HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 27, 2017

SEKTA YA UVUVI IKIPEWA KIPAUMBELE ITACHANGIA UKUAJI WA UCHUMI-MTAFITI

NA JANETH JOVIN
UTAFITI  wa mwaka 2014 uliofanywa na baadhi ya wataalamu wa masuala ya uvuvi  umeonyesha kuwa licha ya Tanzania kuwa na eneo kubwa la bahari, asilimia 90 ya wavuvi wake wamekuwa wakivua samaki tani 52,000 tu kwa mwaka tofauti na nchi zingine zenye eneo dogo lakini wanavua zaidi ya kiwango hicho.
Akizungumzia  utafiti huo hivi karibuni wakati  akitoa mafunzo kwa waandishi wa Habari juu ya uharibifu wa mazingira kwenye bahari, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM) kutoka Idara ya Sayansi za Maji na Uvuvi, Dk Benaisha Benno alisema utafiti huo umebainisha kuwa hali hiyo inachangiwa na wavuvi kutumia zana duni ambazo haziwezi kufika katika kina kirefu cha bahari kunapopatikana samaki  wengi .
Benno alisema kutokana na kuwepo kwa uhaba wa vitendea kazi kwa wavuvi hao kumepelekea wanavua samaki wachache zaidi na kushindwa kwenda kwenye kina hicho kirefu cha bahari.
“Tungekuwa na zana kubwa na za kisasa tungeweza kufika katika kina kirefu na kupata samaki wengi zaidi ya hao tunaowapata sasa lakini  vifaa vinavyotumiwa na wavuvi wetu  vinawafanya wanashindwa kwenda kuvua  samaki  katika bahari kuu matokeo yake wanashindwa kuvua samaki wakubwa na wengi.
"Samaki wanaovuliwa na wavuvi wetu ni wadogo na uvuliwa sehemu za karibu karibu na sio Kwenye kina cha bahari ambapo ndio upatikana samaki wakubwa zaidi," alisema Dk.Benno
Aidha Dk. Benno aliwataka wavuvi kuacha uvuvi haramu kwani unasababisha uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri), Baraka Kuguru alisema sekta ya uvuvi ikipewa kipaumbele itachangia ukuaji wa uchumi na hivyo kutekeleza malengo ya viwanda na uchumi wa kati.
Kuguru alisema tafiti ziaonyesha kuwa sekta ya uvuvi imekuwa na mchango mkubwa kwa nchi ambazo zimewekeza hasa katika ukanda wa bahari ambapo rasilimali zilizopo kwenye bahari zina thamani ya dola za Marekani 333 bilioni huku uwekezaji ukiwa asilimia 20 mpaka sasa.
Naye Mmoja wa wavuvi wa soko kuu la samaki la Zanzibar, Habibu Othuman  alisema wavuvi wengi hawana sehemu rasmi ya kupata mikopo hivyo anaiomba serikali iwatengenezee mazingira bora yatakayowawezesha kupata mikopo iliyokuwa na na riba nafuu au isiyo nariba kabisaa.
Aidha alisema miongoni mwa changamoto inayowakabili ni ya ukosefu wa boti zenye uwezo wa kuvua samai katika kina kirefu hivyo wanaiomba serikali pia iingie ubia na kampuni kubwa ziweze kutafuta vyombo hivyo vya uvuvi vinavyoweza kufika mbali.
“Serikali iingie  ubia na wawekezaji wakubwa watuletee vyombo hivyo vya kisasa kisha watukopeshe tuone kama tutashindwa kuvua samaki wengi lakini pia tunaziomba benki zije kutupa elimu juu ya umuhimu wa kukopa kwa lengo la kukuza biashara,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages