HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 27, 2017

MAHAFALI YA 25 YA WAKALA WA MAENDELEO YA UONGOZI WA ELIMU YAFANYIKA BAGAMOYO

Baadhi ya wahitimu wa kozi za Stashahada ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu (DEMA) na Stashahada ya Ukaguzi wa Shule  (DSI) wakiwa katika picha ya pamoja katika mahafali ya 25 ya Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu  (ADEM) yaliyofanyika hivi karibuni Bagamoyo mkoani Pwani.
NA JANETH JOVIN
WAKURUGENZI wa Halmashauri za Mikoa na Wilaya wametakiwa kutekeleza kwa vitendo mpango wa Maendeleo Endelevu namba nne  kwa kutoa fursa kwa walimu na watu wote wanaotaka kujiendeleza kielimu.
Hayo yalibainishwa juzi na Katibu Mkuu wa  Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo  kwenye mahafali ya 25 ya Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) yaliyofanyika Bagamoyo mkoani Pwani.
Katika mahafali hayo wanafunzi 736 wamehitimu katika kozi za  Stashahada ya Uongozi na usimamizi wa Elimu (DEMA) na Stashahada ya Ukaguzi wa shule (DSI)
Dk Akwilapo alisema kuwa Dira ya Maendeleo ya  Taifa ya mwaka 2025, ambapo Tanzania imeanza kutekeleza ujenzi wa uchumi wa viwanda, Mkakati wa Kitaifa wa Kupunguza Umasikini na Kukuza Uchumi (MKUKUTA), Sera ya elimu ya mwaka 2014 na Sera ya Kimataifa ya Elimu kwa Wote (EFA) zinatambua umuhimu wa elimu bora katika kuleta maendeleo endelevu.
Alisema maendeleo hayo yatafanikiwa endapo sera zilizowekwa  zitatekelezwa ipasavyo kwa kuwa zinaelekeza utoaji wa elimu kwa wote kwa kutoa fursa kwa wafanyakazi kujiendeleza.
Alisema kuwa wapo baadhi wa waajiri ambao wanawazuia wafanyakazi wao kuendelea na masomo ya elimu ya juu ambapo wanavunja haki yao ya msingi ya kujiendeleza.
''Matarajio ya serikali ni kuona kwamba wahitimu wa kozi zote mrudipo shuleni mnasimamia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo (2014), sheria, kanuni na taratibu za elimu ili kupunguza migogoro shuleni na kudhibiti nidhamu za wanafunzi,'' alisema Dk Akwilapo.
Pia alisema walimu hao wanapaswa kusimamia na kutekeleza mtaala kwa ufanisi mkubwa kwa kutoa takwimu sahihi za shule, kupanga mipango ya maendeleo ya shule inayotekelezeka, kusimamia fedha za elimu bila malipo na rasilimali nyingine.
Aidha, alisema wanatarajia kuona uanzishwaji wa timu za ukaguzi wa ndani ya shule kabla ya wakaguzi wa nje kufika, kufanya tafiti ndogo zinazohusu changamoto mbalimbali ikiwemo mimba za utotoni, utoro uliokithiri na nidhamu mbaya kwa wanafunzi shuleni.
''Mafunzo ya uongozi na usimamizi wa elimu pamoja na ukaguzi wa shuel katika nchi yetu ni muhimu katika kuwapa uwezo waliohitimu na viongozi wa elimu kufanya kazi zao kwa weledi, ufanisi na kwa kujiamii hususani katika kipindi hili cha maendeleo ya sayansi na teknolojia,'' alisema.
Aliongeza kuwa ''wahitimu wanapaswa kuwa chachu ya mabadiliko katika uongozi na utawala bora pamoja na uthibiti ubora wa shule kwa kutumia ujuzi na maarifa mliyoyapata kwa walimu ambao hawajapata fursa hii.''
Kwa mujibu wa Dk Akwilapo, serikali inathamini kazi za kitaaluma zinazofanywa na ADEM katika kusimamia mafunzo kwa walimu wa darasa la tatu na la nne katika kukuza stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) katika mikoa 26 ambapo jumla ya walimu 31,993 walipata mafunzo hayo.
Hata hivyo, alisema walimu wawe rafiki wa utunzaji wa mazingira ili kupambana na majanga mbalimbali, kukataa rushwa, kupambana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na dawa za kulevya ambazo huathiri mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dk Siston Masanja alisema kuwa pamoja na kutoa mafunzo mbalimbali kwa walimu na wakuu wa shule, wanatarajia kuendesha mafunzo kwa walimu wanaofundisha madarasa ya Memkwa wapatao 1,500 na walimu wa darasa la kwanza na la pili 1,600.
Dk Masanja alisema katika kuboresha utendaji kwa walimu, ADEM imefanya mapitio ya mtaala kwa kuongeza baadhi ya masomo ya kufundishia kwa walimu wanaosoma masomo ya uongozi na usimamizi wa elimu kama vile Historia, Jiografia, Hisabati, Kiswahili na stadi zake na Kiingereza.
''Tunaamini kuwa kiongozi mzuri ni yule anayekyuwa na uelewa na umahiri unaohitajika katika kutenda kazi. Kuingiza masomo ya kufundishia katika mtaala kutamsaidia mhitimu wetu kufanya ufuatiliaji na tathmini ya shughuli za ufundishaji kwa weredi mkubwa,'' alisema Dk Masanja.
Hata hivyo, aliomba Wizara hiyo kuwasaidia kutenga fedha kwa ajili ya kukarabati jengo lililokuwa la mapadri, mabweni na kujenga ukumbi wa mhadhara.
Pia alisema waweke sera kwamba uteuzi wowote wa uongozi katika elimu na uthibiti ubora wa shule utokane na taaluma hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages