapo katika Manispaa
ya Dodoma.
“Ninawapongeza wanafunzi wanaohitimu lakini
ni lazima mtambue kwamba huu siyo mwishi wa safari yenu ya masomo kwani dunia
ya sasa inataka wasomi. Kwa hiyo, muongeze bidii hadi mfike elimu ya vyuo
vikuu,” alisisitiza.
Aliushukuru uongozi wa shule hiyo na
walimu wote kwa malezi mema wanayoyatoa kwa watoto hao na kwamba mafunzo yao
yanadhihirika miongoni mwa watoto kwa jinsi walivyolelewa kimwili, kiroho na
kiakili.
“Mtoto wangu nilimleta akiwa na miaka
mitano, ameanza elimu ya chekechea na sasa anahitimu darasa la saba. Sasa hivi
amekua na ana hofu ya Mungu, anatambua mema na mabaya, tunawashukuru sana,”
alisema.
Kwa upande
wake, Mwalimu
Mkuu wa shule hiyo, Bw. Gilbert Nhuguti wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji
ya shule, alisema kwa zaidi ya miaka mitano, shule hiyo ambayo ni ya kutwa na
ya bweni, imekuwa na rekodi ya kufanya vizuri kiwilaya na kimkoa kwa kushika
nafasi za kwanza.
“Mwaka jana tulishika nafasi ya kwanza
kimkoa na nafasi ya saba kitaifa kwa wastani wa daraja la ‘A’. Hata mwaka huu,
kwenye mitihani ya majaribio (mock exams) tumeshika nafasi ya kwanza, tumepania
kuchukua nafasi ya kwanza kitaifa katika matokeo ya mwaka huu,” alisema.
Alisema mafanikio hayo yanachangiwa na ubora
wa walimu wa shule hiyo ambao wana shahada, astashahada na stashahada.
Aliwataka wahitimu hao wawe mfano huko
waendako, wamtangulize Mungu katika kila walifanyalo na wasiwe watu wa kutaka
kupata makubwa bila kufanya kazi kwa bidii. “Fanyeni kazi kwa bidii na
mafanikio yatakuja,” alisisitiza. Pia aliwataka waendeleza tabia ya kutunza mazingira popote pale waendapo.
Naye Mbunge wa Mtera, Bw.
Livingstone Lusinde ambaye alipewa nafasi kutoa nasaha kwa niaba ya wazazi,
aliwataka wahitimu hao watambue kuwa wanapohitimu elimu ya msingi wajione kuwa
wamejengewa msingi imara.
“Kuhitimu elimu ya msingi ni sawa na
kujengewa msingi imara wa nyumba. Kwa hiyo, mkauendeleze kwa kujenga matofali
imara, hautakuwa na maana kama mtaujenga kwa kutumia matofali mabovu juu yake,”
alisema.
Wanafunzi wa darasa la saba kote nchini,
wanatarajiwa kufanya mitihani yao ya kitaifa Septemba 6 na 7, mwaka huu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA.
JUMAPILI, SEPTEMBA 3, 2017.
No comments:
Post a Comment